Tuesday, October 25, 2016

MD KAYOMBO AMUAGIZA AFISA MTENDAJI KUSIMAMIA MAPATO YA SOKO LA MBURAHATI KWA UAMINIFU


Afisa Mtendaji wa Kata ya Mburahati Jijini Dar es salaam ametakiwa kusimamia kwa uaminifu mapato ya soko Mburahati ili kuimarisha mapato ya Manispaa hiyo ambayo yataimarisha uboreshaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo wakati alipofanya ziara sokoni hapo kwa lengo la kujionea hali halisi ya soko pamoja na hali ya ukusanyaji wa mapato.
Sambamba na agizo hilo pia Mkurugenzi amemtaka Afisa Mtendaji huyo kwa kushirikiana na kamati ya soko Kuandaa orodha ya majina ya walipaji wote pamoja na kiasi wamachotakiwa kulipa, kutolewa namba pamoja na kuwepo na orodha ya kiasi kinachotakiwa kukusanywa kutoka katika maduka hayo, Kutoa mapendekezo mapya ya viwango vya tozo, na kuwepo na jina la kila mmiliki wa meza sokoni hapo na kiasi cha ushuru anacholipa.
MD Kayombo ametoa siku tano kwa Afisa Mtendaji huyo kwa kumtaka Kuwasilisha orodha ya watu wote wanaodaiwa tozo na kodi katika soko na vibanda pamoja na muda wanaodaiwa sambamba na Kutengeneza data base ya wafanyabiashara wote katika soko hilo.
Pamoja na ukaguzi huo Mkurugenzi alipata maelezo juu ya ukusanyaji mapato katika soko la Mburahati lililopo pembeni ya jengo la soko linalojengwa. Akisomewa taarifa ya soko hilo na katibu wa soko Ndg Fikiri Pazi alisema kuwa wenye meza hulipa kiasi cha shs 200 kwa siku na wenye vibanda (maduka)hulipa shs21000 kwa mwezi viwango ambavyo wamekuwa wakilipa tangu kuanza kwa soko hilo mwaka 1982.
Mkurugenzi hakuridhika na viwango hivyo kwa ni ni viwango vilivyopitwa na wakati kutokana na hilo ameagiza tozo hizo ziangaliwe upya na walete mapendekezo ya viwango vipya ambapo menejimenti ya Manispaa itavipitia na kulinganisha na mapendekezo ya viwango vya menejimenti na kisha kufanya maamuzi ya viwango vipya.
Akiendelea kutoa taarifa alisema mashine ya kukatia risiti imeharibika hiyvyo kusababisha ushuru kutokusanywa tangu 6/10/2016,baada ya kusikia hayo Mkurugenzi ameagiza apate jumla ya kiasi kilichotakiwa kulipwa na kumtaka kufuatilia pesa hizo na ziingizwe kwenye akaunti mpya ya Manispaa ya Ubungo na kuwasilisha slip ya benki ofisi za Manispaa.
Pamoja na ukaguzi wa soko Mkurugenzi alikagua pia Zahanati ya Mburahati iliyopo katika kata hiyo na kujionea kukamilika kwa ujenzi wa Zahanati hiyo na kutoa maagizo yakufanyika usafi  ili Zahanati hiyo ianze kufanya kazi na kuhudumia wananchi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata Mburahati Mhe Yusufu Yenga amemshukuru Mkurugenzi huyo kwa kuwatembelea na kujionea hali halisi na changamoto zilizopo.
Diwanihuyo alisema kuwa NdgKayombo ni Mkurugenzi wa kwanza kufika hapo kwa ajili ya kujionea hali halisi ya ukusanyaji wa mapato na ziara ya kikazi katika eneo hilo ambapo Ameahidi kumpa ushirikiano na kumuunga mkono katika juhudi zake za kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo za Halmashauri yake.
Mkurugenzi huyo ameahidi kurudi tena katika eneo hilo akiwa na timu ya waandisi wanaosimamia ujenzi wa soko hilo kwa ajili ya ukaguzi zaidi.

No comments:

Post a Comment