Saturday, January 7, 2017

MUZIKI WA TANZANIA; TUNAENDA MBELE?


Na JOHN KITIME wa 
www.johnkitime.co.tz

Januari 2013, niliandika makala kuhusu nilivyouona muziki mwaka 2012. Naona nirudie makala ile kama nilivyoiandika, na kukuachia msomaji kulinganisha na hali ilivyokuwa 2016.
Mwaka 2012 ndio huoo umetokomea, ni vizuri kuangalia yaliyopita ili kujitayarisha na yajayo. 

Muziki wa nchi yetu ulitawaliwa na muziki wa Bongoflava, Taarab, muziki wa bendi, matarumbeta, muziki wa enjili, na muziki wa kiasili. Si siri kuwa muziki wa Bongoflava ndio uliokuwa ukitawala katika vyombo vya habari na sehemu nyingi za maonyesho. Muziki huu ulikuwa  ukifuatiliwa na muziki wa Taarab na muziki wa enjili.  Katika muziki wote huu jambo lililokuwa wazi ni kuwa waimbaji ndio waliokuwa wakipewa kipaumbele katika tasnia hii.  

Waimbaji katika aina zote za muziki uliotajwa hapo juu ndio waliotajwa sana na kupewa sifa kwa ubora wa muziki. Kumekuweko na mashindano kadhaa ambayo yote yamejikita katika kutafuta vipawa vya waimbaji japo mara nyingi yamejitambulisha kama mashindano ya kusaka vipaji mbalimbali.

Hakuna ubishi muziki wa dansi na muziki wa asili ndio muziki uliopewa muda mchache sana katika vyombo vya habari. Na hata katika muziki huo, bendi ambazo zimejikita kufuata mipigo ya Kikongo zilipewa nafasi zaidi kuliko bendi ambazo zimejichagulia njia nyingine za muziki wao.


Kuna sababu kadhaa ambazo zimefanya muziki wa bongoflava kuchukua nafasi zaidi katika vyombo vya habari, la kwanza ni uwingi wa kazi za bongoflava zinazorekodiwa. Karibu kila mji una studio ya kurekodi, na katika studio hizo kazi nyingi zaidi zinazorekodiwa ni aina hiyo ya muziki, hivyo kutokana na uwingi wa kazi hizo ni wazi kabisa ndizo ambazo zitaendelea kutawala anga la vyombo vya habari, na kutokana na mfumo wa vyombo vyetu vyote kujikita katika mfumo wa aina fulani tu za muziki.
Kwa mtizamo wangu heka heka za muziki wa Enjili zilipungua 2012. 

Yale matamasha makubwa ya muziki huo yalipungua sana, na hata nyimbo za kushtua jamii hazikuwa nyingi  kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Muziki wa Taarab haujaleta mabadiliko kimuziki, mengi yaliyofanywa katika 2012 ni marudio tu ya ubunifu uliofanyika nyuma. Kama vile uanzishwaji wa kucheza show katika taarab, upigaji wa gitaa na kuliachia pekee yake kama ilivyokuwa kwa bendi kuachia gitaa la rhythm miaka kabla ya tisini. Kumekuweko tu ubunifu wa misemo na mipasho, jambo jingine ambalo limesababisha kuenziwa zaidi kwa waimbaji tu katika fani hiyo.


Bendi ziko katika wakati mgumu, wakati wanamuziki wengi wa bendi wakilalamika kuwa muziki wa bendi haupigwi katika redio na TV, kumekuweko na jitihada ndogo za bendi kurekodi nyimbo mpya, maelezo mengi yamekuwa ni kuhadithia enzi ambapo muziki wa bendi ulitawala na kuona kama hiyo ni sababu tosha ya muziki huo kuendelea kurushwa hewani. Bendi chache zilizorekodi hazijaja na  nyimbo zilizoweza kuteka umma wa  Tanzania na hivyo kusababisha muziki huu kukosekana katika anga za muziki. Matangazo mengi ya muziki wa dansi yamekuwa ni kutangaza rap mpya au kupatikana kwa msanii mpya, lakini kiujumla hakujakuwa na kitu kipya katika muziki wa bendi.

Muziki asili pia umekosekana kwenye vyombo vya habari kwa kuwa si vikundi vingi vya muziki huu vyenye uwezo wa kulipia gharama za studio. Pia studio nyingi zimejengwa kuruhusu wasanii wa Bongoflava tu kurekodi, studio za kuweza kuruhusu kundi la muziki wa asili kurekodi ni zenye gharama kubwa sana. Kundi la Makirikiri lilitakiwa kuwa elimu tosha kwa wasanii wa muziki wa Kiasili, kuwa na muziki wao ukifuata taratibu nzuri unauza, bahati mbaya kuna vikundi sasa vimeacha kuboresha muziki na ngoma zao, badala yake vinaiga uchezaji wa  Makirikiri.


Pengine watu watasema nimesahau muziki wa kwaya, sijausahau, kwa kweli muziki huu umebaki  hasa kwenye muziki wa Enjili. Hapo zamani ulikuwa ukitumika sana mashuleni na kwenye siasa na kampeni , lakini kwa mwaka 2012 hali imekuwa mbaya kwa muziki huu.
Pamoja na kuwa wengine wangeweza kusema tunasonga mbele katika muziki, kwangu mimi naona tunarudi nyuma kitaaluma. Tasnia inaingiza pesa nyingi zaidi, na hata kuna wasanii walioingiza pesa nyingi sana, lakini  kwangu hilo si kipimo cha maendeleo katika tasnia hii.
Kama nilivyoanza kusema washika maikrofon wamekuwa ndio alama ya muziki wa Tanzania. 

Muziki ni zaidi ya kuimba. Katika kuimba sauti nzuri ya muimbaji ni muhimu, na ninashukuru kwa hilo tunao waimbaji wazuri wengi sana, lakini  ule muziki unaomsindikiza muimbaji ni muhimu sana kwani ule hauna mipaka wala lugha, na ndio unaoweza kutufungulia mlango wa soko la kimataifa. Wengi tunapenda sana muziki wa kutoka Kongo, Nigeria, South Africa, pamoja na kuwa hatujui hata moja wanaloliongelea tunaupenda muziki huo kutokana na mpangilio wa vyombo vyao. 

Kutokujali wapigaji katika mfumo wa nchi yetu ndio unatupelekea kuwa watu wa ‘copy and paste’ wa upigaji wa muziki wa nchi nyingine. Ukiorodhesha nyimbo zote zilizotikisa nchi hii kwa mwaka 2012 utagundua asilimia kubwa ya muziki uliotumika ulikuwa ni wa kunakili mipigo kutoka muziki wa nchi nyingine, Nigeria, Congo na Afrika Kusini ndio wamekuwa waalimu wetu wakuu wa muziki. 

No comments:

Post a Comment