Sunday, October 30, 2016

Mtanzania atunukiwa nishani na Rais wa Korea Kusini

Rais wa Korea Kusini, Park Geun-hye amemtunuku nishani ya heshima aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bw.Henry Clemens kwa kutambua juhudi zake katika kuleta maendeleo katika vijiji vya Mfuru Mwambao na Njianne kupitia mfumo Saemaul Undong (SMU) yaani kijiji kipya cha maendeleo.

SMU ni mfumo uliotumika Korea katika kujiletea maendeleo mpaka sasa kufika katika orodha ya nchi tajiri duniani. Mfumo huo unasisitiza swala la wananchi wenyewe kufanya kazi kwa kujitolea kwa ajili ya maendenelo yao wenyewe.Bw. Clemens ambaye ni mwenyekiti wa SMU Tanzania alisema wazo hilo alilipokea mwaka 2009 akiwa Mkuu wa wilaya ya Mkuranga na kulifanyia kazi katika vijiji viwili na kuleta matokeo mazuri.

“kumekuwa na maendeleo makubwa mara baada ya kutoa mafunzo kwa wanakijiji juu ya thamani ya ardhi na umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano,” alisema Bw. Clemens.Alisema uzalishaji wa mazao kama mhogo, papai na nazi umeongezeka kwa asilimia kubwa kutokana na ushirikiano wa wanavijiji wa Mfuru Mwambao na Njia nne.

“Kujitolea kwa wanakijiji katika kujiletea maendeleo kupitia dhana ya Saemaul Undong ndio imetupatia heshima kubwa ya kutunukiwa nishani na Rais wa Korea Kusini,” alisema Bw. Clemens.Akielezea matumaini yake alisema ni muhimu dhana hiyo ya Saemaul Undong ikaenea nchi nzima kwani inakwenda sawa na azma ya serikali ya kuondoa umasikini kwa kufanya kazi kwa bidii.

Wakati huo huo, Balozi wa Korea Kusini hapa nchini, Bw. Song Geum-Young mwishoni mwa wiki ametembelea kijiji cha Njia nne na kujionea maendeleo yaliyofikiwa na wananchi kwa kutekeleza dhana ya Saemaul Undong yaani kijiji kipya cha maendeleo.“Nimejionea maendeleo na changamoto hasa za miundombinu ya barabara na daraja ambavyo ni muhimu katika kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa huku” alisema balozi huyo. 

Alisema Serikali ya Korea Kusini imejipanga katika kujenga miundombinu nchini ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine katika kupata masoko ya bidhaa zao.Alisema amefarijika sana na maendeleo waliyoyafikia wanakijiji hao na kuwaomba waendelee kufanya kazi kwa bidii kwani mafanikio huja kwa kujitolea.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi, Sekta za Uchumi na Uzalishaji toka TAMISEMI, Dkt. Lucy Ssendi alisema atafikisha changamoto zinazowakabili wananchi wa Njia Nne hasa ya kukamilishiwa daraja linalounganisha kijiji hicho na Nyamihimbo.“Juhudi kubwa zimefanywa hadi sasa, nitafikisha taarifa hizo kwa mamlaka husika ili kufanikisha umaliziaji wa daraja,” alisema.

Mmoja wa wanakijiji wa Njia nne Bi. Zuwena Kasinde aliishukuru serikali ya Korea kwa kuchagua wilaya yao kuwa sehemu ya mfano wa mfumo wa SMU na kusema kuwa watakuwa mfano kwa Tanzania katika maendeleo kupitia dhana hiyo.

Mwenyekiti wa Saemaul Undong Tanzania(SMU), Bw.Henry Clemens akikambidhi zawadi kwa niaba ya wanakijiji wa Njianne, wilayani Mkuranga Balozi wa Korea Kusini Nchini Bw.Song Geum-young alipotembelea katika kijiji hicho kujionea maendeleo waliofikia kwa kupitia dhana ya Saemaul Undong yaani kijiji kipya cha maendeleo ambayo ndio dhana iliyowafanya wao kupiga hatua kiuchumi mpaka kufikia katika prodha ya nchi tajiri Duniani. Katikati ni mwasisi wa SMU Mchungaji Joshua Lee
Mwenyekiti wa Saemaul Undong Tanzania,(Mkuu wa Wilaya Mstaafu wa Mkuranga) Bw.Henry Clemens akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) medani ya heshima na cheti alichokabidhiwa na Rais wa Korea kusini Park Geun-hye kwa kutambua mchango wake wa kuviendeleza vijiji vya Mfuru mwambao na Njia nne vilivyopo Wilaya ya Mkuranga kupitia mfumo wa saemaul undong( kijiji kipya cha maendeleo).
Balozi wa Korea Kusini Nchini Tanzania Bw.Song Geum-young akipiga picha daraja linalounganisha kijiji cha Njia nne na Nyamihimbo wakati waziara yake katika kijiji hicho na kujionea maendeleo waliofikia kwa kupitia dhana ya Saemaul Undong yaani kijiji kipya cha maendeleo ambayo ndio dhana iliyowafanya wao kupiga hatua kiuchumi mpaka kufikia katika prodha ya nchi tajiri Duniani. Kulia ni Mbunge mstaafu wa Mbinga Magharibi Bw.Gaudence Kayombo. Kushoto ni mwasisi wa SMU Tanzania,Mchungaji Joshua Lee. Wapili kushoto Mwenyekiti wa Saemaul Undong Tanzania Bw.Henry Clemens

No comments:

Post a Comment