Wednesday, October 5, 2016

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora walaani mauaji ya watafiti watatu huko Iringa na Mvumi, Dodoma


Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuuwawa kwa watafiti watatu (3) wakiwa kazini, tukio lililotokea Oktoba mosi mwaka huu katika kijiji cha Iringa-Mvumi, Wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma.

Tume inalaani vikali mauaji haya ya kikatili ya watu wasiokuwa na hatia na yenye kuitia aibu nchi yetu. Aidha, inaungana na watanzania wengine nchini kuwapa pole wafiwa na wote walioguswa na msiba huu.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari watafiti hao kutoka Chuo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo ya Ardhi cha Selian, Arusha wakiwa kijijini hapo kukusanya sampuli za udongo kwa ajili ya utafiti walivamiwa na kundi la wanakijiji na kushambuliwa kwa mapanga na silaha za jadi na kisha kuchomwa moto kwa imani kwamba eti walikuwa wanyonya damu. 

Haki ya kuishi kama zilivyo haki nyingine, inalindwa na sheria na hakuna mtu anayepaswa kuporwa haki hii ya msingi kiholela. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 14, kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria. 

Pia Mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeridhia inatoa ulinzi juu ya haki ya mtu kuishi. Baadhi ya Mikataba hiyo ni: Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu la 1948 (Kifungu cha 3) na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa 1966 (Kifungu cha 6) vinavyoeleza kuwa kila mtu anayo haki ya asili ya kuishi, inayolindwa kisheria na hakuna atakayenyimwa haki hii ya msingi kiholela.

Hivyo kuuwawa kwa watafiti hao wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao kwa taifa ni kitendo kinachopaswa kulaaniwa vikali na kila mwananchi anayethamini uhai na kuheshimu haki za binadamu.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa matukio ya wananchi kujichukulia sheria mikononi mwao ni jambo linalojirudiarudia na limekuwa likisababisha uvunjifu wa haki za binadamu na madhara makubwa kwa jamii, hususan kwa wanawake na watoto.

Hivyo basi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora:
1. Inaiomba Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kudhibiti mauaji ya kiholela nchini na kulipatia ufumbuzi tatizo la wananchi kutoheshimu sheria na kujichukulia sheria mkononi. 

2. Inawakumbusha wananchi kuwa vitendo vya ukatili, mauaji, na matendo yote yanayokiuka Sheria yanayofanywa na raia wasio wema ni ukiukwaji wa Sheria, haki za binadamu na misingi ya utawala wa sheira; Hivyo Tume inakemea matendo haya na kutaka yapigwe vita.

3. Inawataka wananchi kuheshimu mamlaka zilizopo katika maeneo yao na ngazi mbalimbali wakitambua kuwa ndio wenye dhamana juu ya masuala mbalimbali ya kiutendaji katika maeneo husika.

4. Inapendekeza Kamati za Ulinzi na Usalama katika ngazi za vijiji, vitongoji na kata, wakiwemo watendaji watimize wajibu wao ili kuepuka madhara kama haya kujirudia au kutokea katika maeneo mengine.

5. Pia inapendekeza watendaji wa taasisi za Serikali na binafsi wajitahidi kuzingatia utaratibu wa kutoa taarifa mapema, ikiwezekana kwa maandishi kwenye ngazi mbalimbali za uongozi katika maeneo wanayokwenda kufanyia kazi. Aidha, wazingatie utamaduni wa kujitambulisha kwa viongozi wa ngazi za chini na kuomba kupatiwa watu wa kuambatana nao katika kazi zao wawapo katika maeneo hayo. 

6. Vilevile inaona ipo haja ya elimu zaidi kutolewa kwa umma juu ya masuala ya haki za binadmu na wajibu, sheria, utawala bora na uraia.

7. Inalipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua za kuwakamata watuhumiwa haraka. Aidha, inaliomba jeshi hilo lifanye uchunguzi wa kina na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wote watakaobainika kuwa walihusika na mauaji na uharibifu wa mali uliotokea katika tukio hili.

8. Mwisho, Tume inatoa wito kwa wananchi wa kijiji cha Iringa-Mvumi na maeneo mengine kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kuhakikisha wote waliohusika na unyama huu wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo husika ili sheria ichukue mkondo wake. 

Imetolewa na:
(SIGNED)
Mhe. Iddi Ramadhani Mapuri
Makamu Mwenyekiti 
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Oktoba 5, 2016.

No comments:

Post a Comment