Sunday, January 8, 2017

Timu ya kuchunguza chanzo cha moto soko kuu la Kayanga yaundwa


 Na Mwandishi wetu.
Kufuatia kuungua kwa mara ya pili kwa soko kuu la kayanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Ofisi ya Mkuu wa mkoa Kagera imeiagiza Halmashauri hiyo kuunda timu mara moja na kuanza uchunguzi wa chanzo cha moto huo katika soko hilo, ambalo kwa mara ya kwanza liliungua  tarehe 11 Machi, 2016.

Sehemu ya soko kuu la Kayanga imeungua usiku wa kuamkia tarehe 7 Januari, 2017, saa 9:00 usiku, ambapo vibanda 52 vilivyojengwa kwa mbao na meza 24 za wafanyabashara wadogowadogo wa nafaka, matunda na mbogamboga vimeteketea kwa moto pamoja na mali za wamachinga waliokuwa wanapanga chini wapatao 33 nao mali zao zimeteketea kwa moto.

Akiongea mara baada  ya kukagua athari za janga la moto katika soko hilo Katibu tawala wa Mkoa wa Kagera Kamishina Diwani Athumani, leo tarehe 7 Januari, 2017,  na kuteketeza sehemu ya soko kuu la Kayanga wilayani Karagwe kwa mara ya pili ikiwa limewahi kuungua, amebainisha kuwa tayari Halmashauri ya wilaya hiyo imeshatekeleza maelekezo yao ya kuunda timu ya uchunguzi ambayo inaanza kutekeleza majukumu yake kesho, tarehe 8 Januari, kwa muda wa siku nne.

“Tumeunda timu tujue kwa nini hili soko linakuwa na majanga ya moto ya mara kwa mara, nawaomba wananchi wote wa Kayanga toweni ushirikiano wa kutosha kwa timu hii na yeyote mwenye taarifa ya chanzo cha moto awasilishe taarifa zake kwenye kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hii”  Alisisitiza Athumani.
Aidha, Athumani alifafanua kuwa yeyeyote atakaye bainika kuwa ndo chanzo cha kusababisha majanaga ya moto kutokea mara kwa mara katika soko  hilo hatua stahiki zitachukuliwa kwa kuwa  kuungua kwa soko hilo kumekuwa kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiara wa soko hilo.
Akiongea wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Adeodata  Agustine, amefafanua kuwa thamani ya awali ya mali iliyoteketea inakisiwa kuwa Tsh, 80,000,000/= (mazao ya nafaka, mbogamboga , matunda pamoja na nguo na bidhaa za dukani), na thamani ya vibanda ni Tsh, 52,000,000/= na meza ni 9,600, 000/=.

“Chanzo cha moto hadi sasa hakijajulikana na kikosi cha zimamoto kwa kushirikiana na na Polisi na TANESCO wanaendelea na uchunguzi, taarifa hii ni ya awali tutapata taarifa kamili ya thamani ya mali na chanzo cha  janga la moto baada ya timu kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa” alisema Adeodata.

Naye mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko kuu la Kayanga, Wilton William, aliishukuru halmashauri hiyo kwa juhudi walizo zifanya za kuzima moto huo pamoja na hatua walizozichukua za kuchunguza chanzo cha moto huo amabao umeunguza soko hilo kwa mara ya pili mfululizo.

Soko la Kayanga lina jumla ya vibanda 257, ambapo  vibanda 122  vimejengwa kwa matofari, na vibanda 135 vimejengwa kwa mbaao.  Katika tukio la janaga la moto la mwaka jana vibanda 117 ikiwa  ni viband 83 vya mbaao na 34 vya tofari viliteketea kwa moto.
 Katibu tawala Mkoa wa Kagera Kamishina, Diwani Athumani akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Adeodata Agustine juu ya janga la moto katika soko kuu la Kayanga alipotembelea soko hilo kujionea athari za moto tarehe 7 Januari 2017.
Katibu tawala Mkoa wa Kagera Kamishina, Diwani Athumani (katikati) akipata maelezo ya uratibu wa majanga kutoka kwa  Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Brg. Jen. Mbazi Msuya wakati alipotembelea soko hilo kujionea athari za moto tarehe 7 Januari 2017 (kushoto) ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Adeodata Agustine.(PICHA ZOTE NA OFFISI YA WAZIRI MKUU)
 Baadhi ya Wafanyabiashara wa mazao ya nafaka wakipakia mabaki ya mazao  yao baada ya vibanda vyao vya biashara kuungua moto kufuatia moto uliozuka usiku wa saa 9:00 usiku wa tarehe 7Januari, 2017,  na kuteketeza sehemu ya soko kuu la Kayanga wilayani Karagwe kwa mara ya pili ikiwa limewahi kuungua tarehe 11 Machi 2016.
 Muuonekano wa Soko Kuu la Kayanga  baada ya vibanda  vya baadhi ya wafanyabiashara kuungua moto kufuatia moto uliozuka usiku wa saa 9:00 usiku wa tarehe 7 Januari, 2017, ikiwa soko hilo limewahi kuungua tarehe 11 Machi 2016.

No comments:

Post a Comment