Wednesday, January 11, 2017

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA AWEKA JIWE LA MSINGI KATIKA MRADI WA UJENZI WA NYUMBA 252 ZA MAKAZI MBWENI ZANZIBAR


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimwa Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) uchangamkie fursa za uwekezaji wa ujenzi wa nyumba za makazi Tanzania Bara hasa kwenye Makao Makuu ya nchi Dodoma hatua ambayo itauwezesha mfuko huo kuongeza maradufu mtaji wake kwa uuzaji wa nyumba hizo.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati anaweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba 252 za makazi katika eneo la MBWENI kisiwani Unguja ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Makamu wa Rais amesema kutokana na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na mfuko huo wa ZSSF hasa ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi ni muhimu kwa mfuko huo kuangalia namna bora ya kwenda kuwekeza katika mikoa mbalimbali ya Tanzania bara kutokana maeneo mengi kuwa na mahitaji makubwa ya nyumba za makazi.

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema ujenzi wa nyumba za makazi Tanzania Zanzibar ulitokana na fikra na ahadi za hayati mzee Karume kupitia ASP wakati wa haraka za kudai uhuru za kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora ya kuishi katika kisiwa cha Pemba na Unguja kutokana na idadi kubwa ya wananchi katika kipindi hicho kuishi katika mazingira yasiyoridhisha.

“Miradi yote hii ni katika kuenzi utekelezaji wa kauli ya Mapinduzi Daima yanayotaka kuleta maendeleo yanayoonekana kwa wananchi kila uchao hususani kipindi hiki tunapotimiza miaka 53 ya Mapinduzi yetu ya Matukufu ya Zanzibar”

Makamu wa Rais pia amewahimiza wananchi wote wachangamkie fursa za kununua na kumiliki nyumba kwa bei nafuu na zenye miundombinu ya kisasa na huduma zote za kijamii ikiwemo viwanja vya michezo.

Kuhusu umiliki wa nyumba kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameziagiza Wizara zinazoshughulika na masuala ya ardhi Tanzania Bara na Zanzibar kutoa ufafanuzi au tafsiri sahihi ya sheria zinazoongoza masuala ya ardhi na umiliki wa nyumba ili kuondoa sintofahamu iliyopo kuhusu wana diaspora kumiliki nyumba.

Amesisitiza kuwa Serikali zote mbili zimekuwa zikisisitiza wana diaspora kuchangia maendeleo ya nchi na kutumia fursa mbalimbali zilizoko nyumbani ikiwemo kununua nyumba zinazojengwa na mifuko na mashirika mbalimbali hivyo ni muhimu kwa wizara zinazoshughulikia masuala ya ardhi kutoa maelekezo haraka ili kuondoa sintofahamu iliyopo kwa sasa kuhusu wana diaspora kulimiki nyumba kwa ajili ya makazi.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema ni muda muafaka sasa hivi kwa mifuko hiyo kuwekeza katika sekta ya viwanda hasa kwenye miradi yenye tija kwani viwanda vitatoa fursa kwa vijana wengi kuajiriwa na kuongeza kipato na kuongeza huduma za kijamii na kupunguza umaskini kwa wananchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipngo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt Khalid Salum Mohamed amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Serikali hiyo inaendelea kumuezi Mzee Karume kwa vitendo kwa kujenga nyumba za makazi na kukarabati nyumba zilizopo ili kuhakikisha wananchi katika Kisiwa cha Pemba na Unguja wanapata makazi bora ya kuishi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba 252 za makazi zinazojengwa na Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) zilizopo Mbweni, Zanzibar ikiwa moja ya maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan akihutubia mara tu alipoweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba 252 za makazi zinazojengwa na Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) zilizopo Mbweni, Zanzibar ikiwa moja ya maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan akiwa ndani ya moja ya nyumba hizo 252 mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba hizo za Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) zilizopo Mbweni, Zanzibar ikiwa moja ya maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan akiangalia ramani ya ujenzi wa nyumba 252 za makazi zinazojengwa  na Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) zilizopo Mbweni, Zanzibar ikiwa moja ya maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi.

Pichani ni Nyumba za makazi zinazojengwa na Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) zitakazokuwa na nyumba 252, Viwanja vya Michezo kwa Watoto,Sehemu ya kuogelea na Ukumbi mkubwa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan akfurahia jambo na wanafunzi waliojitokeza kushuhudia uwekaji wa  jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 252 za makazi zinazojengwa na Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) zilizopo Mbweni, Zanzibar ikiwa moja ya maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi.

No comments:

Post a Comment