Tuesday, January 10, 2017

Gambo awasihi Wizara ya Kilimo kusitisha kutoa vibali vya Kusafirisha Mahindi Nje ya Nchi

Nteghenjwa Hosseah, Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameitaka Wizara ya Mifugo, Chakula na Ushirika kuacha kutoa vibali vya kusafirisha mahindi nje ya nchi kwa wafanyabiashara wa hapa nchini kwani Serikali Mkoani Arusha ilishapiga marufuku usafirishwaji wa mahindi hayo nje ili kulinda viwanda vya hapa nchini.

Mhe. Gambo alisema hayo jana baada ya kutembelea maghala matatu ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula{NFRA} Kanda ya Arusha kujionea hali halisi ya uhifadhi wa mahindi katika maghala hayo na kuskiliza changamoto zake na kukuta tani 6,620 za mahindi zilizoko kwa sasa.

Alisema serikali Mkoani Arusha ilishapiga marufuku uuzwaji wa mahindi nje ya nchi lakini kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekamatwa na vyombo vya ulizni na usalama wakiwa na vibali kutoka Wizarani vinavyowaruhusu kupeleka mahindi nchi jirani ya Kenya hali inayowafanya watendaji wa serikali kushindwa kufanya kazi kutokana na mkanganyiko huo.

Mkuu huyo alisema uamuzi wa kupiga marufuku uuzwaji mahindi nje ulitolewa na serikali kuu na Mkoa ulisimamia hilo kwa lengo la kuvilinda viwanda vya hapa nchini kwa uzalishaji wa bidhaa hivyo na kunufaika na unga na pumba za mahindi tofauti na ilivyo sasa.

Alisema kutokana na mkanganyiko huo aliwaomba watendaji wa Wizara kuacha kutoa vibali kwa wafanyabiashara kuuza mahindi nje ili kuwasaidia wenye viwanda vya nafaka kuuza unga na pumba nje wenye kiwango ili nao waweze kupata faida na nchi iweze kupata faida zaidi.

Mhe. Gambo alisema mbali ya hilo pia serikali Mkoani Arusha imefanikiwa kuziba njia zote za panya zilizokuwa zikitumika na wafanyabiashara kutorosha mahindi kwenda nchi jirani ya Kenya na kusema kuwa hilo nalo linapaswa kuungwa mkono na Wizara ili amri hiyo iweze kutekelezeka.

‘’Vibali vya Wizara kwa wafanyabiashara kuuza mahindi nje vinatuchanganya sana na vinapingana na amri yetu na nchi kwa ujumla na kutokana na hali hiyo tunaiomba wizara iache kufanya hivyo kwa maslahi ya nchi na wafanyabishara wa ndani ili waweze kuuza unga badala ya mahindi kwani watanufaika zaidi’’alisema Gambo

Naye Meneja wa NFRA Kanda ya Arusha, Abdillah Nyangasa alikitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, alisema kuwa zoezi la ununuzi lililoanza agosti 25 mwaka jana na kumalizika novemba 30 mwaka huo huo malengo yalikuwa kununuwa mahindi tani 15,000 lakini walifanikiwa kununuwa mahindi tani 5,111 tu na hiyo ni kutokana na ufinyu wa bajeti.

Nyangasa alisema changamoto iliyowakabili katika kipindi cha ununuzi kipindi hicho ilikuwa uzalishaji mdogo wa nafaka hususani mahindi ambo haukwenda sambasamba na mahitaji au matumizi ya kukidhi nchi na hali hiyo ilichangia sana bei ya mahindi au unga kupanda kwa kasi kubwa kwenye soko lake karibu nchi zima.

Alisema changamoto nyingine ni udhibiti mdogo wa soko la mahindi kwenye maeneo ya mipakani kwani kumekuwa na njia nyingi zizizo rasmi maarufu kwa njia ya panya kwa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na mahindi mengi yamevuka kwenda nchini Kenya kitu ambacho yangesaidia sana uhaba mkubwa wa chakula ulioko sasa endapo yangedhibitiwa.

Meneja huyo alisema kutokana na ununuzi mdogo wa mahindi Kanda ya Arusha NFRA makao makuu inaanga lia uwezekano wa kuongeza akiba hiyo kwa kuhamisha sehemu ya akiba yake kutoka katika kanda zake za Nyanda za Juu Kusini ambazo ununuzi wake ulikuwa wa kuridhika kidogo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo (Pili kushoto) akiwasili katika Ofisi za Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula Kanda ya Kaskazini zilizoko Mkoani Arusha kuangalia na kukagua hali ya uhifadhi wa Chakula.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo(kwanza kushoto) pamoja na Meneja wa NFRA Kanda ya Kaskazini Ndg.Abdillah Nyangasa wakitembelea maghala ya kuhifadhia Chakula wakati wa ziara yake katika Ofisi hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo(kwanza kulia) akikagua taarifa za mazao yaliyohifadhiwa katika Magahala ya NFRA wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya Uhifadhi wa Chakula.
Kutoka kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Ndg. Richard Kwitega akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo na Meneja wa NFRA Ndg. Abdillah Nyangasa wakati wa kikao na wafanyakazi wa NFRA Kanda ya Kasikazini.

No comments:

Post a Comment