Thursday, March 24, 2016

TRL KUSAFIRISHA SARUJI YA TANGA KWA NJIA YA RELI

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Martine Shigela akitoa taarifa ya hali ya miundombinu katika mkoa wa Tanga kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ofisini kwake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji cha Tanga (Simba Cement), Bw. Reinhart Swart (wa pili kulia) akimwonesha moja ya nyaraka Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) Bw. Masanja Kadogosa (wa pili kushoto) kabla ya kusaini makubaliano ya kusafirisha saruji ya kiwanda hicho kwa njia ya reli kutoka Tanga kwenda mikoa ya Kigoma na Mwanza.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa tatu kushoto) akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji cha Tanga (Simba Cement), Bw. Reinhart Swart (wa tatu kulia) pembeni ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) Bw. Masanja Kadogosa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) Bw. Masanja Kadogosa (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji cha Tanga (Simba Cement), Bw. Reinhart Swart (kushoto) wakisaini makubaliano ya kusafirisha saruji ya kiwanda hicho kwa njia ya reli kutoka Tanga kwenda mikoa ya Kigoma na Mwanza. Huku Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakishuhudia.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) Bw. Masanja Kadogosa (kulia) kabla ya kusaini makubaliano ya kusafirisha saruji ya kiwanda hicho kwa njia ya reli kutoka Tanga kwenda mikoa ya Kigoma na Mwanza. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji cha Tanga (Simba Cement), Bw. Reinhart Swart.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifafanua jambo baada ya kusaini makubaliano ya kusafirisha saruji ya kiwanda hicho kwa njia ya reli kutoka Tanga kwenda mikoa ya Kigoma na Mwanza. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji cha Tanga (Simba Cement), Bw. Reinhart Swart na (Kushoto) ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Martine Shigela.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akisaidiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji cha Tanga (Simba Cement), Bw. Reinhart Swart (wa pili kulia) wakipakia mfuko wa saruji kwenye kontena kabla ya kuanza kusafirishwa kwa njia ya reli kutoka katika kiwanda cha Simba Cement kwenda mikoa ya Kigoma na Mwanza.

Kiwanda cha Saruji Tanga (Simba Cement), kimeingia makubaliano na Shirika la Reli Tanzania (TRL), kusafirisha shehena ya saruji kwa njia ya reli kutoka mkoani Tanga kwenda mikoa ya Mwanza na Kigoma.

Chini ya Makubaliano hayo zaidi ya tani laki nne na nusu zitasafirishwa kwa mwaka na hivyo kupunguza gharama ya bei ya Saruji katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi kutokana na usafirishaji wa reli kuwa wa bei nafuu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema katika mkataba huo TRL litapata zaidi ya shilingi Bilioni 40 na hivyo kufufua huduma ya usafirishaji wa mizigo katika reli ya kati na kuongeza mapato kwa nchi.

Prof. Mbarawa amewataka wafanyabiashara nchini kuanza kutumia reli kusafirisha bidhaa zao, kwani usafiri huo ni salama na nafuu na unachukua shehena kubwa kwa wakati mmoja.

“Asilimia 95 ya mizigo hapa nchini inasafirishwa kwa barabara hivyo mkakati wa Serikali wa kufufua viwanda utafanikiwa kwa haraka endapo wasafirishaji watatumia njia ya reli “, amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, amefafanua kuwa usafirishaji wa reli ukiimarika utapunguza ajali za barabarani zinazosababishwa na malori na kupunguza kasi ya uharibifu wa barabara unaotokea sasa kutokana na maroli kuzidisha uzito.

Prof. Mbarawa amewataka watumishi wa TRL na wananchi kulinda miundombinu ya reli na kutumia fursa ya usafiri huo kujiongezea mapato.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Martine Shigela amesema usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli utatoa fursa za ajira na kuwezesha bandari ya Tanga kupata shehena kubwa ya mizigo na hivyo kurudisha hadhi ya Mkoa wa Tanga.

“Tanga tuna reli, barabara na bandari hivyo tukio la kuanza kusafirisha mizigo kwa njia ya reli itaongeza shehena kubwa katika bandari ,itatengeneza ajira kwa wakazi wa Tanga na kukuza uchumi wa mkoa”, amesema Bw. Shigela.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli (TRL) Bw. Masanja Kadogosa amesema kusainiwa kwa mkataba huo kutawezesha TRL kusafirisha tani elfu thelathini na tano za Saruji kati ya tani laki moja na elfu tano zinazozalishwa na kiwanda hicho.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji Tanga Bw. Reinhart Swart, amesema usafirishaji wa Saruji kwa njia ya reli utaongeza kasi ya usafirishaji wa saruji na kuwezesha kuwafikia watumiaji kwa bei nafuu.

Kiwanda cha Saruji Tanga kinakuwa kiwanda cha kwanza kuingia mkataba na TRL kusafirisha shehena ya mizigo tangu Serikali kuanza mikakati yake ya kufufua reli na kupunguza usafirishaji wa shehena kubwa kwa njia ya barabara na hivyo kuzuia uharibifu wa barabara na kupunguza ajali.

No comments:

Post a Comment