Balozi wa Jamhuri ya Korea Nchini Tanzania Bwana Song Geum Young akifafanua jambo wakati akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. |
Serikali ya Jamhuri ya Korea imekusudia kufungua Ubalozi Mdogo Visiwani Zanzibar katika azma yake ya kuimarisha uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya Nchi hiyo na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Jamhuri ya Korea Nchini Tanzania Bwana Song Geum – Young wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Song Geum – Young alisema hatua hiyo kwa kiasi kikubwa itatoa fursa pana zaidi ya ukaribu wa Nchi yake kuzidisha nguvu za kuunga mkono harakati za maendeleo ya Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.
Alisema Korea imekuwa mshirika mkubwa wa Maendeleo wa Zanzibar na hilo linathibitishwa katika miradi kadhaa mikubwa iliyoanzishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kufadhiliwa na Taifa hilo la Bara la Asia.
Balozi Song aliutaja Mradi Mkubwa wa Ujenzi wa Skuli Mpya ya Ghorofa na Kituo cha Habari na Mawasiliano cha Tumaini katika Mtaa wa Kwarara uliomo ndani ya Wilaya ya Magharibi “B ” unaoendelea kujengwa na kutarajiwa kukamilika mapema mwaka ujao.
Alifafanua pia kwamba kikundi cha wajasiri amali wanawake cha Jamuhuri ya Korea kimejitolewa kutoa mafunzo kwa wajasiri amali wa Zanzibar katika mpango maalum wa utengenezaji wa taa za kutumia mwanga wa jua.
Balozi Song alisema Taa hizo ambazo tayari zinatengenezwa na wajasiri amali wa Mkoa wa Dodoma kupitia mpango huo zimeonyesha uwepo wa soko la uhakika litakalowasaidia wajasiri amali hao ambapo Taa moja inafikia thamani ya dola Saba za Kimarekani.
Akigusia miradi mengine ya kiuchumi na Maendeleo Balozi wa Jamuhuri ya Korea alisema jitihada zinaendelea kuchukuliwa na pande hizo mbili katika kuanzisha miradi wa ujenzi wa viwanda vidogo vidogo vya mazao ya Baharini chini ya usimamizi wa Shirika la Kimataifa la Kilimo { FAO }.
Alisema utaratibu maalum utaanzishwa kwa kutolewa mafunzo ya awali kwa washirika wa mpango huo utakaosimamiwa kwa pamoja kati ya wataalamu wa Korea na wale wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Balozi wa Jamuhuri ya Korea Bwana Song alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya Korea na Zanzibar utaendelea kuimarishwa kwa maslahi ya Wananchi wa pande hizo mbili.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimpongeza Balozi Song kwa uamuzi wa Serikali yake ya kutaka kufungua Ubalozi Mdogo Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina pingamizi na uamuzi huo na kumshauri Balozi Song kutayarisha maombi maalum yatakayopelekwa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Kikanda na Kimataifa kwa hatua zaidi za Kidiplomasia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Zanzibar bado iko shwari na ya amani na kumuomba Balozi Song kutumia nafasi yake ya Kidiplomasia kuwashawishi wawekezaji wa Nchi yake kuanzisha miradi ya Kiuchumi Visiwani Zanzibar.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
23/09/2016.
No comments:
Post a Comment