Sunday, October 30, 2016

MWIJAGE: VIWANDA VIDOGO NA VYA KATI VIJENGWE KUKUZA SEKTA YA VIWANDA NA KUINUA PATO LA NCHI

WAZIRI wa viwanda ,biashara na uwekezaji ,Charles Mwijage (mb),akisaini kitabu kwenye banda la  SIDO baada ya kuzindua  maonyesho ya tisa  ya wajasiriamali mwaka 2016 ,yaliyoratibiwa na SIDO Kanda ya Mashariki yanayofanyika wilayani Bagamoyo (picha na Mwamvua Mwinyi)

Waanachi mbalimbali wakionekana kujitokeza kununua bidhaaa zilizotengenezwa kwa mikono ya wajasiriamali kutoka ndani ya Tanzania kwenye maonyesho ya tisa ya wajasiriamali mwaka 2016 ,yaliyoratibiwa na SIDO Kanda ya Mashariki ,yaliyofanyika wilayani Bagamoyo.(picha na Mwamvua Mwinyi)







WAZIRI wa viwanda ,biashara na uwekezaji, Charles Mwijage (mb),akitembelea mabanda mbalimbali ya wajasiriamali waliojitokeza kuuza bidhaa zao kwenye maonyesho ya tisa  ya wajasiriamali mwaka 2016 yaliyoratibiwa na shirika la  kuhudumia viwanda vidogo vidogo SIDO ,Kanda ya Mashariki,yanayofanyika wilayani Bagamoyo.


Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza jambo kabla ya kumkaribisha kuzungumza  na wananchi waziri wa viwanda,biashara na uwekezaji Charles Mwijage(mb)katika maonyesho ya tisa  ya wajasiriamali mwaka 2016 ,yaliyoratibiwa na SIDO Kanda ya Mashariki,wilayani Bagamoyo.


Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
WAZIRI wa viwanda ,biashara na uwekezaji ,Charles Mwijage(mb),amesema wakati serikali ikiendelea kusisitiza kukuza sekta ya viwanda na kuinua uchumi wa kati ni lazima kuanza na ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati.
Aidha ameitaka mikoa na wilaya kubaini na kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga viwanda pamoja na kuhamasisha wajasiriamali kuwa na uthubutu wa kujenga viwanda .
Akizindua maonyesho ya tisa (9)ya wajasiriamali mwaka 2016,yaliyoratibiwa na SIDO ,Kanda ya Mashariki,alisema mwaka 2013 viwanda vilivyokuwa vinafanya kazi ni zaidi ya 49,243 sawa na asilimia 99.15 .
Mwijage alisema kati ya viwanda hivyo ni vidogo sana,viwanda vidogo na vya kati hivyo kuna kila sababu ya kuendelea kuongeza wigo wa kuwa na viwanda hivyo kwenye maeneo mbalimbal .
Alieleza kuwa kulingana na taarifa zilizowahi kutolewa na bank ya dunia ilieleza kuwa nchi ya India viwanda vidogo ni asilimia 95.1 ambapo wajasiliamali wadogo na viwanda vidogo wanachangia asilimia 38 la pato la taifa.
Mwijage alisema Tanzania isije ikajibeza kwa takwimu za mwaka 2013 zilizopo kwani nchi nyingi duniani zimekuwa kiuchumi na kuongeza pato la taifa kutokana na viwanda vidogo na vya kati.
“Viwanda vidogo katika nchi ya China ni asilimia 90 ,Malaysia asilimia 98,Thailand asilimia 99,Ghana asilimia 97 ,Afrika ya kusini asilimia 97.7 ,Marekani ni asilimia 98.8 na Japan ni asilimia 98.7 .
Alisema ni lazima kulenga viwanda vidogo kwani vinapatikana kwa mitaji midogo na vipo vijijini na watanzania zaidi ya 70 wapo vijijini hivyo kwa kuwaondolea umaskini ni kuwapelekea viwanda na maendeleo.
“Wananchi wengi watapata maendeleo kwa kulima na kuuza kwenye viwanda lakini ukitumia nguvu nyingi na kwenda kuuza mjini kwa nusu gharama ujue umepigwa vidole”
“Mkoa wa Pwani unajenga viwanda vingi ikiwemo vya kusindika matunda,viwanda vya kuchakata matunda ,kwa hiyo kuna uhakika wa kupanua wigo wa soko nje na ndani ya nchi”alisema Mwijage.
Aliwaomba wajasiliamali hao kufunga bidhaa kwa ubora, kuwa na mbinu mpya hasa katika soko la ushindani hali itakayosaidia kukuza biashara na kupata masoko makubwa.

Alisisitiza kwamba Tanzania bila ya viwanda inawezekana ni msemo wa zamani kwasasa ni Tanzania inajenga viwanda na inawezekana.

Mwijage alieleza kikubwa ni kuainisha maeneo na viwanda vinavyojengwa katika wilaya husika kulingana na taswira ya wilaya na mkoa.
Alisema kikwazo kikubwa ni maeneo ya kufanyia shughuli ,na kuyaainisha kwani kosa kubwa linalofanywa na halmashauri za wilaya nyingi ambazo wanakimbilia kuyauza maeneo kwa kuyakata vipande na kuyauza kwa scare mita1 sh 10,000 heka moja mil. 60 .
Waziri huyo alisema vijana wanaotoka shule hawawezi kumudu gharama hizo hivyo kunufaisha watoto wenye uwezo pekee na kuwakandamiza wale hohehahe na hatimae kugeuka panyaroad .
Wakati huo huo ,Mwijage alisema anatarajia kupeleka makatibu wake watatu kwenda mikoani kuwasomea waraka wake wa waziri unalenga kuibua vijana wanaotoka shule kujifunza teknolojia ili waweze kujitegemea.
Alisema serikali za mikoa zisaidiane na serikali na ameahidi kuwapeleka katibu mkuu anaeshughulika na viwanda ,katibu mkuu anaedhughulikia uwekezaji na naibu katibu mkuu wa viwanda ,biashara na uwekezaji kwa ajili ya kuusemea waraka huo.
Alisema makatibu hao wataenda kushirikiana nao katika maeneo yaliyotengwa na halmashauri ili kutamia vijana mbalimbali na endapo watakua wataendelea kujitegemea.
Katika hatua nyingine Mwijage,aliwaalika wajasiliamali waliojitokeza katika maonyesho hayo kwenda kwenye maonyesho yanayotarajiwa kufanyika des 7 hadi des 11 mwaka huu,kwenye viwanja vya sabasaba.
Awali mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,alisema mkoa huo umejipanga kuwa ukanda wa viwanda na uwekezaji.

Alisema wakati jiji la Dar es salaam likiwa limejaa hakuna budi wakurugenzi na wakuu wa wilaya mkoani humo wakaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji.

Mhandisi Ndikilo alitoa rai kuboresha miundombinu kwenye maeneo ya wawekezaji ili kuwavutia kukimbilia mkoani hapo.
Nae mkurugenzi wa shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo (SIDO)prefesa Injinia Silvester Mpanduji,aliiomba jamii na wadau wa kibiashara kujenga tabia ya kununua bidhaa zinazotokana na ubunifu na mikono ya watanzania.
Alisema ni faraja kununua bidhaa za nchini kwani hazinatofauti na zile za nje ya nchi na zinauzwa kwa gharama nafuu.
Profesa Injiani Mpanduji,alisema SIDO ina mikakati mbalimbali ikiwemo madhubuti ya kuinua (kutotoa)vijana wajasiliamali wenye ubunifu na kujiamini katika soko la ushindani.
Alieleza katika maonyesho hayo wajasiriamali zaidi ya 200 kutoka mikoa ya kanda hiyo ikiwemo Pwani, Morogoro, Lindi, Dar es salaam na Mtwara na kutoka nchini Kenya wameshiriki kwenye maonyesho hayo.
Profesa Injinia Mpanduji,alisema  kauli mbiu ya maonyesho hayo ni uchumi wa viwanda unategemea viwanda vidogo .
Alisema maonyesho hayo yalianza octoba 26 hadi 31 ambapo yanatarajiwa kufungwa na mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo.

No comments:

Post a Comment