Thursday, January 19, 2017

KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YATEMBELEA MAKAO MAKUU YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, MPINGO HOUSE

 Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki (kulia) akisalimiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Nditiye baada ya kuwasili makao makuu ya Wizara hiyo Mpingo House Jijini Dar es Salaam jana huku akiongozana na wajumbe wa kamati hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kushoto) akizungumza katika kikao cha Kamati ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii  katika ukumbi wa Ngorongoro wizarani hapo jana. Kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Ramo Makani, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kemilembe Lwota, Mwenyekiti wa Kamati, Mhandisi Atashasta Nditiye, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Aloyce Nzuki.
Kikao kikiwa kinaendelea katika ukumbi wa Ngorongoro, Makao Makuu ya Wizara hiyo, Mpingo House, Jijini Dar es Salaam.
 Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Idara ya Wanyamapori, Bw. Robert Mande akiwasilisha taarifa kuhusu taratibu za uhifadhi wa ghala la meno ya tembo kwa Kamati ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii katika ukumbi wa Ngorongoro makao makuu ya Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam leo.
 Baadhi ya wajumbe wa kamati ya bunge Ardhi, Maliasili na Utalii katika kikao hicho. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki.
 Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo.
Baadhi ya wakurugenzi wa Idara katika Wizara ya Maliasili na Utalii, wakifuatilia mjadala kwenye kikao hicho.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge.
 Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge.

NA HAMZA TEMBA - WMU
...........................................................................

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imetembelea makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mpingo House jijini Dar es Salaam leo na kuzuru ghala la nyara za Serikali kuona utunzaji wa meno ya tembo na changamoto zake.

Kabla ya kutembelea ghala hilo kamati hiyo ilipokea taarifa maalum ya wizara juu ya mchakato mzima wa taratibu za ukusanyaji wa meno ya tembo, usafirishaji, uhakiki, usajili kwenye mfumo maalum wa kielektroniki, uhifadhi wake na ulinzi thabiti wa ghara hilo.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa hiyo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Idara ya Wanyamapori, Bw. Robert Mande alisema meno yanayohifadhiwa katika ghala hilo ni yale yanayotokana na vifo asilia, kuuawa kutokana na uharibifu wa mali na maisha ya binadamu na yale yanayotokana na ujangili.

Waziri wa Maliasili na utalii, Prof. Jumanne Maghembe akijibu moja ya swali la wajumbe wa kamati hiyo ambao walitaka kujua uwezekano wa kuuza meno hayo ya tembo yaliyohifadhiwa ili kulipatia taifa mapato,  amesema msimamo wa Serikali ya Tanzania kwa sasa sio wa kuuza wala wa kuchoma meno hayo.

"Msimamo wetu ni kama ule wa nchi za Kenya, Uganda, Zambia, Malawi na Msumbiji wa kutokuuza meno haya kwa sasa kwasababu mbalimbali za kimsingi kabisa, moja ikiwa ni sababu za kiutafiti ambapo vinasaba vya meno ya zamani vinaweza kutumika kubaini mambo mbalimbali ikiwemo utafutaji wa dawa ya magonjwa ya tembo”, alisema.

Alisema kitendo cha kuuza meno hayo pia ni kuchochea zaidi biashara hiyo kwakuwa kitaongeza upatikanaji wa bidhaa hiyo kwenye masoko hivyo kuendelea kuipa uhai biashara hiyo haramu duniani.

Hapo awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Generali, Gaudence Milanzi akizungumza kwenye kikao cha kamati hiyo mkoani morogoro kilichohusisha uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) alisema ujangili hapa nchini kwa sasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba nyara zinazokamatwa kwa sasa ikiwemo meno ya tembo ni za zamani zilizokuwa zikisubiria kusafirishwa nje ya nchi.

Alisema hatua hiyo ya kupungua kwa uhalifu huo imefanikiwa kutokana na kazi kubwa inayofanywa vikosi maalum vya Askari wa wanyamapori vya kudhibiti ujangili kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini.

Alisema hatua ya Serikali ya China kupiga marufuku biashara ya meno ya tembo nchini humo ni jambo la kupongezwa na kwamba uamuzi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msukumo wa vitendo vya ujangili nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Naye mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Nditiye amewapongeza viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii namna walivyojipanga katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo na kuwaahidi ushirikiano kutoka kwa kamati yake.

Aliahidi kutoa ushirikiano kwa uongozi wa wizara hiyo katika kuhakikisha kuwa wanaikabili changamoto kubwa ya uvamizi wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi. "Sisi tunaungana na nyie, hatukubali mifugo kwenye hifadhi zetu, kwakuwa zinaharibu ubora wa hifadhi hizo, tunawaahidi ushirikiano wa kukabiliana ma changamoto hiyo"

Kamati hiyo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilitembela pia makao makuu ya Wakala ya Mbegu za Miti Tanzania (TTSA), Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) zote za mkoani Morogoro.


No comments:

Post a Comment