Wednesday, May 4, 2016

Serikali yaeleza Mikakati yake katika kuhakikisha Usawa wa Kijinsia Katika Elimu nchini

Wahitimu wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari WAMA- Nakayama wakionyesha maonyesho ya masomo kwa Mgeni Rasmi, Mhe. Ummy Mwalimu, Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete pamoja na wageni waalikwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama, Dr. Ramadhani Dau, akitoa neno la ukaribisho kwa wageni waalikwa katika Sherehe za mahafali ya Kidato cha sita shule ya sekondari WAMA Nakayama
Kaimu Balozi wa Japan hapa nchini Bw. Hiroyuki KUBOTA akisoma hotuba yake wakati wa Sherehe za Mahafali.
Mke wa Rais Mstaafu na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete akisoma hotuba yake kwa wageni waalikwa na wahitimu wakati wa Sherehe za Mahafali ya kwanza ya Kidato cha Sita ya Shule ya WAMA- Nakayama.
Wahitimu wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari ya WAMA - Nakayama katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa WAMA mara baada ya kumkabidhi Cheti cha Shukrani kwa mchango wake katika maendeleo ya elimu yao.
Mgeni Rasmi Mhe. Ummy Mwalimu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto akihutubia wahitimu, walimu na wageni waalikwa wakati wa sherehe za mahafali.

Na Philomena Marijani, WAMA Foundation

Serikali imechukua hatua maalum za kisera na kimipango kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia katika elimu, mafunzo, sayansi na teknolojia. Maelezo hayo yametolewa na Mhe.Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati wa sherehe za Mahafali ya kwanza ya Kidato cha Sita ya Shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama yaliyofanyika mwishoni wa wiki katika ofisi za WAMA zilizopo Kawe, Dar es Salaam.

Mhe.Ummy Mwalimu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo amesema moja ya hatua hizo ni pamoja na kuongeza idadi ya wasichana wanaopata elimu ya msingi ili kuwepo na idadi sawa ya wavulana na wasichana.

Aliongeza kuwa kwa mwaka 2008 serikali ilifanyia marekebisho Sheria ya Elimu na mafunzo ili kukidhi matakwa ya usawa wa kijinsia. “Baadhi ya maswala ambayo yamerekebishwa ili kuboresha mazingira ya shule yaweze kuwa rafiki kwa wasichana ni pamoja na kuhamasisha jamii kutoa chakula shuleni, kujenga mabweni na vyoo kwa ajili ya wasichana na pia kuongeza idadi ya walimu.

Wizara yangu pia imeandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 na Sheria ya Mtoto No.21 ya mwaka 2009 ambayo inasisitiza jamii kuzingatia utoaji wa haki za msingi kwa watoto, moja ya haki hizo ni haki ya kuendelezwa.” Alisema Mhe. Ummy Mwalimu.

Mhe. Mwalimu aliwashauri wahitimu wa WAMA-Nakayama wasiridhike na elimu ya kidato cha sita bali wajiendeleze kwa kujiunga na vyuo mbalimbali hapa nchini na hatimaye serikali ipate viongozi wengi wanawake.

Akiongea katika sherehe za mahafali hayo Mke wa Rais Mstaafu na Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete alisema Shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama ilianzishwa ili kutoa mchango katika Juhudi za Taifa za kumkomboa mwanamke kwa kuwapatia fursa za elimu bora ya sekondari watoto wa kike wanaotoka katika mazingira magumu wakiwemo yatima.

“Taasisi inatambua kwamba ili mtoto wa kike aweze kupata mafanikio katika masomo yake ni muhimu kumjengea mazingira wezeshi ya kusomea na kuishi. Ndiyo maana tuliamua kuwajengea shule yenye mahitaji yote ya kupata elimu bora na pia kuepuka vishawishi mbalimbali vinavyoweza kupelekea kukatisha masomo. Alisema Mama Kikwete.

Mama Kikwete aliwashukuru wadau wote ambao wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali tangu kuanzishwa kwa shule ya WAMA- Nakayama na kusema ushirikiano huo umesaidia kufanikisha ndoto ya kuwasaidia watoto wa kike na matunda yake yanaonekana kwa wanafunzi wanaohitimu kidato cha sita.

Akisoma hotuba yake Kaimu wa Balozi wa Japan hapa nchini,Bw. Hiroyuki KUBOTA alisema shule hii iliweza kuanzishwa kwa msaada kutoka kwa Bw. Nakayama wa Japan ambaye alichangia hela za ujenzi wa shule. Aliongeza kuwa Ubalozi wa Japan hapa nchini umekuwa ukisaidia shule katika masuala mbalimbali ikiwemo maboresho ya sick- bay, maabara, na kwa sasa ubalozi unasaidia upanuzi wa jengo la utawala ambao utamalizika baada ya muda mfupi.

Shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama iliyopo Nyamisati, Rufiji katika Mkoa wa Pwani ilianza rasmi mwaka 2010. Shule inasaidia wasichana yatima na waliotoka katika mazingira hatarishi kutoka mikoa yote Tanzania bara na visiwani.

Jumla ya wanafunzi wa kike 27 watamaliza kidato cha sita mwezi mei mwaka huu katika michepuo ya ECA na PCB.

No comments:

Post a Comment