Wednesday, October 5, 2016

WAFANYABIASHARA MKOANI SIMIYU WAHIMIZWA KUSAJILI BIASHARA NA MAKAMPUNI


Na Stella Kalinga, Simiyu

Wafanyabiashara Mkoani Simiyu wamehimizwa kusajili na kurasimisha biashara zao ili zitambulike na kupata fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikopo. 

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati wa ufunguzi wa Semina ya Uhamasishaji ya majukumu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) katika Ukumbi wa Mikutano wa Kanisa Katoliki Mjini Bariadi.

Mtaka amesema katika kuunga mkono Juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli za kuifikia Tanzania ya Viwanda, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wana nafasi kubwa ya kuwaandaa Watanzania kupokea mabadiliko hayo na kuona umuhimu wa kusajili biashara zao.

Aidha, Mtaka amesema Mkoa wa Mkoani Simiyu umedhamiria kuwa Mkoa wa mfano kwa kutekeleza, ambapo kwa sasa umeanza kuzalisha chaki na maziwa na umejipanga kuanzisha viwanda vidogo na vya kati vitakavyozalisha bidhaa ambazo malighafi yake yanapatikana nchini ambazo ni bandeji, pamba za hospitali, pamba za hospitali na maji ya dripu.

Mtaka amesema katika mwaka 2016/2017 mkoa wa Simiyu utatimiza azma yake ya kila wilaya kuzalisha bidhaa moja (one district one product) na biashara hizo zote zitasajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA). 

“Nimesema, nimechagua Mkoa wa Simiyu kuwa Mkoa kiongozi wa kuiongoza nchi hii kufikia malengo ambayo watu huko Duniani wanatarajia kuyaona kupitia Mhe. Rais wa Tanzania, ningetamani kuona mkoa wa Simiyu unakuwa miongoni mwa mikoa mitano ya mfano na ya kutumainiwa kibiashara nchini, haya malengo tutayafikia kwa kushirikiana na ninyi” alisema Mtaka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga amesema endapo Wafanyabiashara watasajili na kurasimisha biashara na makampuni yao wataepuka hasara zisizo za lazima kwa kuwa wataajiri watu watakaowasaidia kuendesha biashara na makampuni yao kitaalamu.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Frank Kanyus amesema wanaendelea kutoa elimu na kuwahamasisha wafanyabiashara kusajili majina ya biashara na makampuni nchini na Mkoa wa Simiyu umekuwa mkoa wa nne kufikiwa na fursa hii.
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, katika ufunguzi wa Semina ya Uhamasishaji ya majukumu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Mjini Bariadi.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Frank Kanyus akizungumza na Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, katika ufunguzi wa Semina ya Uhamasishaji ya majukumu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Mjini Bariadi.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA)Frank Kanyus (kushoto) na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara mkoa wa Simiyu,  Njalu Silanga wakifuatilia hotuba ya ufunguzi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, katika Semina ya Uhamasishaji ya majukumu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Mjini Bariadi
 Baadhi ya Wafanyabiashara wa mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika ufunguzi wa Semina ya Uhamasishaji ya majukumu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Mjini Bariadi
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara na Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga, akizungumza na Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, katika ufunguzi wa Semina ya Uhamasishaji ya majukumu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Mjini Bariadi.

No comments:

Post a Comment