Friday, January 6, 2017

NAIBU WAZIRI JAFO APIGA MARUFUKU WAKINAMAMA WAJAWAZITO KUJIFUNGULIA KTK KITANDA CHA KAMBA

 Naibu Waziri ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo wa kati kati akiwa katika boti maeneo ya nyamisati mto Rufiji kwa ajili ya kujiandaa na safari ya kwenda kuwatembelea wananchi wa Wilaya ya Rufiji hususan wale wanaoishi katika maeneo ya Delta ikiwa ni ziara yake ya kikazi Mkoani Pwani ya kukagua miradi  mbali mbali ya maendeleo(PICHA NA VICTOR MASANGU)
Naibu Wazari Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo wa kati kati akiwa kwenye boti katika ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Kibiti na viongozi wengine wa serikali,na wa kwanza kulia  kwake ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Khatibu Chaurembo kwa ajili ya safari ya kwenda kuwatembelea wananchi wa maeneo ya Delta kwa ajili ya kukagua miradi ya  mbali mbali maendeleo.(PICHA NA VICTOR MASANGU)  


NA VICTOR MASANGU, KIBITI

LICHA ya serikali ya awamu ya tano kuongeza juhudi za kuboresha sekta ya afya katika maeneo mbali mbali hapa nchini bado sehemu nyingine utoaji wa huduma hali bado ni tete kutokana na kukabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ukosefu wa wauguzi,madaktari, madawa, magari ya kubebea wagonjwa,vitanda pamoja na vifaa tiba hivyo kusababisha wagonjwa kupata shida kubwa pindi wanapokwenda kupatiwa matibabu.

Changamoto hizo ambazo zinadaiwa ni sugu na hazijafanyiwa utekelezaji wowote zimeweza kubainika baada ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Japo kufanya ziara yake ya kikaz ya siku mbili kwa wananchi wa Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani hususan katika maeneo ya wananchi wanaoishi katika maeneo ya Delta kwa ajili ya kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kubaini changamoto za muda mrefu zilizokuwa zinawakabili ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi.

Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo Mwandishi wa habari hizi aliweza kuzungumza na baadhi ya wakinamama ambao ndio wameonekana kuguswa zaidi katika afya akiwemo Fatma Mbashilu na Hafiswa Hamada wametoa kilio chao kwa Naibu Waziri huyo na kuweka bayana changamoto zinazowakabili wakati wa kujifungua kwani wanapandishwa katika kitanda cha kamba ambacho sio salama na kinawaumiza sambamba na kijifungulia kwa kutumia mwanga wa kibatali kutokana na eneo hilo la visiwani kutokuwa na nishati ya umeme.

“Sisi katika kijiji chetu hususan kinamama wajawazito kwa sasa tunakabiliwa na changamoto nyingi hasa katika upatikanaji wa kupewa huduma, kwani kwa sasa tunajifungulia katika kitanda cha kamba kwa hiyo tunajikuta wakati wa kujifungua tunapata maumivu mara mbili, kwa hiyo tunamwomba Waziri Jafo kwa kuwa ameamua kuja kututembelea huku visiwani atusaidie sisi wakinamama,”walisema kwa uchungu wakinamama hao.

Aidha walisema mbali na kukabiliwa na changamoto hiyo ya kitanda pia kero yao nyingine kubwa ni kutokana na kutumia mwanga wa kibatari katika kujifungulia na wakati mwingine wanakosa kabisa hela ya kununulia mafua ya taa, hivyo wanajikuta wanapata shida sana hasa katika nyakati za muda wa usiku wanakuwa katika hali ya sintofahamu.

Pia wakinamama hao walimpongeza Jafo kwa kuamua kwenda kuwatembelea katika maeneo ya delta wanayoishi kwani kwa kipindi kirefu hawajawahi kuona kiongozi mkubwa wa kitaifa wa serikali ambaye amekwenda kuwajulia hali, hivyo ujio wa waziri huo utaweza kuleta mabadiliko chanya katika kuleta maendeleo kwa wakazi wanaoishi maeneo hayo.

Naye Mganga mfawidhi wa zahanati ya Mchinga Kuluthumu Zuberi amekiri kuwepo kwa tatizo la kipindi cha muda mrefu kwa wakinamma hao kujifungulia katika mazingira amabayo sio rafiki kwa upande wao kwa kutumia kitanda kilichojengwa kwa miti na kamba ambapo amedai kiafya sio nzuri hivyo serikali inapaswa kuwasaidia ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

Akijibu malalamiko ya hayo ya wananchi Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Seleman Jafo ambaye alionekana kuchukizwa na kuwepo kwa hali hiyo aliamua kuchukua maamuzi magumu na kwa kupiga marufuku kabisa tabia ya kuona wauguzi au madaktari kuwalaza wakinamama wajawazito katika vitanda vya kamba pindi wanapokwenda kujifungua kwani kufanya hivyo kuna hatarisha usalama wa uhai wa mama na mtoto anayezaliwa.

Jafo alisema kuwa serikali ya awamu ya tano lengo lake kubwa ni kihakikisha kwamba wanaboresha sekta ya afya kuanzia ngazi za vijijini hivyo wamejipanga vilivyo katika kuzitatua changamoto zinazowakabili wananachi ili kuweza kuwapatia huduma nzuri, na kuongeza kuwa ameshamwagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Kibiti kupeleka kitanda katika zahanati ya kijiji cha Mchinga ili wakinamama waondokana na kero hiyo ya kujifungulia katika kitanda cha kamba.

“Ninaagiza kuanzia sasa sitaki kuona wakinamama wajawazito wanajifungulia wakiwa katika kitanda cha miti, hii kwa upande wangu sipapendezwa nayo hata kidogo kwani inahatarisha maisha ya mama pamoja na mtoto wake kwa hivyo viongozi wa Wilaya ya Kibaiti kwa hili naomba mlifanyie kazi kwa haraka kupeleka kitanda kingine,”alisema Jafo.

Aidha katika hatua nyingine Jafo amewaagiza viongozi wa halmashauri ya Kibiti kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wajikite zaidi kuwahudumia wananchi wao ikiwa sambamba na kuweka kipaumbele zaidi katika kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa madawa ya kuwatibu wagonjwa wakati wote hasa katika zahanati zote zilizopo katika maeneo yote yaliyozungukwa na maji Delta.

Naibu Wazari huyo kwa sasa yupo anaendelea na ziara yake ya kikazi katika  Mkoani Pwani ikiwa ni moja kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kuweza kuibaini changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi hasa wale hasa wale wanaoishi vijijini ambao wamekuwa wakisahaulika na viongozi wao na kujikuta wanakosa mahitaji na huduma mbali mbali za msingi ikiwemo, afya, elimu, maji hivyo kuwafanya waishi katika mazingira magumu na kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo.

No comments:

Post a Comment