Thursday, January 19, 2017

MHE. MHAGAMA ASHAURI CHAMA CHA AKIBA NA MIKOPO OFISI YA WAZIRI MKUU (MAKAMU SACCOS) KUWA WABUNIFU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama ameshauri uongozi wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Ofisi ya Waziri Mkuu (Makamu Saccos) kuwa na ubunifu katika utendaji ili kuleta manufaa zaidi kwa wanachama wake.

Mhe. Mhagama ameyasema hayo wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wanachama wa Chama hicho uliofanyika Januari 19, 2017 mkoani Dodoma.

Katika Mkutano huo Mhe. Waziri alisisitiza kuwepo na mikakati madhubuti ya kubuni miradi itakayowezesha chama kuwa na vyanzo vyake vya mapato na kuwa na mikakati ya kuongeza wanachama wapya kwa kuzingatia umuhimu wa chama hicho.“Ni muhimu kuwa na mikakati madhubuti ya kubuni miradi, kuongeza wanachama pamoja na kuwa na vitu vya kiupekee na vya kiufanisi vitakavyokisaidia chama kuwa imara katika utendaji wake”, alisema Waziri Mhagama.

Aliongeza kuwa chama hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wanachama wake amabapo wengi wao wamekuwa na maendeleo mbalimbali kutokana na uwepo wa fursa za mikopo isiyokuwa na masharti magumu.

“Chama kimekuwa mkombozi mkubwa kwa wanachama wake kwani wamekuwa wakikopa na kusaidia katika shughuli za kimaendele, ikumbukwe kuwa asilimia kubwa ya wafanyakazi wana maendeleo kwakuwa wanachukua mikopo mbalimbali inayowasaidia kuwepo na maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja”, alisisitiza Mhe.Mhagama.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Joseph Muhamba aliahidi kuyachukua mapendekezo yote yaliyotolewa na Mhe.Waziri na kuyaweka katika vitendo ili kuhakikisha chama kinaongeza mbinu za ubunifu ikiwemo eneo la kuongeza wanachama wapya na kuweka mazingira mazuri zaidi kwa wanachama waliopo.

Mhe. Mhagama aliahidi kutoa ushirikiano wake kwa Chama hicho na kueleza kuwa chama kiitumie fursa ya Serikali kuhamia Dodoma kama chachu ya kuongeza wanachama wapya.

 “Ninawaahidi kuwapa ushirikiano wa hali na mali na kuamini kuwa chama hiki ni msaada mkubwa kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwani kipo kisheria kabisa na zipo kanuni zinazoelekeza juu ya uwepo wa chama na kwa kuonesha mfano mimi na Naibu Waziri Mhe. Dkt. Possi tunajiunga rasmi hii leo ili kuwa mstari wa mbele kukisaidia chama hiki”. Alisema Mhe. Mhagama.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akisalimia wanachama waChama cha Akiba na Mikopo Ofisi ya Waziri Mkuu (hawapo pichani) wakati wa Mkutano wao wa mwaka Uliofanyika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma tarehe 19 Januari, 2017.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza jambo wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Wanachama wa Chama cha Akiba na Mikopo Ofisi ya Waziri Mkuu Januari 19,2017 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma.
 Baadhi ya wajumbe Chama cha Akiba na Mikopo Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia maelekezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa Mkutano wa kwanza wa mwaka Januari 19, 2017 Mkoani Dodoma.
 Mkurugenzi Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Issa Nchasi akizungumza jambo wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wanachama wa Akiba na Mikopo wa Ofisi hiyo Mkoani Dodoma Januari 19, 2017.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akikabidhi ada ya uanachama na hisa zake kwa Katibu wa chama Bi. Algensia Ngalapa mara baada ya kuamua kujiunga rasmi na Chama cha Akiba na Mikopo Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa Mkutana wao Januari 19, 2017 Dodoma.
 Mwenyekiti wa Chama cha Akiba na Mikopo Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Joseph Muhamba akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama wakati wa Mkutano wa chama hicho mkoani Dodoma tarehe 19 Januari, 2017.
 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri (watu wenye Ulemavu) Mhe. Dkt. Abdallah Possi akizungumza wakati wa mkutano wa Wanachama wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Ofisi ya Waziri Mkuu kilichofanyika Ukumbi wa Mikutano hiyo Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (wa pili kutoka kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Ofisi ya Waziri Mkuu, Kulia kwake ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri (watu wenye Ulemavu) Mhe. Dkt. Abdallah Possi na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Joseph Muhamba. PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU

No comments:

Post a Comment