Wednesday, January 4, 2017

WAKULIMA BUSEGA KUANZA KILIMO KIKUBWA CHA UMWAGILIAJI

Na Stella Kalinga, Simiyu.

Serikali Mkoani Simiyu  imewashauri wakulima wote wilayani Busega  wenye mashamba yaliyo karibu na ziwa Victoria kuorodhesha jumla ya ekari za mashamba waliyonayo ili waweze kusajiliwa na kuingizwa katika mpango wa  kilimo cha umwagiliaji kinachotarajiwa kuanza mapema mwaka huu.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mtaka katika ziara yake maalum ya kuwatembelea wananchi wa vijiji vilivyopo  kandokando ya ziwa Victoria Wilayani Busega, ambapo ameanza na vijiji vya Nyamikoma na Nyakaboja  kata ya Kabita.

Mtaka alisema endapo wakulima watakuwa tayari kufanya  kilimo cha umwagiliaji  kwa kufuata ushauri wa kitaalamu na kutumia mbegu bora watapata mazao mengi yatakayokubalika katika soko la ndani na nje ya Mkoa ikiwa sambamba na  na kujikwamua kiuchumi.

Alieleza kuwa  lengo la serikali  ya Mkoa ni kuhakikisha dhana ya mapinduzi ya kilimo kwa mfumo wa umwagiliaji inatekelezwa kwa vitendo kwa kuwapatia elimu ya kitaalamu wakulima ili waweze kuzalisha mazao bora na mengi yanayotosheleza soko la ndani ya nchi na kupunguza uagiziaji mazao nje ya Mkoa.

 “Tumekuja kama mkoa kuzungumza na wananchi ili wale watakaokuwa tayari waanze kutekeleza. Ni lazima tufanye maamuzi ya kufanya mapinduzi ya kilimo kama watu tulio kandokando ya ziwa Victoria ili uwepo ziwa utunufaishe” amesema Mtaka.

Aidha alifafanua kuwa kilimo hicho katika maeneo ya  Wilaya ya Busega  kitahusisha mazao ya Mpunga,  mboga mboga, mahindi na mazao jamii ya mikunde, hivyo wakulima kwa kushirikiana na Serikali wanatakiwa kuendelea kubuni mbinu  mbalimbali za uzalilishaji mazao hayo kwa wingi ili kwenda sambamba na fursa ya masoko ya ndani na nje ya nchi hasa kwa mazao ya mikunde.

Mtaka ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi imetoa fedha katika Taasisi za fedha kwa ajili ya shughuli za kilimo, hivyo akawashauri wananchi kujiunga katika vikundi ili iwe rahisi kuwatambua na kuwawezesha kwa pembejeo na miundombinu  ya kilimo cha umwagiliaji kulingana na makubaliano yatakayowekwa.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa amewasihi vijana nchini kujiajiri wenyewe kupitia kilimo hicho kwa lengo la kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira badala ya kukimbilia mijini wakati fursa za kujiajiri zipo nyingi vijijini.

Kwa upande wake Mkulima wa kilimo cha mpunga Charles Malombo kutoka  katika kijiji cha Nyakaboja alisema licha ya serikali kuwa na mpango mzuri kwa kuwapatia matumaini makubwa ya mafanikio katika kilimo cha umwagiliaji bado wanahitaji msaada wa kitaalamu utakaowasaidia kutumia teknolojia ya kisasa  katika umwagiliaji maji  ya ziwa Victoria ili waweze kupata mazao mengi zaidi ya wanayopata kwa sasa.

Naye Samuel Chochomo ambaye ni Mkulima wa mazao mbali mbali ya Mboga mboga alikiri kilimo hicho ndicho kitakachowatoa wakulima na wananchi katika janga la njaa
  
Alieleza kuwa   kilimo cha kutumia teknolojia ya umwagiliaji maji ni kizuri na  hakitegemei msimu wa mvua, wakulima wanaweza kulima wakati wote kama  wakiwa na miundombinu mizuri ya upatikanaji wa maji kutoka Ziwani na mipira imara ya kusambazia maji.

Wilaya ya Busega ni wilaya pekee Mkoani Simiyu iliyo na maji ya uhakika ya Ziwa Victoria na eneo la takribani ekari 7200 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
  Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyakaboja wilayani Busega katika Mkutano wa hadhara kwa lengo la kuwahamasisha kuanza kutekeleza mpango wa kilimo cha umwagiiaji wilayani humo.
 Mkuu wa Wilaya ya Busega Tano Mwera akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Nyakaboja wilayani humo katika Mkutano wa hadhara kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kuanza kutekeleza mpango wa kilimo cha umwagiiaji wilayani humo.
Afisa Ardhi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Bibi.Grace Mgombera akitoa  ufafanuzi wa juu masuala ya ardhi yaliyowasilishwa na wananchi wa Kijiji cha Nyamikoma B wilayani Busega  kama kero kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka katika mkutano wa hadhara uliofanyik kjijini hapo.
 Diwani wa Kata ya Kabita wilayani Busega akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Nyakaboja wilayani humo katika Mkutano wa hadhara kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kuanza kutekeleza mpango wa kilimo cha umwagiiaji wilayani humo.
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa pili kulia) akisaini kitabu mara baada ya kuwasili katika Kijiji cha Nyakiboja kata ya Kabita wilayani Busega  kabla ya kuwahutubia wananchi wa eneo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Nyamikoma B Kata ya Kabita, wilayani Busega wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika Mkutano wa hadhara kuwahamasisha kuingia na kuanza kutekeleza mpango wa kilimo cha umwagiiaji wilayani humo.
 Baadhi ya Maafisa wa Sekretarieti ya Mkoa walioambatana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika ziara yake ya kuwahamasisha wananchi wa Busega kutekeleza mpango wa kilimo cha umwagiliaji.

No comments:

Post a Comment