Thursday, January 5, 2017

HALMASHAURI YA CHALINZE YASHIRIKIANA NA RIDHIWANI KUWAPIGA TAFU WENYEVITI WA VIJIJI/VITONGOJI

Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze, Saidi Zikatimu, akizungumzia mikakati waliyojiwekea kuwalipa posho wenyeviti wa vijiji na vitongoji sanjali na kuinua mapato ya ndani
Mbunge wa  Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete.
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
HALMASHAURI ya mji mdogo wa Chalinze,mkoani Pwani,imetenga kiasi cha sh.mil 36 katika kipindi cha mwaka 2016/2017 kwa ajili ya kuwalipa posho wenyeviti wa vijiji na vitongoji katika halmashauri hiyo.
Kati ya fedha hiyo wenyeviti hao wanalipwa kila mmoja sh.30,000 kwa mwezi hadi mwezi july mwaka huu itakapokoma bajeti hiyo.
Akizungumzia kuhusiana na mpango huo,kwa waandishi wa habari mjini hapo,mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Chalinze ,Said Zikatimu ,alisema halmashauri hiyo imeamua kuwalipa posho wenyeviti hao kwani wanafanyakazi kubwa ndani ya miaka mitano bila kuambulia chochote.
Alisema wameshirikiana na mbunge wa jimbo la Chalinze,Ridhiwani Kikwete,kuona namna ya kuwatupia jicho wenyeviti hao wa vijiji na vitongoji  .
Aidha Zikatimu alieleza kwamba ,fedha hizo zitawawezesha wenyeviti hao kujikimu na kuondokana na hali ya kuuza ardhi za vijiji kwa visingizio vya kukosa posho ama mishahara.
Alibainisha ,fedha hiyo pia itaweza kuwasaidia wenyeviti hao kuwa na morali na ari ya kuchapakazi kwenye maeneo yao  na wamejipanga kila mwaka watakuwa wakitenga fedha hizo.
“Kiasi hiki cha sh.mil.36 ni fedha watakazolipwa hadi july 2017 na bajeti inayofuata tutaangalia kama kuna uwezekanao wa kuongeza kiasi kilichopangwa katika bajeti hii ama ibakie kiasi kilichotengwa kwenye bajeti hii”alifafanua Zikatimu.
Hata hivyo Zikatimu alisema ,wanachotarajia ni wenyeviti hao kuendelea kuwa wasimamizi wazuri katika vyanzo vya mapato na kuachana na tabia ya kuuza maeneo ya vijiji kinyume na taratibu.
Alisema wanawahamasisha kusimamia vyanzo vya mapato ili kuinua makusanyo hasa ya vyanzo vya ndani ikiwemo vizuizi mbalimbali vya pembezoni na ndani ya mji huo.
Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa halmashauri nyingine nchini kuwaangalia wenyeviti hao kwani kwa Chalinze imeshaleta tija ndani ya miezi sita tangu kuanza kwa mpango huo.


Aliiomba serikali na halmashauri hizo ziangalie namna ya kuwatengea fedha wenyeviti wa vijiji na vitongoji kama ilivyo kwa madiwani na wabunge wanavyotengewa posho wakimaliza muda wao,ili waweze kuwa na moyo wa kufanya kazi pasipo kukosa chochote.
“Halmashauri ni sehemu ya kwanza na serikali kuu ni sehemu ya pili,hivyo halmashauri zionyeshe nia ili serikali ilione hili,kwa kuwapa kipaombele ya kuwatengea fedha bila kuwaacha”
Zikatimu alisema wenyeviti hao wanasimamia chaguzi mbalimbali na ilani ya CCM hivyo waangaliwe katika suala hilo ili waweze kujiona ni viongozi wanaoaminika kwenye maeneo yao.

No comments:

Post a Comment