Thursday, May 5, 2016

Bodi ya wataalamu wa Ununuzi na Ugavi yang’ara kimataifa

Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB Bw. Clemence Tesha akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) juu ya tuzo ya kimataifa ya viwango iliyotolewa na International Federation of Purchasing and Supply Manangement(IFPSM) kwa bodi hiyo hivi karibuni kulia ni mkurugenzi wa mafunzo Bw. Godfrey Mbanyi.
Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB Bw. Clemence Tesha akionesha kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) vitabu vya mtaala mpya wa mafunzo ulioanza na Bodi ya wataalamu ya manunuzi na Ugavi (PSPTB)Desemba mwaka 2015 kulia ni mkurugenzi wa mafunzo Bw. Godfrey Mbanyi.
Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB Bw. Clemence Tesha akionesha kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) tuzo ya viwango vya kimataifa kutoka International Federation of Purchasing and Supply Manangement(IFPSM) iliyotolewa kwa kwa bodi hiyo hivi karibuni kulia ni mkurugenzi wa mafunzo Bw. Godfrey Mbanyi.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifatilia mkutano wa Bodi ya wataalamu wa manunuzi na ugavi uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Hassan Silayo MAELEZO).

Na Raymond Mushumbusi, MAELEZO

Bodi ya wataalam wa manunuzi na ugavi (PSPTB) imetunukiwa tuzo ya viwango vya kitaalamu vya kimataifa na International Federation of Purchasing and Supply Manangement(IFPSM) na kutambulika rasmi kimataifa kwa kuwa na vigezo vya utoaji huduma katika viwango vya kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dare s Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB Bw. Clemence Tesha amesema tuzo hiyo imetolewa kwa PSPTB mwezi Februari mwaka 2016 na kuifanya PSPTB kuwa bodi ya kwanza barani Afrika kupata tuzo hiyo ya viwango vya kimataifa kutoka IFPSM.

“Upatikanaji wa tuzo hiyo ni matunda ya ushirikiano kati ya watendaji na mimi mwenyewe kama Mkurugenzi Mtendaji wa bodi katika kuiendesha bodi hiyo kufanikisha malengo na mipango yake katika utendaji kazi.

Bw Tesha ameeleza kuwa mara baada ya PSPTB kupata tuzo hiyo wamepata pongezi kutoka Rais wa IFPSM Dkt Paul Davi kwa niaba ya Bodi ya wataalamu wa viwango vya kimataifa kwa kazi kubwa walioifanya na kuwa taasisi ya kwanza Barani Afrika kufikia kiwango cha kutambulika kimataifa kwenye taaluma hiyo.

Kabla ya kupata tuzo hiyo, PSPTB ilikuwa mwanachama muhusishwa wa IFPSM tangu mwaka 2015 lakini kutokana na utendaji wa kazi wake, Bodi ya viwango ya kimataifa ikawatunuku tuzo ya kuwa na viwango vya kimataifa katika utoaji wa taaluma hiyo Barani Afrika kwa ujumla.

Aidha , PSPTB imezindua mtaala mpya wa mafunzo tangu Desemba mwaka 2015 na mtaala huo kwa sasa unaendelea kufundishwa katika vituo mbalimbali vya maandalizi ya mitihani ya Bodi ambapo mtihani wa kwanza chini ya mtaala mpya utafanyika November 2016.

Umuhimu wa mtaala huo ni pamoja na utaratibu wa kuanzisha masomo ya usimamizi wa manunuzi wa umma kuanzia ngazi za chini hadi juu na pia utaratibu huu utawataka watahiniwa kufaulu ngazi yoyote ya mtihani ndani ya miezi 24 toka kufanyika kwa mtihani husika kwa mara ya kwanza.

Katika kuzingatia utoaji wa taaluma ya manunuzi na ugavi nchini Bodi ya wataalamu wa manunuzi na ugavi itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kusaidiana na kupambana na changamoto zilizopo katika kupeleka mbele gurudumu la taaluma hiyo.

No comments:

Post a Comment