Saturday, July 2, 2016

CCM ZANZIBAR YAENDELEA KUFANYA UHAKIKI WA MALI ZAKE

Na Is-haka Omar, Zanzibar.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka wananchi wanaoishi katika maeneo yanayomilikiwa na chama hicho kuhakikisha wanafunga mikataba rasmi ili kuepuka usumbufu wakati maeneo hayo yatakapohitajika kwa ajili ya shughuli za kichama.

Kimesema kuna baadhi ya wananchi waliopewa maeneo ya kuishi kwa muda kwa nia ya kuwasaidia na badala yake wameyageuza kuwa makaazi yao ya kudumu jambo ambalo sio sahihi.Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ndg. Vuai Ali Vuai kwa nyakati tofauti katika mwendelezo wa ziara ya kuhakiki mali na maeneo mbali mbali yanayomilikiwa na CCM huko Mbweni Mkoa wa Magharibi Kichama.

Alisema chama kinaendelea na zoezi la kuhakiki mali zake kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wanaotengeneza hati na mikataba bandia ya kujimilikisha mali za chama hicho kinyume na utaratibu.

Ndg. Vuai alifafanua kwamba katika hatua za kupunguza kero hizo chama kimeamua watu wote ambao wamepewa kibinadamu sehemu za kuishi ama kufanya biashara kwa muda katika maeneo yanayomilikiwa na CCM wafunge mikataba rasmi ili chama kiweze kunufaika na rasilimali zake.

“ Watu waliopewa kwa dharura sehemu za kuishi na kufanya biashara kama hatujawapa mikataba rasmi inayotambulikana kisheria, ambayo ni kielelezo cha kumtambulisha nani mmiliki halali wa maeneo hayo baadae inaweza kuwa fursa ya kufanya utapele na kusababisha usumbufu na lawama kwa chama. 

Tujaalie kwamba mtu anaishi katika kiwanja cha Chama bila mkataba wa kisheria na imetokea ameondoka au amehama watoto, ndugu na jamaa zake hawatokubali mali hizo zirudishwe kwa CCM na kitakachotokea hapo ni ugomvi na kupelekana mahakamani hali ambayo chama hakipo tayari kuona inatokea ”,. Alifafanua Vuai na kuongeza kuwa CCM haitokuwa tayari kuona mali zake zinatumiwa na watu wachache bila ya makubaliano ya kimaandishi ama mikataba ya kisheria.

Alisisitiza kuwa Chama hicho kitaendelea kuhakiki, kukagua na kuratibu mali zake zote zilizopo nchini kwa lengo la kuziimarisha na endapo patajitokeza vitendo vya udanganyifu na uvamizi vitatafutiwaufumbuzi wa kudumu na taasisi hiyo.

Alisema bila ya kuwepo na utaratibu maalum na endelevu wa kuhakiki mali za chama hicho baadhi ya watu watakuwa wanajimilikisha na kujinufaisha wenyewe huku chama kikibaki kuwa maskini.Alifahamisha kwamba CCM itaendelea kutekeleza kwa vitendo sera zake zinazoelekeza na kukitaka Chama kutumia rasilimali na vyanzo vyake vya mapato kukuza uchumi wa taasisi hiyo.

Alitoa wito kwa Wana CCM na wananchi kwa ujumla kuunga mkono juhudi za chama hicho za kuhakikisha mali zake zinabaki salama bila ya kuhujumiwa na watu wachache wanaojali maslahi binafsi badala ya Chama na Serikali kwa ujumla.Wakati huo huo Naibu Katibu wa CCM Zanzibar, alitembelea Jumba la kihistoria la Afro-Shiraz Party (ASP) lililopo katika eneo la Kijangwani na kueleza kwamba dhamira ya CCM ni kuhakikisha eneo hilo linaenziwa kwa kujengwa nyumba ya kisasa zinazoendana na hadhi ya Chama.

Alifafanua kwamba Jengo hilo lilianzishwa na Chama cha Shiraz association ambacho baadae mwaka 1957 iliungana na Chama cha African association na kuunda Chama kimoja kilichoitwa Afro Shiraz Party(ASP) , na hatimaye kuungana na TANU na kuzaliwa kwa CCM mwaka 1977.

“ Jengo hili lina historia kubwa ya Chama kwani lilikuwa likitumika na viongozi mbali mbali wa chama kabla na baada ya harakati za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964”, alisema Vuai.Aidha amewataka viongozi wa Mkoa Mjini kuhakikisha wanaadhika historia ya eneo hilo na kuiweka katika kumbukumbu za kudumu za chama ili ziweze kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Naibu Katibu Mkuu huyo, aliwapongeza wafuasi wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kwa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa marudio ulioiweka madarakani CCM, na kuwasihi kufanya kazi za ujenzi wa Taifa kwa bidii huku wakisubiri Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Nao Viongozi wa Mikoa miwili kichama ikiwemo Mkoa wa Magharibi na Mkoa Mjini kwa nyakati tofauti wameipongeza CCM kwa uamuzi wake wa kukagua mali za chama katika maeneo tofauti ya mikoa hiyo, na kuahidi kuendelea kuunga mkono hatua hiyo itakayosaidia Rasilimali za chama kubaki salama.

Katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo ametembelea maeneo mbali mbali yakiwemo Viwanja vya Chama katika eneo la Mbweni, Nyumba ya Chama eneo la Shangani pamoja na Jumba la kihistoria la ASP lililopo Kijangwani Zanzibar, ambapo ziara hiyo itakuwa ni endelevu kwa upande wa Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment