Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kulia) akiwa
katika picha ya pamoja na Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso
Puente, wakati Balozi huyo alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es
Salaam hivi karibuni.
Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso Puente (Kushoto), akisaini
Kitabu cha Wageni ofisini kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo (Kulia), alipomtembelea Waziri na kufanya naye
mazungumzo kuhusu ushirikiano baina ya nchi hizo mbili hususan katika
uwekezaji kwenye sekta ya nishati.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kushoto),
akimsikiliza kwa makini Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso
Puente (Kulia), wakati Balozi huyo alipomtembelea Waziri Ofisini kwake
jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kufanya mazungumzo naye kuhusu
masuala ya uwekezaji katika sekta za nishati na madini. Wengine pichani
ni Maafisa wa Wizara waliohudhuria mkutano huo.
Na Veronica Simba
Serikali ya Brazil imeonesha nia kuwekeza katika sekta ya nishati nchini
hususan katika kuzalisha umeme kwa kutumia maji na mabaki ya miwa.
Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam na Balozi wa Brazil nchini
Tanzania, Carlos Alfonso Puente, alipomtembelea Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake na kufanya mazungumzo
naye.
Balozi Puente alimweleza Profesa Muhongo kuwa nchi yake inao ujuzi na
uzoefu wa kutosha katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo
mbalimbali hususan maji.
Alisema, Brazil ingependa kuchangia kufanikisha azma ya Rais John
Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.
“Kutekeleza mchakato wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda, unahitaji
umeme mwingi unaotokana na vyanzo mbalimbali. Ni bahati nzuri kwamba
Tanzania inazo njia za kufanikisha azma hiyo,” alisema.
Alisema kuwa, nchini Brazil, kuna Kampuni kubwa zenye uzoefu wa muda
mrefu unaofikia miaka 20 hadi 40 katika kazi hiyo, ambazo huzalisha
umeme wa maji nchini mwao na hata nje ya nchi.
Pia, alitaja eneo jingine ambalo nchi yake ina nia ya kuwekeza kuwa ni
uzalishaji wa umeme unaotumia mabaki ya miwa ambayo aliielezea kuwa
chanzo kizuri cha nishati safi.
Balozi Puente alisisitiza kuwa, Brazil ikiwa ni nchi inayozalisha miwa kwa
kiwango kikubwa duniani, itasaidia kuleta mabadiliko katika sekta ya nishati
kwa kuzalisha umeme unaotokana na mabaki ya miwa kwa kutumia
teknolojia za kisasa.
Kwa upande wake, Waziri Muhongo, akimjibu Balozi Puente, alikiri kuwa
kuwa Brazil ina ujuzi, uzoefu na uwezo mkubwa hususan katika maeneo
ambayo Balozi aliyataja na hivyo akamwambia nchi hiyo inakaribishwa
kuwekeza Tanzania kwa kufuata masharti na utaratibu uliowekwa na
Serikali.
Akizungumzia zaidi kuhusu utaratibu wa uwekezaji, Waziri Muhongo
alieleza kwamba Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara yake, inabadilisha
utaratibu wa kupokea wawekezaji katika sekta husika.
Alisema, kunaandaliwa utaratibu maalum utakaokuwa wa wazi na
kuruhusu ushindani kwa wenye nia ya kuwekeza kwa malengo ya
kupunguza au kuondoa kabisa mazingira ya rushwa na muda mrefu
unaotumika katika majadiliano pasipo sababu za msingi.
Profesa Muhongo alifafanua zaidi kwamba, Serikali itaweka mazingira
mazuri zaidi ya ushindani kwa kuandaa maelezo ambayo pamoja na
mambo mengine yatabainisha aina mbalimbali za vyanzo vya umeme
vilivyopo nchini pamoja na maeneo vilipo.
Alisema, Kampuni zenye nia ya kuwekeza zitakaribishwa kupendekeza
viwango vya bei vitakavyotumika kuuza umeme utakaozalishwa na
zitashindanishwa, ambapo washindi wachache watachaguliwa kwa ajili ya
majadiliano kabla ya kuingia mkataba wa uwekezaji husika.
“Kwa hivyo, tunaandaa kabrasha maalum litakalokuwa na maelezo husika
na litakuwa tayari mwezi wa Septemba mwaka huu. Kabrasha hilo lenye
maelezo litatumika kama mwongozo wa ushindanishaji maombi mbalimbali
ya uwekezaji hususan katika kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo
mbalimbali kwa uwazi,” alisisitiza.
Alivitaja vyanzo hivyo kuwa ni pamoja na gesi asilia, makaa ya mawe, maji,
jua, upepo, jotoardhi, mawimbi ya bahari pamoja na nishati mbadala.
Waziri Muhongo alisema kuwa maelezo hayo maalum yatasambazwa kwa
wadau mbalimbali wa sekta husika wakiwemo wale wote wenye nia ya
kuwekeza ikiwa ni pamoja nan chi ya Brazil kupitia Ubalozi wake hapa
nchini.
“Kwa kutumia Kabrasha hilo maalum lenye maelezo husika, wewe Balozi
utaweza kuwashawishi wafanyabiashara kutoka nchini kwako kutoa
mapendekezo ya uwekezaji ambayo yana vigezo vyote muhimu
vinavyoshawishi wapate fursa husika za uwekezaji katika sekta ya nishati,”
Profesa Muhongo alimweleza Balozi Puente.
Kuhusu Mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la kusafirisha mafuta kutoka
Uganda hadi Tanzania, ambao pia Brazil imeonesha nia kuwa ingependa
kuwekeza kwa kushirikiana na Tanzania; Profesa Muhongo alisema
Serikali itaweza kulisemea hilo baada ya kipindi cha miezi takribani 45
kupita, ambapo mambo yote ya kisheria kuhusu Mradi huo yanatarajiwa
kuwa yamekamilika.
Aidha, Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo kuomba nafasi za masomo
nchini Brazil kwa wanafunzi wa kitanzania katika ngazi za Shahada za
Uzamili na Uzamivu katika sekta ya Nishati hususan Mafuta na Gesi, kwa
kuzingatia kuwa Brazil imeendelea sana katika sekta hiyo.
“Ninyi mnazo Taasisi bora kabisa za Utafiti duniani. Mnafanya vizuri sana
katika maeneo mbalimbali.”
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, Brazil ni miongoni mwa nchi Tano (5)
bora duniani zinazozalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu kwa
sababu umeme mwingi wanaozalisha unatokana na maji, kutoka katika
Mito mikubwa waliyonayo.
No comments:
Post a Comment