Monday, January 9, 2017

Waziri Mhagama azindua Bodi mpya ya NEEC

SERIKALI  imeridhishwa  na utekelezaji wa sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuiagiza Bodi mpya ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kufanya kazi karibu na watendaji baraza hilo ili kufikia malengo yake.

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Bi.Jennista Mhagama, amesema serikali ina imani kubwa na bodi mpya ya Baraza na hivyo kulitaka kutekeza majukumu yake kwa uwazi na ufanisi.
 “Jukumu lenu kubwa ni kushauri na kuelekeza utendaji wa majukumu ya Sekretarieti ya Baraza ili waweze kuchochea Uwezeshaji unaotekelezwa na taasisi za umma na zile zile za binafsi,”alisema Bi.Mhagama wakati akizindua Bodi mpya ya Baraza juzi jijini Dar es Salaam.
Waziri Mhagama alisema kuwa Serikali inaimani kubwa Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Baraza na pasipo shaka  uzoefu wenu katika masuala mbalimbali ya Uwezeshaji yataiwezesha Serikali kufikia ndoto yake ya kuona Mwananchi amewezeshwa katika maeneo yote muhimu hasa katika uchumi.
 ”Dhana nzima ya Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ni kuona kuwa sehemu kubwa ya uchumi wa Tanzania inamilikiwa na watanzania wenyewe,” alisema na kuongeza kuwa jukumu la bodi ni kuhakikisha nafasi kubwa ya uwezeshaji inatolewa kwa makundi yote hasa yale yenye uwezo mdogo na kuwapa nafasi zaidi wanyonge.
 Alisema yote haya yanawezekana tukishirikiana kwa pamoja katika kutekeleza azma ya serikali ya kukuza uchumi imara kwa wananchi unaoweza kuhimili ushindani katika soko la dunia katika mazingira ya utandawazi.
“Ni vizuri Baraza likawapa elimu  wananchi juu ya utunzaji fedha ili waweze kupata mitaji ya kuendeleza au kuanzisha miradi ya biashara kwani utunzaji fedha ni njia mojawapo ya kumkomboa mwananchi katika umaskini,” alisisitiza.
Waziri alilitaka Baraza kuandaa mfumo wa kufuatilia Maendeleo ya shughuli za kiuchumi na mfumo wa Menejimenti ya Habari za Uwezeshaji ili kuwa na taarifa sahihi katika maswala ya uwezeshaji nchini.
“Kupitia Madawati ya Uwezeshaji kuanzia Wizarani, Idara na Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa fuatilieni kwa ukaribu Taarifa za utekelezaji wa Miradi na Programu za Uwezeshaji kutoka katika Madawati hayo,” alisisitiza Bi.Mhagama
 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya NEEC, Dkt. John Jingu alisema sera ya uwezeshaji italitekeleza kwa vitendo na kuhakikisha wananchi wanapiga hatua kiuchumi na nchi kufikia uchumi wa kati kama sera inavyoeleza.“Tutajitahidi kuwa wabunifu katika kutatua changamoto zitakazojitokeza ili kuhakikisha malengo ya serikali yanatekelezeka kikamilifu,” alisema Dkt. Jingu
Alisema ushirikiano ndio nyenzo pekee katika kufanikisha malengo ya serikali ya kuwawezeshaji wananchi kiuchumi  linafanikiwa kwa kiwango kikubwa.Naye Katibu Mtendaji wa NEEC, Bi.Beng’i Issa alisema mambo muhimu ambayo Waziri amesisitiza ni kufanya kazi kwa pamoja ili kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa wanyonge.

“baraza litaendelea kuhamasisha na kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujiunga na SACCOS na VICOBA pamoja na kuweka akiba pia kutengeneza mpango wa utekelezaji wa programu ya ushiriki wa watanzania katika uwekezaji(LOCAL CONTENT).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Bi.Jennista Mhagama akisisitiza jambo katika kikao cha uzinduzi wa Bodi mpya ya Baraza la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi(NEEC). Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt.John Jingu na kushoto ni katibu mtendaji wa NEEC,Bi.Beng’i Issa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Bi.Jennista Mhagama akikabidhi nyenzo za kazi kwa Mwenyekiti wa bodi ya Baraza la Uwezeshaji wananchi kiuchumi(NEEC), Dkt. John Jingu katika kikao cha uzinduzi wa bodi hiyo mpya ya Baraza. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na W,alemavu Bi.Jenista Mhagama akikabidhi nyenzo za kazi mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Baraza la Uwezeshaji wananchi kiuchumi(NEEC), Prof.Samuel Wangwe katika kikao cha uzinduzi wa Bodi mpya ya Baraza hilo.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC),Bi.Beng’i Issa akizungumza jambo katika kikao cha uzinduzi wa Bodi mpya ya Baraza hilo. Kulia kwake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Bi.Jennista Mhagama na wapili kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya NEEC, Dkt. John Jingu

No comments:

Post a Comment