Friday, May 27, 2016

TASAF KUWANUSURU WAHADZABE


Mfuko wa Maendeleo ya jamii –TASAF-umeanza mkakati maalumu utakaowezesha jamii ya Wahadzabe walioko katika mikoa ya Arusha,Manyara na Singida kuandikishwa katika Mpango wa Kunusuru Kaya maskini unaotekelezwa na mfuko huo nchini kote.

Wakizungumza wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini unavyotekelezwa katika wilaya ya Karatu mkoani Arusha,viongozi wa TASAF walioambatana na wadau wa maendeleo walioongozwa na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchi za Tanzania Bi.Bella Bird,na baadhi ya maafisa wa benki hiyo kutoka Marekani ,baadhi ya wahadzabe waliomba kuorodheshwa katika Mpango huo ili waweze kunufaika na huduma zitolewazo kupitia utaratibu wa kuhawilisha fedha.

“ baadhi ya wananchi wenzetu wameandikishwa kwenye mpango huku wengi wetu hatujapata fursa hiyo na tumeanza kuona namna wanavyonufaika na huduma za mpango huo’’ alisisitiza mmoja wa wahadzabe katika kijiji cha Endamaghan umbali wa kilometa 70 kutoka makao makuu ya wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Akizungumza baada ya kutembelea makazi ya wahadzabe Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird amepongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- kwa kuweza kuwafikia wananchi ambao wanakabiliwa na umaskini nchini kote.

‘’Benki ya Dunia inatambua na kuunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania katika kukabili tatizo la umaskini miongoni mwa wananchi wake,umuhimu mkubwa pia unapaswa kuwekwa katika kunusuru jamii za watu walioko katika mazingira magumu wakiwemo wahadzabe” alisisitiza Bi. Bird.

Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF-Bwana Ladsilaus Mwamanga alisema zoezi la kutambua na kuziandikisha kaya maskini katika jamii ya Wahadzabe lilifanyika. Hata hivyo alisema zoezi hilo liliathiriwa kwa kiwango kikubwa na mfumo wa maisha ya jamii hiyo wa kuhamahama kutafuta chakula kwa kuwinda wanyama na kuokota matunda na asali.

“Hatukuweza kuwaandikisha wote ingawa kimsingi wanastahili kuingizwa kwenye Mpango,hii ilitokana na kuhamahama kwa wananchi hao kujitafutia chakula hususani matunda, asali na mizizi” alisisitiza Bwana mwamanga.

Hata Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF ameahidi kuwa kazi ya kuziandikisha kaya za walengwa katika jamii hiyo ya wahadzabe na nyingine zenye maisha ya kuhamahama itafanyika upya na kwa haraka ili waweze kuziingiza kwenye Mpango wa Kunusuru na Kaya Maskini unaotia mkazo katika kuboresha maisha ya walengwa hususani kupitia sekta za elimu, afya,lishe na kukuza kipato kwa kaya za walengwa.

Zifuatazo ni picha za ziara ya viongozi wa TASAF na Wadau wa Maendeleo katika maeneo ya wahadzabe,wilayani Karatu Mkoani Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga (aliyevaa Kaunda suti) akiwasikiliza baadhi ya wananwake wa jamii ya Wahadzabe katika kijiji cha Endaghan wilayani Karatu mkoani Arusha wakati wa ziara ya wadau wa maendeleo na TASAF kuona utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini .
Baadhi ya Wananchi kutoka jamii ya Wahadzabe wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird ( hayupo pichani) alipotembelea kijiji cha Endamaghan kuona utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia TASAF.
Mmoja wa wananchi kutoka jamii ya Wahadzabe akieleza jambo kwa viongozi wa TASAF na Benki ya Dunia waliotembelea kijiji cha Endamaghan wilayani Karatu mkoani Arusha kukagua utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya maskini. Wananchi hao wameomba kuingizwa kwenye Mpango huo ambao umeorodhesha baadhi yao kutokana na tabia yao ya kuhamahama na hivyo kuwa vigumu kuwapata.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya dunia Bi. Bella Bird (watatu kushoto waliochuchumaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Endamaghan ambao ni wahadzabe ambao wameomba kuingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya .

Wananchi jamii ya Wahadzabe wakiwa mbele ya nyumba yao katika eneo la Endamaghan wilaya ya Karatu mkoani Arusha. TASAF inakusudia kuiorodhesha jamii hiyo katika mpango wa kunusuru kaya maskini.

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird akiwahutubia wakazi wa Endamaghan katika wilaya ya Karatu mkoani Arusha juu ya utekelezaji wa Mpango 
Mmoja wa Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Endamaghan kutoka jamii ya Wahadzabe akipokea fedha za ruzuku kupitia mpango huo.
Mmoja wa wananchi jamii ya Wahadzabe katika kijiji cha Endamaghan katika wilaya ya Karatu mkoani Arusha (aliyevaa bangili) akipokea fedha za ruzuku kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na TASAF.
Baadhi ya walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini katika kijiji cha Endamaghan wakiwemo jamii ya Wahadzabe wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird (hayupo pichani) juu ya utekelezaji wa Mpango huo.

No comments:

Post a Comment