Tuesday, October 25, 2016

WAZIRI WA BIASHARA VIWANDA NA MASOKO BALOZI AMINA SALUM ALI AZINDUA BARAZA JIPYA LA KUSIMAMIA MFUMO WA UTOWAJI LESENI



Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar 25.10.2016

Baraza jipya la Kusimamia Mfumo wa Utoaji Leseni (BLRC) limeagizwa kusimamia mfumo huo kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2013 ili kuondosha kasoro zilizojitokeza katika mfumo wa zamani na kurahisisha ufannyaji wa biashara Zanzibar.

Waziri wa Biashara,Viwanda na Masoko Balozi Amina Salum Ali ametoa maagizo hayo Ofisini kwake Migombani alipokuwa akizindua Baraza hilo lenye wajumbe 13 kutoka Taasisi za Serikali na watu binafsi likiongozwa na Mwenyekiti wake Vuai Mussa Vuai.

Amesema mfumo uliokuwa ukitumika wa utoaji leseni za biashara ulikuwa sio rafiki kwa wadau, ni wenye unaurasimu na unachukua muda na pia unagharama kubwa katika upatikanaji wa baadhi ya leseni.

Ametaja kasoro nyengine za mfumo wa zamani wa utoaji leseni kuwa ni kuwepo kwa sheria na vyombo vingi vya utaji leseni, kutokuwepo msimamizi wa vyombo hivyo na kuwepo kwa aina tofauti za leseni, vibali au ruhusa ya kuendesha biashara ambazo zote zina lengo moja.

Balozi Amina amelitaka Baraza hilo katika kutekeleza majukumu yake kuondosha urasimu na kupunguza muda katika utaratibu wa kuomba na utoaji leseni, kusimamia utaratibu rahisi na wa kupunguza gharama katika upatikanaji wa leseni na kuwepo masharti ya kusimamia biashara.

Aidha amelielekeza Baraza kuzingatia misingi na vigenzo katika utoaji wa leseni, kusimamia uanzishaji wa mfumo wa kielektroniki katika utoaji wa leseni kwa mamlaka zinazotoa leseni na kuhakikisha malipo ya leseni yanalipwa kupitia benki kila inavyowezekana.

Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko amelishauri Baraza kuanzishwa daftari maalum la leseni, vibali na ruhusa nyengine katika katika kuendesha biashara na kupendekeza mfumo bora wa utoaji leseni za biashara kwa kuzingatia mazingira ya nchi nyengine zenye kufafana na Zaznzibar.

Amesema Wizara yake imegundua zipo biashara nyingi zimepewa leseni bila kusajiliwa kwa wakala wa usajili hivyo ametaka kuhakikisha biashara zote  zinasajiliwa kwa wakala wa usajili wa Biashara na Mali kabla ya biashara hizo kupewa leseni.

Mwenyekiti wa Baraza la Kusimamia Mfumo wa utoaji Leseni Vuai Mussa Vuai amemuhakikishia Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko kuwa Baraza hilo litafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha malengo ya kuazishwa kwake yanafikiwa. Ameahidi kuwa watafuata sheria na kanuni za mfumo huo mpya wa utoaji wa leseni za biashara ili kupunguza kasoro nyingi zilizojitokeza katika katika mfumo uliokuwa ukitumika kabla.

No comments:

Post a Comment