Sunday, January 15, 2017

Wakulima viazi Njombe waishukuru SAGCOT kuwawezesha

Na Mwandishi Wetu, Njombe

WAKULIMA wa viazi Mkoani Njombe wameushukuru Mpango wa kuendeleza Kilimo Ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kwa kuwaletea mradi wa uzalishaji na usambazaji mbegu bora za viazi pamoja elimu juu ya zao hilo ambapo sasa uzalishaji wake umeongezeka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima wa viazi mkoani hapa wamewaambia waandishi habari jana kuwa kuwepo kwa mradi huu toka SAGCOT umetusaidia kutoka katika kilimo cha mazoea na kuingia kwenye kilimo biashara.

Mchungaji Michael Nyagawa toka kijiji cha Lunguya, kata ya Mtwango Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ni mmoja wa wakulima waliofaidika na mradi wa uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za viazi toka SAGCOT alisema wakulima wa viazi walikuwa na mazingira magumu katika uzalishaji.

“Tulifika kipindi hekali moja ya viazi unavuna gunia 20 tu, lakini sasa tunapata gunia 60 mpaka 80 kwa hekali,” alisema MchungajiNyagawa na kufafanua kuwa kupitia mafunzo na mbegu mpya toka SAGCOT uzalishaji wa viazi umeongezeka na kuinua vipato kwa wakulima,” alisema.

Mchungaji huyo hakusita kusema kuwa kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu zao hilo vilichangia uzalishaji kuwa mdogo kama vile uandaaji wa shamba, namna ya kupanda mbegu, uhifadhi wa mbegu katika maghala na pia mbegu ilikuwa ya zamani sana.

“SAGCOT imetupatia mbegu za aina nne ambazo ni Tengeru,Sherekea,Asante na Meru ambazo zimetolewa bure kwa sisi wakulima” alisema Mchungaji Nyagawa na kuongezea kuwa hata pale tunapovuna mazao yote yanakuwa mali yetu.

Alisema SAGCOT imembadilisha na sasa amekuwa akizalisha mbegu na kusambaza kwa wakulima wengine ili kuisaidia SAGCOT katika usambazaji wa mbegu bora na elimu juu ya uzalishaji wa viazi.

“ Elimu waliyonipatia nami nitaitoa kwa wakulima wengine ili kukuza uzalishaji na kujikwamua kiuchumi,” alisema Mchungaji huyo na kuishukuru SAGCOT.

Naye, Bi.Sara Martin kutoka kijiji cha Maduma, Kata ya Kichiwa Halmashauri ya wilaya ya Njombe alieleza jinsi alivyoupokea mradi huo toka SAGCOT na jinsi ulivyomsadia katika kujikwamua kiuchumi.

“Ilikuwa vigumu kuachana na mbegu tuliyoizoea lakini baada ya mafunzo na kupanda mbegu mpya nikaona mafanikio makubwa katika mbegu hizi mpya,” alisema Bi.Nyagawa na kuongezea kuwa uzalishaji ulikuwa mara mbili ya tulivyokuwa tukizalisha kabla ya mradi huu.

Alisema baada ya kulima kwa majaribio msimu wa pili aliweza kulima heka kumi zilizompekelea kupata zaidi ya magunia 300 na kwa sasa amekuwa mzalishaji na muuzaji wa mbegu kwa wakulima wengine na pia amekuwa akitoa elimu kwa wakulima wengine wajiunge katika kutumia mbegu mpya.

“Nimeweza kumlipia ada ya chuo kikuu mtoto wangu na nimefanikiwa kununua Ng’ombe wa maziwa na maisha kwa ujumla yamebadilika,” alisema Bi.Sara.

“Hali yangu ya maisha ni nzuri kwani kipato changu kimeongezeka lakini kabla mradi huu maisha yalikuwa magumu na nisingeweza hata kulipia ada lakini kwa uwepo wa SAGCOT umenifanya niwe na mafanikio na furaha katika maisha.

Kwa upande wake, Mtaalam toka SAGCOT na Mratibu wa mradi wa uzalishaji na usambazaji mbegu bora za viazi kwa mkoa wa Njombe, Bw.Owekisha Kwigizile alisema mwitiko wa wakulima katika mradi huu umekuwa mkubwa na hata uhamasishaji wa wao kwa wao umekuwa mkubwa.

“Nafarijika kwa mafanikio yanayopatikana kwa wakulima walioupokea mradi huu kwani mafanikio yao ndio hamasa kwetu katika kuendeleza mafunzo zaidi kwa wakulima,” alisema Bw.Kwigizile

Alisema ili kufanya uzalishaji wa viazi kuongezeka wakulima walionufaika na mradi hawanabudi kuwahamasisha na wengine kwa kuwapa mafunzo na mbegu bora ambazo wao sasa wanazalisha ili kuongeza uzalishaji na kuachana na kutumia mbegu ya zamani ambayo haina tija.

Kwa mkoa wa Njombe SAGCOT imejikita katika kutoa mafunzo na kusambaza mbegu za zao la viazi ambalo hapo awali lilionekana kuwa na changamoto katika uzalishaji wake.

Mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya watu wa Marekani (USAID) kupitia Shirika la kusimia mapinduzi ya kijani barani Afrika (AGRA) .

Mtaalam na Mratibu wa Mradi wa kuzalisha na kusambaza mbegu bora za viazi mviringo kwa wakulima – Njombe toka SAGCOT, Bw.Owekisha Kwigizile akitoa mafunzo kwa wanakikundi cha Matunda group katika kata ya Mhaji, halmashauri ya Wilaya ya wanging’ombe Mkoani Njombe hivi karibu alipowatembelea na kuwaelimisha juu y Mradi wa kuzalisha na kusambaza mbegu bora za viazi mviringo unaoratibiwa na Mpango wa kuendeleza kilimo ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT). Chini ya unafadhiliwa na Serikali ya watu wa Marekani(USAID) kupitia Shirika la Kimataifa la kusimamia mapinduzi ya kijani barani Afrika(AGRA).
Mkulima Bi Sara Martin akimwonesha kitu Mtaalam na Mratibu wa Mradi wa kuzalisha na kusambaza mbegu bora za viazi mviringo kwa wakulima – Njombe toka SAGCOT, Bw.Owekisha Kwigizile alimpomtembelea shambani kwake katika kijiji cha Maduma kata ya Kichiwa ,Halmashauri ya wilaya ya Njombe na kuona maendeleo ya kilimo cha zao hilo. Mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya watu wa Marekani(USAID) kupitia Shirika la Kimataifa la kusimamia mapinduzi ya kijani barani Afrika(AGRA)na kuratibiwa na Mpango wa kuendeleza kilimo ukanda wa kusini mwa Tanzania(SAGCOT).
Mkulima Bi. Agusta Madembwe wa kijiji cha Nyanga, kata ya Ikuna, Halmashauri ya wilaya ya Njombe akikagua shamba lake alilipanda mbegu mpya za viazi mviringo alizozipata kupitia Mradi wa kuzalisha na kusambaza mbegu bora za viazi mviringo kwa wakulima – Njombe unaoratibiwa na Mpango wa kuendeleza kilimo ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT). Akiwa na matumaini makubwa ya uzalishaji kwani amelima kwa njia ya kisasa.

No comments:

Post a Comment