Thursday, April 28, 2016

Mnada wa Madini waiingizia Serikali Bilioni 1.6

Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Kaskazini, Elias Kayandabila akisisitiza jambo kabla ya ufunguzi wa masanduku yenye bahasha za ahadi ya bei za madini yaliyopigwa mnada katika Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 19 hadi 21, Aprili, 2016. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Zena Kongoi na kushoto ni mmoja wa Wakurugenzi wa Kampuni ya Sky Associates Faisal Juma Shahbhai inayomiliki mgodi wa Tanzanite One kwa ubia na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji Madini ya Almas na Vito, katika Wizara ya Nishati na Madini, Archard Kalugendo akiangalia maombi ya ahadi za bei ya madini yaliyopigwa mnada katika Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 19 hadi 21, Aprili, 2016. Wanaoshuhudia ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Uchumi na Biashara, Salim Salim (Wa Pili kushoto), Wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Uthamini wa Madini na Huduma za Kimaabara katika Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Mhandisi Gilay Shamika na wa kwanza kulia ni Mthamini Almas wa Serikali, Edward Rweyemamu.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji Madini ya Almas na Vito, katika Wizara ya Nishati na Madini, Archard Kalugendo akionesha masanduku yenye bahasha za ahadi ya bei za madini yaliyopigwa mnada katika Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 19 hadi 21, Aprili, 2016. Wanaoshuhudia ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Uchumi na Biashara, Salim Salim (katikati) na kulia ni Mkurugenzi wa Uthamini wa Madini na Huduma za Kimaabara katika Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Mhandisi Gilay Shamika.
Wadau mbalimbali walioshiriki Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 19 hadi 21 wakimsikiliza Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji Madini ya Almas na Vito, katika Wizara ya Nishati na Madini, Archard Kalugendo (hayupo pichani) wakati akitangaza matokeo ya mnada wa madini uliofanyika katika Maonesho hayo.
Wadau mbalimbali wakishuhudia, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji Madini ya Almas na Vito, katika Wizara ya Nishati na Madini, Archard Kalugendo akifungua masanduku yenye bahasha za ahadi ya bei za madini yaliyopigwa mnada katika Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 19 hadi 21, Aprili, 2016.

Na Teresia Mhagama na Asteria Muhozya, Arusha

Serikali imepata jumla ya shilingi bilioni 1.6 ikiwa ni mapato yaliyopatikana katika mnada wa madini uliofanyika wakati wa Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha katika Hoteli ya Mt.Meru kuanzia tarehe 19 hadi 21, Aprili mwaka huu.

Hayo yameelezwa hivi karibuni jijini Arusha na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji Madini ya Almasi na Vito (TANSORT) katika Wizara ya Nishati na Madini, Archard Kalugendo, wakati akitangaza matokeo ya mnada huo.

Katika maonesho hayo, kulikuwa na Tenda Tatu; Tenda ya Kwanza ilikuwa ya Serikali ikihusisha madini mbalimbali yaliyokuwa yakishikiliwa na Kamishna wa Madini ambapo jumla ya shilingi za kitanzania bilioni 1.3 zilipatikana kutokana na mauzo ya madini hayo.

Tenda ya pili ilikuwa ni madini ya Tanzanite ghafi yaliyozalishwa na mgodi wa TanzaniteOne unaomilikiwa kwa ubia kati ya kampuni ya Sky Associates na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

“Napenda kushukuru mgodi wa TanzaniteOne kwani wametuletea madini ya Tanzanite ambayo ni ghafi yenye thamani kubwa ambapo madini yote kutoka mgodi huu yamenunuliwa kwa thamani ya shilingi za Kitanzania Bilioni Tano (5),” alisema Kalugendo.

Kalugendo alisema kuwa tenda ya tatu ya mnada huo ilikuwa ya kampuni ya El-Hilal inayochimba madini ya Almas nchini. Alifafanua kuwa, kampuni mbili zilizojitokeza katika tenda hiyo hazikufikia kiwango cha chini cha bei iliyowekwa na Serikali hivyo kupelekea madini hayo kutokuuzwa katika mnada huo.

“ Hii ni kusema kwamba madini yote ya Tanzanite yaliyoletwa na mgodi wa TanzaniteOne na Tanzanite iliyoletwa na Serikali katika kifurushi cha kwanza pamoja na dhahabu yote iliyokuwa katika kifurushi hicho yameuzwa,” alisema Kalugendo.

Aliongeza kuwa, fedha yote iliyopatikana kutokana na mauzo ya madini yaliyokuwa yakishikiliwa na Kamishna wa Madini, inaingizwa katika mfuko wa Serikali na kwamba madini ghafi yaliyouzwa kutoka TanzaniteOne yatalipiwa mrabaha serikalini wa shilingi milioni 245,686,000 ili madini hayo yaweze kusafirishwa popote.

Aidha, Kalugendo alisisitiza kuwa mapato hayo ni ya mnada tu hivyo mauzo ya jumla ya maonesho hayo yatatangazwa baada ya kujumuisha matokeo ya mauzo yote yaliyofanyika katika Maonesho husika.

Pia, Mkurugenzi wa Uthamini wa Madini na Huduma za Kimaabara kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Mhandisi Gilay Shamika, akiwa katika Mnada wa Madini yaliyo chini ya Kamishna wa Madini, alitoa wito kwa wafanyabiashara kufuata sheria, taratibu na kanuni za biashara ya Madini ili kutotaifishiwa Madini yao mara wanapokamatwa bila kuwa na vibali husika.

‘Madini haya unayoyaona yakipigwa mnada, yalikamatwa na kutaifishwa pindi yakitoroshwa nje ya nchi bila wahusika kuwa na vibali vya usafirishaji. Ni vema wafanyabiashara kufuata taratibu kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010,’’ Alisema Shamika.

Naye kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia Uchumi na Biashara, Salim Salim aliwashukuru wadau wote walioshiriki na kudhamini maonesho hayo ambayo ni muhimu katika uendelezaji wa Sekta ya Madini nchini.

No comments:

Post a Comment