Friday, June 24, 2016

TANZANIA BADO INAHITAJI WATAALAM WALIOBOBEA KATIKA BIASHARA YA KIMATAIFA NA WALE WANAOSIMAMIA MFUMO WA UZALISHAJI , USAMBAZAJI NA UTUNZAJI WA BIDHAA MBALIMBALI.

 Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Prof. Emanuel Mjema wakati akifungua mkutano wa wadau mbalimbali wa kujadili program mpya mbili za masomo katika ngazi ya Shahada ya Uzamili katika Biashara ya Kimataifa  na Ugavi, Usimamizi mfumo wa uzalishaji na usambazaji, zinazotarajiwa kuanza kutolewa na chuo hicho.
Mmoja wa washiriki wa Mkutano huo akichangia wakati wa Mkutano huo.
Wadau mbalimbali wakifuatilia kwa makini majadiliano kuhusu program mpya mbili za masomo katika ngazi ya Shahada ya Uzamili katika Biashara ya Kimataifa  na Ugavi, Usimamizi wa mfumo wa uzalishaji na usambazaji, zinazotarajiwa kuanza kutolewa na CBE.
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Prof. Emanuel Mjema akiwa katika picha ya pamoja  na wadau mbalimbali waliohudhuria katika chuo hicho kujadili program mpya mbili za masomo katika ngazi ya Shahada ya Uzamili katika Biashara ya Kimataifa  na Ugavi, Usimamizi mfumo wa uzalishaji na usambazaji, zinazotarajiwa kuanza kutolewa na chuo hicho.

Na.Aron Msigwa  Dar es salasam.

Tanzania bado inahitaji wataalam waliobobea katika Biashara ya Kimataifa na wale wanaosimamia mfumo wa uzalishaji, usambazaji na utunzaji  wa bidhaa mbalimbali hususan mazao ya chakula ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika uagizaji, utunzaji, usambazaji na kuharibika  kwa mazao inayowakumba wafanyabiashara kabla ya kufikisha bidhaa zao kwa walaji.

 Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Prof. Emanuel Mjema wakati akifungua mkutano wa wadau mbalimbali wa kujadili program mpya mbili za masomo katika ngazi ya Shahada ya Uzamili (Masters)katika Biashara ya Kimataifa  na Ugavi, Usimamizi wa mfumo wa uzalishaji na usambazaji, zinazotarajiwa kuanza kutolewa na chuo hicho.

Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo zinazowakumba wakulima na wafanyabiashara walio wengi hasa wale wa matunda ambao hupoteza karibu asilimia 40 ya mazao yao, lazima hatua madhubuti zichukuliwe kwa kuwajengea uwezo wa kitaalamu vijana wa Kitanzania ambao wataweza kukabiliana na changamoto ya wakulima kupata hasara kwa kuhakikisha mazao yanayotoka kwenye maeneo ya uzalishaji yanafika yakiwa salama.

Leo tuna mkutano wa wadau kwa sababu CBE tuko katika hatua za mwisho za mchakato wa kuanzisha Programu mpya za Shahada za uzamili katika katika masuala ya Ugavi (Procurement and Supply Chain Management) pia Shahada ya Uzamili katika Biashara ya Kimataifa (International Business Management) ili tuweze kutoa mafunzo yatakayowasaidia watanzania’’
Amebainisha kuwa mazao kama matunda mara nyingi yamekuwa yakiharibika katika hatua ya kuvunwa, kusafirishwa na kuhifadhiwa jambo linalowasababishia hasara wakulima pamoja na wasafirishaji kwa kuwa hawana ujuzi na utalaam wa usimamizi wa bidhaa na mazao yao.

Aidha, ameongeza kuwa asilimia 40 ya gharama hizo hutumika katika masuala ya usafirishaji na  ufuatiliaji wa bidhaa husika kuifikisha kwa mlaji na kusisitiza kwamba gharama hizo husababishwa na mfumo mzima unaopaswa kupitiwa kabla ya kuifikisha bidhaa husika sokoni jambo ambalo lingerekebishwa kwa kuwa na wataalam wa kutosha kusimamia sekta hiyo. 
"Tanzania tunahitaji wataalam waliobobea katika eneo hili, tumekuwa na changamoto nyingi, mfano mfanyabiashara  akinunua mahindi kutoka wilaya ya Mpanda au Namanyele anayapata kwa bei ya chini kwa kuwa eneo lile lina wazalishaji wengi,  akiyasafirisha kuyaleta jijini Dar es salaa gharama yake inapanda karibu mara tano gharama hii ni ile inayoletwa na mfumo wa usambazaji wa bidhaa husika" Amesisitiza Prof. Mjema.

Amesema uanzishwaji wa Programu hizo utayaangalia masuala mbalimbali yakiwemo ya ufungaji wa bidhaa husika, maghala ya kuhifadhia bidhaa hizo, suala la usafirishaji na usimamizi wa bidhaa husika yakiwemo mazao ya kilimo kuhakikisha kuwa hayaharibiki kabla ya kuwafikia walaji.

Kuhusu uanzishwaji wa programu ya Biashara ya Kimataifa amesema kuwa kutokana na uchumi wa Tanzania kukua kwa kasi, watanzania wengi sasa wanafanya biashara ya Kimataifa na wengi wao wanakosa weledi katika kufikia matarajio ya biashara zao.

Amesisitiza CBE imeliona eneo hilo kuwa linapaswa kutazamwa na kufanyiwa kazi ili Watanzania wanaofanya Biashara ya kimataifa waweze kupata  mafanikio katika biashara za Kimataifa, kuelewa changamoto za biashara hiyo na vitu vinavyotakiwa kuzingatiwa ili kupata matokeo yaliyokusudiwa. 
"Uchumi wa Tanzania unakuwa kwa kasi,  tunaanzisha programu hizi ili kuwawezesha watanzania kujua kwamba katika biashara za Kimataifa kuna changamoto gani, lazima tuwaandae watanzania kuingia katika uchumi wa dunia wakiwa na utaalam na uelewa wa kutosha kuhusu mikataba ya kimataifa na biashara ya kimataifa ili kukidhi haja ya nchi na mahitaji ya kimataifa" Amesisitiza Prof. Mjema.

Amesema kuwa uanzishwaji wa programu ya Suppy Chain Management unatumia mtaala wa Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) ambao pia  unakubalika na Shirika la Kimataifa la Biashara (WTO)  kwa kuwa unatumika kufundishia duniani kote na kuongeza kuwa mtaala huo wameushusha katika ngazi ya Taifa kwa kuangalia hali halisi ya mazingira na changamoto zinazoikabili 
Tanzania katika masuala ya Ugavi.
"Wahitimu wa fani ya Usimamizi wa Mfumo wa Usambazaji wa bidhaa mbalimbali (Supply Chain Management) watakaopata vyeti vyetu vya kuhitimu wataweza kufanya mtihani wa ITC utakaowawezesha kukidhi viwango vya kimataifa na kuwawezesha wahitimu hao kukubalika duniani kote katika fani hiyo" Amesisitiza Prof. Mjema. 
Naye Mshauri Msimamizi kutoka SCM na Mwakilishi wa Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO) Tanzania, Bw. Pamphill Kiluwa akizungumza wakati wa mkutano huo amesema kuwa uanzishwaji wa program ya Biashara ya Kimataifa na ile inayohusika na Ugavi na Usimamizi wa mfumo wa Uzalishaji, Usambazaji na Utunzaji wa bidhaa kutoka kwa mzalishaji kwenda kwa mlaji unalenga kuzalisha wataalam wenye weledi wa kutosha .
Amesema kuwa uzalishaji wa wataalam hao utaweza kukidhi haja ya wateja kulingana na mahitaji yao ndani na nje ya nchi kwa kukidhi mahitaji yaliyopo katika masuala ya Ununuzi, usafirishaji ,uhifadhi wa bidhaa na vifaa mbalimbali katika ngazi ya Taifa na Kimataifa.

Naye Mkurugenzi wa Elimu ya Juu wa chuo hicho  Dkt. Michael Haule akizungumzia programu  hizo amesema kuwa zitakuwa mkombozi kwa Watanzania huku akisisitiza kuwa kumekuwa na mapungufu katika masuala ya Ugavi na Manunuzi hasa upande wa kununua,kupakia na kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka eneo la uzalishaji hadi kumfikia mlaji wa mwisho na kusisitiza kuwa uanzishwaji wa programu hizo.

Amesema Shahada ya Biashara ya Kimataifa itawaezesha wahitimu kufanya kazi katika mashirikia na taasisi za kimataifa za ndani na nje ya nchi na kueleza kuwa  ufundishaji wa kozi hizo utachukua miezi 18. 
Dkt. Haule amebainisha  kuwa ufundishaji wa kozi hizo chuoni hapo utatumia mbinu na Teknolojia  ya kisasa kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa njia ya mtandao huku akibainisha kuwa chuo hicho sasa kiko katika hatua za mwisho za majadiliano yanayohusisha wadau mbalimbali kupata ushauri wa kitaalam ili kiweze kuufanyia kazi kuboresha mitaala hiyo kabla ya kuwasilisha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa ajili ya usajili ili ianze kutumika ikiwa ni hatua ya mwisho.

Aidha, amesema kuwa katika kufanikisha hatua mbalimbali za mchakato wa kuanzishwa kwa program hizo mpya, wataalam wa CBE walitembelea mikoa 17 wakihoji waajiri, wanafunzi , wananchi na wadau mbalimbali maeneo ya uzalishaji ili kupata uhakika wa mahitaji halisi ya soko la kozi hizo nchini Tanzania.



No comments:

Post a Comment