Monday, January 16, 2017

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Kaijage akagua mwenendo wa Uchaguzi Mdogo kata ya Ngh'ambi

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage (kushoto) akisalimiana na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mpwapwa Bw. Mohamed Maje baada ya kuwasili wilayani Mpwapwa kutembelea kata ya Ngh’ambi inayotarajia kufanya uchaguzi mdogo Januari 22 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Polisi wilaya ya Mpwapwa OCD Hussein Mdoe baada ya kuwasili wilayani Mpwapwa kutembelea kata ya Ngh’ambi inayotarajia kufanya uchaguzi mdogo Januari 22 mwaka huu.Katikati ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mpwapwa Bw. Mohamed Maje.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R) Semistocles Kaijage (katikati) akiongoza kikao cha kupokea taarifa kuhusu mwenendo wa uchaguzi mdogo wa Kata ya Ngh’ambi unaotarajiwa kufanyika Januari 22 mwaka huu.Kulia kwake ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mpwapwa Bw. Mohamed Maje, Mkuu wa Polisi wilaya ya Mpwapwa OCD Hussein Mdoe na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa NEC Bw. Emmanuel Kawishe, Mkuu wa Kanda ya Kati ya Uchaguzi Bi. Saada Kangeta na Afisa Utumishi wa Tume Athumani Masesa.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage (katikati) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri wakati alipomtembelea ofisini kwake kabla ya kutembelea Kata ya Ngh’ambi.Kulia ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mpwapwa Bw. Mohamed Maje.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mpwapwa Bw. Mohamed Maje (aliyesimama) akitoa maelezo ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage (kulia kwake) baada ya kuwasili kwenye Kata ya Ngh’ambi kufuatilia mwenendo wa uchaguzi mdogo wa diwani wa kata hiyo unaotarajiwa kufanyika Januari 22 mwaka huu.
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Ngh’ambi James Mkinga (wa pili kulia) akimueleza Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R) Semistocles Kaijage (wa pili kushoto aliyekaa) kuhusu mwenendo wa Uchaguzi Mdogo wa Kata hiyo unaotarajiwa kufanyika tarehe 22 Januari mwaka huu.Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa NEC Bw. Emmanuel Kawishe, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mpwapwa Bw. Mohamed Maje (katikati) na kulia ni Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Kata hiyo Clemence Fugusa.
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Ngh’ambi James Mkinga (aliyesimama) akitoa taarifa ya mwenendo wa Uchaguzi Mdogo wa kata hiyo.
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe (kushoto) akifafanua jambo kwenye kikao cha kupokea taarifa ya mwenendo wa Uchaguzi Mdogo wa Kata ya Ngh’ambi unaotarajiwa kufanyika Januari 22 mwaka huu.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mpwapwa Bw. Mohamed Maje (kulia) akimueleza jambo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage (katikati) na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe baada ya kikao cha kupokea taarifa ya mwenendo wa Uchaguzi Mdogo wa Kata ya Ngh’ambi.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage (kushoto) akikagua daftari la kudumu la wapiga kura kwenye kituo cha kupigia kura cha Kata ya Ngh’ambi kilichopo kwenye Zahanati ya Ngh’ambi. Kushoto kwake aliyevaa miwani ni Afisa Uchaguzi halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa Bi. Martina Batholomeu.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage (aliyevaa kofia nyeusi) akipokea maelezo kuhusu mabango ya Uchaguzi kutoka kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Ngh’ambi James Mkinga (wa tatu kushoto) wakati alipokuwa akikagua mabango hayo nje ya kituo cha kupigia kura cha Kata ya Ngh’ambi kilichopo kwenye Zahanati ya Ngh’ambi.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R) Semistocles Kaijage (kulia) akieleza jambo baada ya kukagua mabango ya Uchaguzi kwenye kituo cha kupigia kura cha kata ya Ngh’ambi.Katikati ni Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa NEC Bw. Emmanuel Kawishe na kushoto ni Afisa Uchaguzi halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa Bi. Martina Batholomeu. Picha na Hussein Makame, NEC.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji (R) Semistocles Kaijage amesema kila kitu kiko sawa tayari kwa uchaguzi mdogo wa kumpata diwani wa kata ya Ngh’ambi iliyoko katika halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

Mhe. Jaji (R) Kaijage ameyasema hayo kutokana na kuridhishwa na maandalizi ya uchaguzi mdogo wa kata ya Ngah’ambi baada ya kutembelea na kufuatilia mwenendo wa uchaguzi wa kata hiyo unaotarajiwa kufanyika tarehe 22 Januari mwaka huu. 

Akitoa taarifa fupi ya mwenendo wa uchaguzi mdogo wa kata hiyo, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mpwapwa  Bw. Mohamed Maje alisema karibu vifaa vyote kwa ajili ya uchaguzi huo vimepokelewa  na kampeni za uchaguzi huo zinaendelea kwa amani na utulivu.

Alisema baada ya uteuzi wa wagombea kufanyika Desemba 22 mwaka 2016 wagombea wanne kutoka vyama vya ADC, CCM, CHADEMA na CUF waliteuliwa ambao ni David Mazengo, Richard Kaleme, Leornard Majenda na Hassan Kiuka, mtawalia.

Kwa upande wa pingamizi kwa wagombea, Bw. Maje alisema walipokea pingamizi kutoka vyama vya CHADEMA na CCM ambapo mgombea wa CHADEMA alipinga uteuzi wa mgombea wa CCM kwa madai kuwa si mkazi wa halmashauri husika.

“Pingamizi hili lilitolewa uamuzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata kwa kutupilia mbali madai hayo baada ya uthibitisho kuwa mgombea wa CCM  ni mkazi halali wa halmashauri husika.Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo pia alikubaliana na uamuzi wa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata.” alisema Bw. Maje na kuongeza kuwa:

“Mgombea wa chama cha CCM alipinga uteuzi wa mgombea wa chama cha CHADEMA kuwa fomu ya uteuzi namba 8 C sehemu C na D imesainiwa na mtu ambaye si Katibu wa chama husika wa mkoa au Wilaya”

“Pingamizi hili pia lilitolewa uamuzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata kwa kutupilia mbali madai hayo baada ya uthibitisho wa maandishi kuwa aliyesaini ndiye Katibu wa chama husika wilaya ya Mpwapwa.Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo alikubaliana na uamuzi huo”

Aliongeza kuwa kamati za maadili kwa ngazi ya jimbo na kata zinafanya kazi na kwamba hadi kufukia Januria 13 kamati hazikupokea malalamiko yoyote kutoka kwenye vyama vinavyoshiriki uchaguzi mdogo kata hiyo.

Alisema wanatarajia kutoa mafunzo kwa makarani waongozaji na wasimamizi wa vituo vya kupigia kura tarehe 18 na 19 Januari na wameshaandaa vituo 12 vya kupigia kura vyenye wapiga kura 4123.

Kwa upande wa Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Mpwapwa OCD Hussein Mdoe alisema hadi sasa kampeni zinafanyika kwa kuzingatia taratibu za nchi na taratibu za uchaguzi na hakuna vurugu zozote zilizojitokeza.

Hata hivyo aliwakumbusha wananchi kuwa jukumu la ulinzi na usalama ni la kila mwananchi na anaamini wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa kata na kamati za maadili zitawakumbusha wananchi jukumu hilo.

Kwa upande wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Ngh’ambi Bw. James Mkinga alisema maandalizi yote ya uchaguzi yamekamilika na wameshabandika daftari la kudumu la wapiga kura kwenye vituo vya kupigia kura.

Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe aliwakumbusha wasimamizi wasaidizi kuhakikisha Sheria, kanuni na taratibu zote za Uchaguzi zinazingatiwa.

Aliwataka wawakumbushe wananchi kufika kwenye vituo vya kupigia kura kwa wakati ili kuepuka kukosa haki ya kupiga kura kwa sababu ya kuchelewa kufika kituoni.

“Hakikisha mnavikumbusha vyama vyote kuondoa mabango ya kampeni yaliyopo kituoni siku ya kupiga kura na kama hawawezi kuyaondoa uwafahamishe kwamba utayaondoa kwa sababu sheria inakataza” alisema Bw. Kawishe na kuongeza kuwa:

“Wakumbusheni wasimamizi wa vituo kufuata Sheria, kanuni na taratibu na yeyote atakayekiuka Sheria Tume ya Taifa ya Uchaguzi haitasita kumchukulia hatua za Kisheria” 

Aliwakumbusha kuhakikisha kuwa mawakala wa vyama wanafuata taratibu zote inapotokea chama kinataka kumbadilisha wakala kwenye kituo cha kupigia kura.


Naye Mkuu wa Kanda ya Kati ya Uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bi. Saada Kangeta aliwakumbusha wasimamizi wasaidizi kuwa iwapo litajitokeza jambo linaloweza kuchelewesha matokeo kama kufanya uamuzi ya kura za mgogoro wawafahamishe wananchi ili kuepuka vurugu.

No comments:

Post a Comment