Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Rukwa Arch.
Deocles Alphonce wakati alipokagua ujenzi wa ofisi za Bonde la Ziwa Rukwa na
Maabara zake zilizopo Sumbawanga Mjini.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua nondo
zilizosukwa kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Kalambo lililopo katika barabara ya
Sumbawanga-Matai- Kasanga yenye urefu wa KM 112, Mkoani Rukwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiendelea na
ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Matai- Kasanga yenye urefu wa KM
112, Mkoani Rukwa.
Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Nicholas O’Dwyer Eng. Farley Vicente akitoa taarifa
kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu
ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Matai- Kasanga yenye urefu wa KM 112, Mkoani
Rukwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa Mkandarasi wa China Railway 15 Bureau Group Corporation kutoka
China Zhang Tonggang (mwenye sweta nyekundu) inayojenga barabara ya
Sumbawanga-Matai- Kasanga yenye urefu wa KM 112 kwa kiwango cha lami, Mkoani
Rukwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akihakiki taarifa
za mapato katika Bandari ya Kasanga iliyopo Mkoani Rukwa. Katikati ni Msimamizi wa
bandari hiyo Bw. Seleman Kalugendo.
Meneja wa Shirika la Posta Tanzania Bi. Zahara Sukeiman akifafanua jambo kwa
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu huduma
ya kutuma na kupokea Vifurushi wakati Waziri alipotembelea ofisini hapo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
Maelekezo kwa Meneja wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) nyanda za juu kusini
Bw. Peter Kaguru wakati alipotembelea ofisi hizo Mkoani Rukwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemuagiza
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kupunguza
idadi ya vikao vya baraza visivyo na ulazima ili kuondokana na matumizi mabaya ya
fedha na badala yake fedha hizo zielekezwe kwenye uendelezaji wa miundombinu ya
bandari za maziwa.
Ametoa agizo hilo mara baada ya kukagua shughuli za utendaji wa bandari ya
Kasanga iliyopo mkoani Rukwa inayohudumia mkoa wa Kigoma, nchi ya Burundi na
Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) ambapo amebaini mapungufu ya kiutendaji
ikiwemo malipo yasiyotumia njia za kielektroniki na miundombinu isiyo rafiki katika
kukidhi ushindani wa kibiashara katika bandari hiyo.
Waziri Mbarawa ameitaka TPA kuweka mfumo wa uendeshaji vikao kwa njia ya
kieletroniki (video conference) kwa lengo la kudhibiti matumizi ya fedha nyingi
zilizokuwa zikitumika katika uendeshaji wa vikao hivyo.
“Nataka TPA muanze kutumia video Conference katika vikao vyenu ili fedha zilizokuwa
zikitumika zifanyie kazi nyingine za maendeleo ya Taifa”, amesema Waziri Prof.
Mbarawa.
Ameongeza kuwa TPA imekuwa na wajibu mkubwa wa kuchangia pato la Taifa kupitia
huduma za upakiaji na upakuaji wa mizigo hivyo wanapaswa kuanza kutumia mfumo
wa kielekroniki katika ukusanyaji wa mapato katika bandari zote nchini ili kudhibiti
upotevu wa mapato.
“Tukianzisha mfumo wa kielekroniki katika bandari hii tutakuwa na uwezo wa kufuatilia
mapato yanayopatikana katika utoaji wa huduma na kujua kama malengo yamefikiwa”,
amesema Prof. Mbarawa
Katika Hatua nyingine Profesa Mbarawa amekagua barabara ya Sumbawanga-Matai-
Kasanga Port yenye urefu wa KM 112 inayojengwa kwa kiwango cha Lami na kumtaka
Mkandarasi wa barabara hiyo China Railway 15 Bureau Group Corporation kukamilisha
ujenzi huo ifikapo Julai mwakani.
Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutaunganisha mji wa Sumbawanga na
Bandari ya Kasanga na hivyo kurahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo
kutoka bandarini hapo na hivyo kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi katika Mikoa ya
Nyanda za Juu Kusini.
“Kukamilika kwa barabara hii kutawawezesha wananchi kusafirisha bidhaa zao, kutoka
sehemu moja hadi nyingine na hivyo kukuza uchumi wao na kuongeza pato la Taifa”,
amesisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha Waziri Mbarawa amemuhimiza Mkandarasi huyo kujenga barabara hiyo kwa
viwango vilivyopo katika mkataba na kuzingatia thamani ya fedha katika ujenzi huo ili
kuwezesha barabara hiyo kudumu kwa muda mrefu.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini, Mkoa wa Rukwa Eng. Masuka Mkina
amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa asilimia 62 ambapo
kukamilika kwa ujenzi huo utatagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 133.
“Mpaka sasa Mkandarasi ameweza kukamilisha kujenga makalvati makubwa 11 kati ya
13, na makalvati ya kawaida 169 kati ya 241”, amesema Eng Mkina.
Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua miradi ya miundombinu na
kuangalia utendaji kazi wa taasisi zilizopo katika Mkoa wa Rukwa.
No comments:
Post a Comment