Tuesday, January 3, 2017

WASIMAMIZI WA UCHAGUZI MDOGO ZINGATIENI SHERIA, KANUNI NA MAADILI, MSIKUBALI KUYUMBISHWA NA MTU.

 Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw.kailima Ramadhani akifungua mafunzo ya siku 3 ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi leo mjini Dodoma. 
Baadhi ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao wakati wa Uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 22, 2017 leo mjini Dodoma. Picha na Aron Msigwa - NEC


Na. Aron Msigwa - NEC
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI imewataka Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi mdogo wa Udiwani utakaofanyika katika Kata 20 za Tanzania Bara na Ubunge katika jimbo la Dimani Visiwani Zanzibar Januari 22, 2017 kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili ili Uchaguzi huo uwe Huru na wa Haki.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhan wakati akifungua mafunzo ya siku 3 ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi leo mjini Dodoma.

Mkurugenzi Kailima amewataka Wasimamizi hao kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali katika kushughulikia mambo yatakayojitokeza wakati wa uchaguzi huo.

Katika kutimiza majukumu yao wawe tayari kutoa ufafanuzi juu masuala mbalimbali kwa kuzingatia sheria na kutokuwa tayari kukubali kuyumbishwa na mtu yeyote atakayekiuka miongozo, sheria na kanuni za Uchaguzi.

Amewataka Wasimamizi hao watende mambo yote kwa kuzingatia kanuni na Sheria na kutoa maamuzi sahihi kwa mustakabali wa Taifa na kuwasisitiza kuepuka kutoa upendeleo katika maamuzi wanayoyafanya na wasikubali kuyumbishwa na matakwa ya baadhi ya watu.

Amewaeleza kuwa milango ya Tume iko wazi pale watakapohitaji ufafanuzi huku akitoa wito kwa Wasimamizi hao kuwasiliana na watendaji wa Tume katika mambo yanayowatatiza ili wapate ufafanuzi.

Aidha, amewataka wawe makini na hatua ya utangazaji wa matokeo kwa kutoa taarifa kwa wananchi mara kwa mara juu ya hatua zinazoendelea vituoni wakati wa ukusanyaji wa matokea ili kuwaondolea wasiwasi pindi wanapoona matokeo yamechelewa kutolewa.

" Hili naomba nilisisitize, mnapoona baadhi ya taratibu hazijakamilika tokeni nje muwaambie wananchi nini kinaendelea ili wawe na taarifa na hii itawaongezea imani wananchi wanaosubiri matokeo na kuepusha vurugu vituoni" Amesisitiza Bw.Kailima.

Amesema kuwa mfumo wa Uchaguzi wa Tanzania ni wa uwazi kwa kuwa kila chama kinakuwa na Wakala anayesimamia maslahi ya chama chake wakati wa uchaguzi, pia uwazi katika hatua zote za uchaguzi ikiwemo upigaji wa kura, uhesabuji wa Matokeo na ujumlishaji wa matokeo ambayo hulinganishwa na vishina.

Kwa upande wa Mawakala wa Vyama vya Siasa watakaoshiriki katika Uchaguzi mdogo amesisitiza kuwa wanatakiwa kuzingatia maadili ikiwemo kuepuka kutoa matokeo ambayo hawajaruhusiwa kuyasema wakati wa zoezi la upigaji wa kura na wanatakiwa kuapa kiapo cha kutunza siri na kujaza fomu kwa mujibu matakwa ya kikanuni.

" Wakala Chama cha Siasa haruhusiwi kutangaza matokeo kwa mgombea wake wakati zoezi la kuhesbu kura likiendelea kituoni, na hili nalilisisitiza Mawakala wote ni lazima waape kiapo cha kutunza Siri, ni matakwa ya kikanuni, wakala asiyeapa na kujaza fomu asipewe ridhaa ya kuwa wakala wa chama cha siasa ndani ya kituo" Amesisitiza Bw. Kailima.

Amesema kila Chama kitakuwa na Mawakala wa aina tatu kwa maana ya Wakala wa Kupiga kura, Wakala wa kuhesabu kura, Wakala wa kujumlisha kura na Kutangaza Matokeo ambao watakua na jukumu la kulinda maslahi ya vyama vyao na wagombea wawapo kituoni, kumsaidia msaidizi wa kituo pamoja na kuangalia taratibu zinavyokwenda kituoni.

Amesisitiza kuwa maamuzi ya kituo yatatolewa na Msimamizi wa kituo na Wakala ambaye hatakubaliana na maamuzi hayo atajaza fomu namba 16 kuonyesha kuridhika au kutokuridhika.

Kuhusu mafunzo amesema yanalenga kuwajengea uwezo Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa Uchaguzi kuelewa Misingi, Sheria na Wajibu wa namna bora ya kutekeleza majukumu yao katika usimamizi wa hatua zote za uchaguzi ikiwemo upigaji wa kura na utangazaji wa matokeo.

Ameongeza kuwa Wasimamizi na Waratibu hao watafundishwa maadili ya kuzingatia wakati wakitekeleza majukumu yao ikiwemo maadili ya uchaguzi,maelekezo kwa wasimamizi ya Uchaguzi, wajibu wao, majukumu ya makarani , taratibu za kupiga kura, kuhesabu kura, kujumlisha kura na kutangaza matokeo, kuandaa taarifa za uchaguzi pamoja na masuala mbalimbali kuhusu uchaguzi huo.


Akizungumzia kuhusu Rufaa za mapingamizi ya wagombea amesema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292, Tume ilipokea Rufaa za wagombea kutoka Kata mbalimbali ikiwemo ya Kijichi - Manispaa ya Temeke, Misugusugu- Halmashauri ya mji Kibaha, Pwani na Kata ya Ihumwa Manispaa ya Dodoma.

Amesema katika kikao cha Tume cha Desemba, 30, 2016 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa maamuzi ya Rufaa zote kwa haki na kwa kuzingatia kanuni, taratibu, miongozo na sheria zinazosimamia Uchaguzi ikiwemo Rufaa ya Kata ya Ihumwa, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ambayo imeondolewa kwa kuwa mkata Rufaa ameiondoa mwenyewe na amejitoa katika ugombea Udiwani kabla Rufaa yake haijasikilizwa.

Kwa Upande wa Rufaa ya jimbo la Dimani, Zanzibar Bw. Kailima ameeleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa kifungu cha 40 (6) ilipokea Rufaa ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi ya kupinga maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo kumthibitisha mgombea wa Chama cha Wananchi CUF kwamba ni mgombea halali katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Dimani, Zanzibar.

Bw. Kailima ameeleza kuwa katika kikao cha Maamuzi cha Tume cha kupitia Rufaa za wagombea, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilikubaliana na Uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo kuwa mgombea wa Chama cha Wananchi CUF aliyewekewa pingamizi na mgombea wa CCM amekidhi vigezo na uteuzi wake ni halali hivyo anaweza kuendelea na kampeni za kugombea nafasi ya Ubunge katika jimbo hilo.




" Napenda nisisitize kuwa maamuzi yote yaliyofanywa na Tume yamezingatia Kanuni, Taratibu, Sheria na miongozo inayosimamia chaguzi, hali hii ya wagombea kukubali maamuzi ya Tume inatujengea msingi imara wa kuendelea kufanya vizuri zaidi kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 huku tukitimiza majukumu yetu kwa mujibu wa sheria bila kupendelea" Amesisitiza Bw.Kailima.

No comments:

Post a Comment