Monday, January 30, 2017

TAZAMA YATAKIWA KUBANA MATUMIZI ILI KUONGEZA UZALISHAJI

Kampuni ya Kusafirisha Mafuta Ghafi ya TAZAMA imetakiwa kutumia uchumi kushusha gharama za matumizi ili kumudu ushindani wa soko Nchini Zambia.

Wito huo umetolewa hivi karibuni kwa nyakati tofauti na Mawaziri wa Nishati wa Tanzania na Zambia, Profesa Sospeter Muhongo (Tanzania) na Mabumba David (Zambia) walipokuwa wakizungumza na wafanyakazi wa Vituo vya Kusukuma Mafuta (Pumping Stations) vilivyopo Mkoani Mbeya na Iringa wakati wa ziara ya kutembelea vituo hivyo.

Profesa Muhongo alisema dhamira ya Serikali za Tanzania na Zambia ni kuhakikisha Bomba pamoja na Mfumo mzima wa uendeshaji wa kampuni hiyo vinaboreka na kuweza kushusha bei ya mafuta ili kumudu ushindani.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) na Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba David (nyuma yake) wakikagua Kituo cha Kusukuma Mafuta Ghafi (Pumping station) cha TAZAMA kilichopo Mkoani Mbeya.

 Alisema kampuni ya TAZAMA haiwezi kuendelea na utendaji wa kizamani huku ikitumia gharama kubwa kwenye uendeshaji na hivyo kusababisha kuuza mafuta yake kwa bei ya juu ikilinganishwa na wauzaji wengine kwenye soko.

Aliongeza kwamba zinahitajika jitihada za makusudi kuhakikisha uzalishaji unaongezeka kwa lengo la kuweza kuingia kwenye ushindani wa soko.

Alisema teknolojia inayotumiwa na kampuni hiyo kwa ujumla wake imepitwa na wakati na ili kuongeza uzalishaji ni muhimu kuhakikisha teknolojia hiyo inaboreshwa sambamba na uboreshwaji wa utendaji wa wafanyakazi wake. “Hampaswi kuridhika na kiwango mnachosafirisha kwani ni kidogo sana ikilinganishwa na hapo awali; mkiendelea hivi mnaweza kujikuta mnasafirisha hata lita laki moja,” alisema.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akikagua moja ya mtambo wa Kusukuma Mafuta Ghafi wa TAZAMA Mkoani Iringa.

Kwa upande wake Waziri David alisema TAZAMA inapaswa kuelewa dhamira ya Serikali hizo mbili ili ifanye jitihada ya kufikia malengo hususan ikizingatiwa kwamba mahitaji ya mafuta nchini Zambia yameongezeka tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Alisisitiza kuwa ni lazima kukafanyika mabadiliko ya kiteknolojia na kiutendaji ili kufikia lengo na alitaja sababu mojawapo inayosababisha mafuta ya TAZAMA kuuzwa kwa bei ya juu kuliko wengine ni kwamba mafuta yanayosafirishwa ni machache wakati gharama ya usukumaji wa mafuta hayo inabaki kuwa kubwa.

“Mkisafirisha mafuta mengi ni lazima gharama zitapungua na hivyo mtaweza kuuza mafuta yenu kwa bei ndogo ikilinganishwa na wengine,” alisema.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza na wafanyakazi wa Kituo cha Kusukuma Mafuta Ghafi cha TAZAMA kilichopo Mkoani Iringa. Kulia kwake ni Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba David. Kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Zambia, Brigedia Jenerali Emelda Chola.

Aliwaasa wafanyakazi wa TAZAMA kuwa waelewa na kukubali kubadilika kwa faida yao binafsi na kwa faida ya nchi za Tanzania na Zambia kwa ujumla.

“Nyie mtakua sehemu ya mabadiliko na mabadiliko hayo ni kutoka kwenye Usafirishaji wa Tani 650,000 hadi kufikia Tani milioni 1.1 ambayo ndio uwezo wa Bomba,” alisema Waziri David. Alisema kuwa kwa tathmini iliyofanywa ya mahitaji ya mafuta Nchini Zambia ifikapo Mwaka 2030, itakuwa ni tani milioni 4 na kwa namna ambavyo kampuni hiyo ilivyo hivi sasa, haitoweza kukidhi soko hilo hivyo ni vyema ikajipanga kujiboresha.

Mawaziri hao wapo katika ziara ya kutembelea njia ya Bomba la Mafuta Ghafi la TAZAMA na Vituo vya Kusukuma Mafuta (Pumping stations) kwenye maeneo yote linapopita Bomba hilo.
Mfanyakazi wa TAZAMA katika Kituo cha Kusukuma Mafuta Ghafi cha Iringa, Yerusalem Anthony akiuliza swali na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha kampuni husika mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kutoka kulia) na Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba David (kulia).
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa tatu kutoka kulia waliosimama) na Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba David (kushoto kwake) pamoja na wafanyakazi wa Kituo cha Kusukuma Mafuta Ghafi cha TAZAMA cha Mkoani Iringa.
Moja ya Mtambo (Pampu) wa Kusukuma Mafuta Ghafi wa TAZAMA Mkoani Iringa. Pampu hizo zilifungwa Mwaka 1968.

No comments:

Post a Comment