Sunday, February 7, 2016

WAZIRI MBARAWA AWATAKA MAKANDARASI KURUDI KAZINI

Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawsiliaano Prof.Makame Mbarawa (Wa pili kushoto), akitoa maelekezo kwa Meneja bishara wa kampuni ya Malaysia inayojenga vichwa vya treni Srinivasan Rajmohan (Wa kwanza kulia) kuhusu kufanya kazi hiyo kwa haraka ( Wa pili kushoto) ni katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi Eng.Leonard Chamuriho na (Wapili kulia) ni Naibu Waziri Eng.Edwin Ngonyani.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewataka Makandarasi waliosimamisha kazi za ujenzi wa barabara nchini kuendelea na ujenzi baada ya Serikali kuanza kuwalipa madai yao.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Magole-Turiani yenye urefu wa kilomita 48.6 Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, Prof. Mbarawa amesema tayari Serikali imeshalipa makandarasi mbalimbali nchini shilingi bilioni 400 na itaendelea kufanya hivyo ili kumaliza madeni yao kwa haraka.

“Hakikisheni mnarejea kazini na kuwapa mikataba ya ajira wafanyakazi wenu katika kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa ili ujenzi wa barabara na madaraja ukamilike kwa mujibu wa mkataba na hivyo kuondoa usumbufu kwa watumiaji wa barabara hii”, amesema Prof Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kulia) akimsikiliza Mbunge wa Mvomero Sadick Murad (kushoto) wakati akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa barabara ya Magole-Turiani yenye urefu wa Km 48.6. Katikati ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Eng. Edwin Ngonyani.

Profesa Mbarawa amemhakikishia mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation anayejenga barabara ya Magole-Turiani kuwa tayari serikali imeshamlipa zaidi ya kiasi cha dola za kimarekani zaidi ya laki 735 na Shilingi za kitanzania zaidi ya Milioni 795 hivyo ni wakati wa kukamilisha ujenzi huo hususan sehemu za madaraja kabla ya mvua za masika kuaanza.

Akizungumza katika ukaguzi huo Mbunge wa Mvomero Mhe. Sadick Murad ameiomba Serikali kumalizia daraja la Diwale lenye urefu wa mita 75 ili liweze kupitika.

Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua karakana ya ujenzi wa vichwa vya treni mjini Morogoro na kumtaka mkandarasi anayekarabati vichwa hivyo kufanya kazi hiyo kwa haraka na kutoa kazi nyingine kwa watanzania ili kuwajengea uwezo wa kazi hizo.
Sehemu ya juu ya daraja la Diwale lenye urefu wa mita 75 likiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake kama linavyoonekana.

Amewataka wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) Kufanya kazi kwa ubunifu, uadilifu na uwazi ili kufufua hadhi ya Shirika hilo ambalo ni muhimu kwa uchumi wa nchi hii.

Amesema takribani asilimia 96 ya mizigo inayoshushwa katika Bandari ya Dar es salaam husafirishwa kwa njia ya barabara hivyo ni jukumu la TRL kuhakikisha inapata mizigo ya kutosha ya kusafirisha ili kupunguza mizigo hiyo kusafirishwa na barabara lakini kufufua uchumi wa TRL na taifa kwa ujumla.

“Fanyeni kazi kwa bidii, uwazi na kwa kushirikiana ili kujenga Shirika la Reli la kisasa lenye uwezo wa kujitegemea acheni vitendo vya hujuma na migomo vinavyoweza kudhoofisha shirika hili”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Mbunge wa Mvomero Sadick Murad akimwongoza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia) kuelekea katika daraja la Diwale, wa tatu kulia ni Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogoro Eng. Dorothy Mtenga.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amekemea vitendo wa wizi wa mafuta na kuhujumu Reli vinavyofanywa na watumishi wasio waaminifu na kuwataka kuwa wazalendo kwa nchi yao ili kuchochea kasi ya maendeleo.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino (Sekta ya Uchukuzi) Eng. Dkt. Leonard Chamuriho amewataka watumishi wa TRL Kuepuka migomo itakayoathiri utendaji wa Shirika hilo, kubuni mikakati ya kuwezesha shirika hilo kujiendesha kwa faida, kupambana na ubadhirifu wa mali na miundombinu na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta tija inayokusudiwa.

Profesa Mbarawa alikuwa kwenye ziara ya kukagua utendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano ambapo amepata fursa ya kukagua ujenzi wa mizani ya kisasa ya Mikese na kituo cha mtandao wa mawasiliano ya simu vijijini ya Halotel unaosambazwa katika taasisi za Serikali ikiwemo Hospitali, Polisi, Mahakama na Shule hapa nchini.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wananchi wa Turiani kuhusu kukamilika kwa ujenzi wa Darajala Diwale.
Muonekano wa Daraja la Diwale linalounganisha wilaya ya Mvomero na Kilindi.
Mafundi wanaotengeneza vichwa vya treni katika karakana kuu ya TRL, Mkoani Morogoro.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipata maelezo kutoka kwa mkandarasi Sanayejenga.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa akizungumza na Wafanyakazi wa TRL (Hawapo pichani), Wa pili kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Ucukuzi na Mawasiliano Eng.Wdwin Ngonyani, akifuatiwa na Kaimu Meneja wa TRL Morogoro Eng.Yusto Goima na Meneja TANROADS Morogoro Eng.Dorothy Mtenga.
Wafanyakazi wa karakana kuu ya Reli Mkoani Morogoro wakimsiliza Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa (Hayupo pichani), akiwapa muongozo wa kufanya kazi.

No comments:

Post a Comment