Sunday, February 5, 2017

IDADI KUBWA YA WAKAZI WA WILAYA YA IGUNGA WAPO HATARINI KUPAMTWA NA MAGONJWA YA SHINIKIZO LA DAMU

Jengo la Ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora kulikofanyikia zoezi la upimaji wa afya kwa watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga,Madiwani wa Halmashaurri hiyo pamoja na wananchi wa Halmashauri waliojiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF).

Na Jumbe Ismailly, Igunga

IDADI kubwa ya wananchi wa Wilaya ya Igunga, Mkoani Tabora wapo hatarini kupatwa na magonjwa ya shinikizo la damu kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kupima afya zao hali ambayo inachangia miili yao kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Dk. Godfrey Mgongo aliyasema hayo wakati wa zoezi la kupima afya kwa watumishi,madiwani pamoja na wananchi ambao ni wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya (NHIF) wa Halmashauri ya wilaya hiyo lililofanyika kwenye viwanja vya Ofisi za Halmashauri hiyo.
 
Baadhi ya wataalamu wa sekta ya afya waliokuwa wakitoa huduma za upimaji afya kwa watumishi wa Halmashauri ya Igunga,Madiwani pamoja na wananchi wa kawaida waliojiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF)ambapo iligundulika kuwa idadi kubwa ya wakazi wake wapo hatarini kupatwa na magonjwa ya shinikizo la damu kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kupima afya zao na hivyo kuchangia miili yao kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi.

“Kitu ambacho tumekigundua ni kwamba watumishi wengi au watu wengi wana uzito uliopitiliza,uzito mkubwa na hii inaweza ikapelekea ukapata magonjwa ambayo yatawaathiri katika maisha yao”alisema Dk.Mgongo.

Hata hivyo mganga mkuu huyo wa wilaya alivitaja vitu vilivyopimwa na wataalamu hao kutoka shirikisho la vyama vya magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza(TANCDA) kuwa ni uzito,shinikizo la damu,homa ya ini pamoja na kisukari na zoezi hilo limefanyika kwa siku nne ambapo lilianza kwa watumishi wa Halmashauri na baadaye huduma hiyo ilielekezwa kwa madiwani pamoja na wananchi.
 
Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora wakiwa kwenye mkutano wa Baraza la kawaida la madiwani wa Halmashauri hiyo ambalo lilitumika pia kushiriki katika zoezi la upimaji afya kwa waliojiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF).(Picha Na Jumbe Ismailly)

Kwa mujibu wa Dk.Mgongo kati ya zaidi ya watumishi 60 wa Halmashauri hiyo waliopatiwa huduma ya upimaji wa afya, imegundulika kuwa tatizo kubwa linalowakabili watumishi hao ni uzito ingawa kuna tatizo la homa ya ini na ugonjwa wa kisukari ndiyo unaofuatia.

“Lakini pia kwa waheshimiwa Madiwani kuanzia asubuhi mpaka sasa wameshapimwa madiwani 61 na imegundulika kwamba robo tatu ya waliopima wanakabiliwa na tatizo la kuwa na uzito mkubwa kupitiliza,kisukari na homa ya ini vina asilimia ndogo sana”alisisitiza Mganga mkuu huyo wa wilaya.

Kuhusu madhara yatokanayo na uzito mkubwa kupitiliza,Dk,Mgonga hata hivyo aliyataja kuwa ni pamoja na shinikizo la damu,kisukari na magonjwa mengine yanayotokea baada ya kupata magonwa hayo na endapo ugonjwa mmoja ukitatuliwa unasaidia kuzuia magonjwa mengine mengi yanayoweza kutokea.

Akitoa ushauri kwa watumishi,wananchi na madiwani wanachama waliohudhuria katika zoezi hilo la kupima afya zao,Mganga Mfawidhi,Bi Elizabeth Mpangala aliwashauri wananchi hao kupunguza matumizi ya chakula kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia pia uzito kupungua.

Aidha Bi Mpangala aliwasisitiza pia kwamba wazidishe matumizi ya mboga za majani,vyakula vya protini pamoja na kufanya mazoezi kutasaidia kupunguza uzito huku akionyesha kutoridhishwa na baadhi ya watu kutotumia mboga za majani ambazo zina sukari ndogo,tofauti na wanga na vyakula vyenye protini.

Naye diwani wa kata ya Iborogelo,Bwana Simbalugombi Ndali aliweka bayana kwamba baada ya kushiriki katika zoezi hilo la kupima afya aligundulika kuwa na kilo 93 na hivyo kutumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanafuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kukabiliana na magonjwa hayo yanayotokana na kuwa na uzito mkubwa kupitiliza.

No comments:

Post a Comment