Wednesday, October 26, 2016

MUSWADA WA HUDUMA ZA HABARI USIPOTOSHWE-MSEMAJI WA SERIKALI

Na May samba-MAELEZO.

Mapema mwezi September mwaka huu muswada wa huduma za habari ulisomwa kwa Mara ya kwanza bungeni na kutolewa fursa kwa wadau wa habari kutoa maoni ili kuuboresha.

Takribani miezi miwili sasa imepita tangu wadau walipotakiwa kuusoma na kutoa maoni, lakini cha kushangaza wamekuja na sababu lukuki ikiwamo “ETI” kukosa muda wa kuusoma, Muswada wenye kurasa 28 tu.

Kimantiki wachambuzi wa masuala haya wanasema kuwa muswada huu unahistoria ndefu ya zaidi ya miaka 20 ambapo wadau katika sekta ya habari wamekuwa wakipigania kuipa heshima taalum hii na kuifanya kuheshimika kama fani za aina nyingine nchini.

Kwa kujua, kutojua au kwa makusudi wapo baadhi ya watu walio ndani ya tasnia ya habari na wasio wanatasnia wamekuwa wakivipotosha vifungu muhimu ndani ya muswada huu inawezekana kwa maslahi yao binafsi au kutumika na watu wenye nia mbaya na tasnia hii waliosahau maslahi mapana ya tasnia ya habari nchini.

Akizungumza kwa nyakati tofauti Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO  Bw. Hassan Abbas amesema lengo la muswada huu ni kuja na sheria itakayokuza na kuimarisha taaluma na weledi katika tasnia ya habari na kuweka mfumo wa usimamizi wa huduma za habari.

Jambo lingine lililoibua mjadala kwenye muswada huu ni kuhusu taaluma kwa waandishi wa habari ambayo imeibua hofu kwamba wanahabari wasiokuwa na kiwango cha elimu kwa ngazi ya shahada watafukuzwa, kuachishwa kazi au kutotambulika kama wanahabari.

Akilitolea ufafanuzi suala hilo Bw. Abbas amesema kuwa waandishi hawapaswi kuwa na hofu kwani kutakuwa na viwango tofauti vya utambuzi katika fani ya habari na pia kutatolewa muda wa miaka mitano kwa waandishi wa habari kujiendeleza.

Aidha Bw Abbas amesema kuwa masuala yote ya taaluma katika muswada huu yataainishwa katika kanuni zitakazoongoza tasnia hii na sio katika sheria.

Jambo la msingi kwa sasa ni kwa wadau wa habari kuungana kwa pamoja katika kutoa maoni ili kuuboresha muswada kwasababu haukandamizi bali ni muswada utaoleta mabadiliko chanya katika tasnia ya habari.

Mojawapo ya mambo yenye kuleta neema katika tasnia ni pamoja na uundwaji wa Bodi ya Ithibati ambayo lengo lake ni kuwa msimamizi wa kanuni za maadili ya wanahabari, viwango na mienendo ya kitaaluma pamoja na kuendeleza vigezo bora vya maadili na nidhamu miongoni mwa wanahabari.

Aidha, kutakuwa  na Mfuko wa Mafunzo kwa waandishi wa  habari ambao utawawezesha wanahabari kuongeza ujuzi katika fani yao na hatimaye kuleta matokeo chanya ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kusaidia katika uwajibikaji wa serikali.

Muswada huu pia  utakuza na kuchangia utafiti na maendeleo katika nyanja ya habari na  kuonesha wazi namna gani tasnia hii inaenda kulikomboa taifa kwa matumizi sahihi ya kalamu za waandishi tofauti na ilivyokuwa awali hali itakayopeleka kutoka kwenye uandishi wa mazoea na kufikia uandishi wenye nia ya kuwasaidia watanzania na serikali kwa ujumla kufikia malengo yanayotakiwa.

Mswada huo pia umelenga kumlinda mwandishi wa habari kwa kumtengenezea mazingira ya kuwa na Bima na Hifadhi ya Jamii kwa kuelekeza kila mwajiri aweke Bima na kuchangia katika Mifuko ya Hifadhi za Jamii kwa ajili ya waajiriwa wote wa chombo husika.

Suala hili limekuwa likipigiwa kelele na waandishi wenyewe kwa muda mrefu hasa kutokana na wengi kukosa huduma muhimu hasa za afya kutokana na kutokuwa na bima na imeshuhudiwa waandishi wengi wakipitia wakati mgumu hasa wamapopatwa na magonjwa.

Masuala mengine yaliyomo katika mswada huo ni uanzishwaji wa Baraza huru la Habari ambalo litasaidia kukuza maadili na viwango vya taaluma baina ya wanahabari na kampuni za habari na pia litakuwa kiungo kati ya wanahabari, vyombo vya habari pamoja na wadau wa habari.

Aidha, Muswada huu pia umekusudia kuwa kiungo kati ya serikali na wananchi kwa kiasi kikubwa ambapo wananchi wataweza kueleza hisia zao juu ya utendaji wa serikali.


Rai yangu kwa wanahabari nchini ni kuacha kulalamika na kutoa sababu bila kujenga hoja zitakazoboresha muswada huu kama inavyofanywa na baadhi ya watu, serikali ina nia njema ya kulimaliza suala hili lililodumu kwa takribani miaka 20 ili hatimaye taaluma hii iweze kutambulika rasmi.

No comments:

Post a Comment