Monday, October 3, 2016

WAZIRI MKUU ABAINI GYPSUM ZA NJE HAZITOZWI KODI

gyp2
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akikagua  uzalishaji katika kiwanda  cha Gypsum cha Premalt cha mjini Dodoma wakati alipokitembelea Oktoba 2, 2016. (Picha na ofisi ya Wairi Mkuu)


*Aahidi kufuatilia suala hilo, asema lazima zitozwe kodi kulinda soko la ndani
*Apokea mchango wa sh. milioni moja kwa ajili ya waliopatwa na maafa Kagera

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atafuatilia ili ajue chanzo ni kwa nini bidhaa za gypsum zinazoagizwa kutoka nje ya nchi hazitozwi kodi.

Waziri Mkuu ametoa ahadi hiyo jana jioni (Jumapili, Oktoba 2, 2016) wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa kiwanda cha Premalt Limited kinachotengeneza unga wa gypsum (gypsum powder) aina ya Afri Bond mara baada ya kukagua kiwanda hicho kilichopo Zuzu nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Waziri Mkuu alisema: “Gypsum inayozalishwa Dodoma ina ubora kama ile inayozalishwa Mchinga, kule Lindi na hakuna gypsum yenye ubora kama huo hapa Afrika isipokuwa gypsum ya Tanzania.”

“Nilikuwa sielewi ni kwa nini gypsum ya wenzetu ilikuwa inakimbiliwa, lakini sasa nimetambua; ilikuwa na bei nafuu kwa sababu tumetoa kodi. Sasa hivi, hili jambo nalibeba, naenda kulishughulikia”.

“Nimeangalia kwenye orodha niliyopewa katika madini yote nimekuta kodi ya gypsum ni asilimia sifuri. Ni lazima tuweke kodi ili tutengeneze soko zuri kwa gypsum inayozalishwa hapa nchini. Ni lazima tuweke kodi kwenye madini yetu mengine kama makaa ya mawe ili tutengeneze soko zuri,” alisema.

Alisema wakazi wa Dodoma wamepata fursa kutokana na uwepo wa kiwanda kama hicho kwani kiwanda kinahitaji mali ghafi kwa hiyo ni jukumu la wakazi wake kuchangamkia fursa ya uchimbaji wa madini hayo.

“Natambua kwamba Mkurugenzi wa kampuni hii ataleta mitambo mikubwa zaidi hivi karibuni. Nendeni benki mkakope ili muweze kununua zana za kuchimbia madini haya. Yeye ukishafikisha hapa, ananunua ili aanze kusaga na kupata unga wa gypsum,” alisema.

Alitumia fursa hiyo pia kumpongeza mmiliki wa kampuni ya STJ Enterprises, Bi. Adella Nungu ambaye ni mmoja wa wajasiriamali wa Kitanzania wanaotumia gypsum kutoka Dodoma na kutengeneza mapambo mbalimbali ya kuezekea ndani ya nyumba. Bi. Nungu alikuwepo kiwandani hapo.

Bi. Nungu alisema anaponunua unga wa gypsum kutoka Dodoma, kwa wastani anaweza kutengeneza bidhaa za tani 20 hadi 25 kwa mwezi kutegemea na hali ya soko na oda kutoka kwa wateja wake

Mbali ya kutengeneza mapambo ya kuezekea, unga wa gypsum hutumika pia kutengeneza ‘muhogo’ (Plaster of Paris-POP) unaotumika kuwafunga wagonjwa waliovunjika mifupa kama sehemu ya matibabu yao.

Mapema, akisoma risala kwa niaba ya uongozi wa kampuni ya Premalt Limited, Bw. Mohammed Ameir Mbaraka alisema wamefanya utafiti na kubaini kuwa makontena ya gypsum yenye tani zaidi ya 3,000 yanaingizwa nchini bila kutozwa kodi.

“Tumegundua kuwa gypsum inayoingizwa kutoka nje ya nchi ni miongoni mwa bidhaa ambazo hazitozwi kodi. Serikali ikiruhusu hali hii iendelee, itaathiri ajira za watumishi hapa kiwandani,” alisema.

Alisema mawe ya madini ya jasi (gypsum) yanachimbwa katika kijiji cha Manda wilayani Chamwino, kilichopo umbali wa km. 80 kutoka Dodoma mjini.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Manda, Bw. Kambona Pius Matonya alimweleza Waziri Mkuu kwamba kijiji hicho kina wakazi zaidi ya 300 ambao wengi wao wanajishughulisha na uchimbaji wa madini hayo lakini wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa soko.

“Kijiji chetu kipo katika jimbo la Mtera. Asilimia kubwa ya wakazi wanafanya kazi ya kuchimba jasi (gypsum) lakini changamoto kubwa kwetu ni soko. Wanakijiji wanachimba jasi nyingi kuliko uwezo wa kiwanda,” alisema.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amepokea mchango wa sh. milioni moja kutoka Mkurugenzi wa Kampuni ya Premalt Limited, Bw. Anand Chandra zikiwa ni mchango wao kwa ajili ya wakazi wa Bukoba walioathirika kwa tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 10, mwaka huu.



IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.

JUMATATU, OKTOBA 3, 2016

No comments:

Post a Comment