Wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini ambalo linaundwa na wawakilishi wawili kutoka kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu wamekutana mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa GEPF uliopo Victoria Jijini Dar es salam kujadili mapendekezo ya mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ndani na baina ya vyama vya siasa .
Mapendekezo hayo yalitolewa na Mtaalamu wa utatuzi wa Migogoro Bw. Ghalib Galant ambaye awali alifanya utafiti wa utatuzi wa migogoro ya ndani na baina ya vyama vya siasa nchini chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na kwa udhamini wa UNDP kupitia mradi wake wa “Democratic Project” ukiwa na lengo la kuiboresha sura namba 258 ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 ili kuendana na mahitaji ya ukuaji wa demokrasia nchini. Utafiti huo ulishirikisha wadau mbalimbali wa demokrasia ya vyama vingi nchini vikiwemo vyama vya siasa.
Akiwasilisha mapendekezo, Msajili Msaidizi Bi. Piencia C. Kiure ,alisema kuwa ilipendekezwa kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa nchini iweke masharti yanayohusu utaratibu wa kutatua migogoro ndani na baina ya vyama vya siasa “ migogoro ndani ya chama ni lazima ishughulikiwe kwanza ndani ya chama cha siasa na kufikia tamati kwa mfumo wa utatuzi wa migogoro uliowekwa kwa mujibu wa katiba ya chama, kabla ya kuwasilishwa katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa ajili ya upatanishi” ilikaririwa sehemu ya mapendekezo
“Upatanishi ukishindikana mgogoro husika uwasilishwe kwenye Baraza la Uamuzi la Migogoro ya Vyama vya Siasa kwa uamuzi. Ikiwa muhusika wa mgogoro asiporidhika na uamuzi wa Baraza la Uamuzi wa migogoro ya vyama vya siasa atawasilisha mgogoro husika Mahakama Kuu mbele ya Majaji watatu kwa mapitio ya uamuzi wa Baraza. Muhusika asiporidhika na uamuzi wa Mahakama Kuu, atakata rufaa Mahakama ya Rufaa” ilifafanua sehemu ya Mapendekezo.
Aidha kumekuwa na msisitizo wa kufuata mtiririko wa hatua katika utatuzi wa migogoro kama ilivyobainishwa hapo juu ili kuepusha migogoro ndani ya vyama kwenda moja kwa moja Mahakamani ambako huchukua muda mrefu na kuathiri ukuaji wa demockaria ndani na nje ya vyama vya siasa hapa nchini.
Wakichangia katika mjadala huo, baadhi ya wajumbe walikubaliana na hoja kuwa vyama vya siasa vitatue kwanza migogoro yake ndani ya vyama na kwamba pale tu itakaposhindikana ndipo ipelekwe kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Wajumbe walishindwa kukubaliana katika hoja ya uwepo wa Baraza la Uamuzi wa Migogoro ya vyama vya siasa, wapo walioona haja ya uwepo wake na wapo walipendekeza kuwa majukumu ya Baraza hilo yafanywe na Baraza la Vyama vya siasa lililopo sasa jambo lililosababisha kutokukubaliana katika hoja hiyo.
Pamoja na michango iliyotolewa , Wajumbe wameishauri Serikali kuona umuhimu wa kuwekeza katika Baraza la Vyama vya Siasa ili kusaidia utatuzi wa migogoro nchini kwa kuwa imebainika kuwa machafuko katika nchi nyingi duniani yamesababishwa na machafuko katika masuala ya siasa.
Akihitaji ufafanuzi wa hatua gani imefikiwa katika uboreshaji wa Sheria ya Vyama vya siasa, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama Vya Siasa, Mhe. Peter Kugar Mziray aliiomba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa ufafanuzi.
Naye Msajili Msaidizi, Bw. Sisty Nyahoza akitoa ufafanuzi alisema tayari vyama vyote vya siasa vimeshapelekewa barua vikiombwa kuwasilisha mapendekezo kwa ajili ya kuboresha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 na kwamba Ofisi inafanya jitihada za kupokea mapendekezo kutoka kwa wadau wa siasa na ikishakamilisha upokeaji huo, mapendekezo hayo yatawasilishwa kwenye kamati ya Katiba na Sheria.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini Mhe. Peter Kuga Mziray akifafanua jambo wakati wa kikao cha Baraza kujadili Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa migogoro ndani na baina ya vyama vya siasa kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam . Kulia ni Mhe. Jaji Francis S.K Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa na Mhe. Vuai Ali Vuai, Makamu Mwenyekiti wa Baraza.
Msajili Msaidizi (Elimu kwa umma na Gharama za uchaguzi) Bi. Piencia C. Kiure akiwasilisha mada ya Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa migogoro ndani na baina ya vyama vya siasa katika baraza la Vyama vya Siasa lilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam.
baadhi ya wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa wakifuatilia mjadala wakati wa kikao cha Baraza kujadili Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa migogoro ndani na baina ya vyama vya siasa kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam.
Bw. John Cheyo mmoja wa wajumbe wa Baraza la vyama vya siasa akichangia hoja wakati wa kikao cha Baraza kujadili Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa migogoro ndani na baina ya vyama vya siasa kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam.
Picha ya Pamoja ya Wajumbe wa Baraza la vyama vya Siasa baada ya kikao cha Baraza kujadili Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa migogoro ndani na baina ya vyama vya siasa kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment