Saturday, February 6, 2016

DC MAKONDA ATOA SIKU 20 WENYEVITI WOTE WA SERIKALI ZA MITAA KINONDONI JIJINI DAR ES SALAAM WAPEWE RAMANI ZA MITAA YAO

 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (kulia), akizungumza na Watendaji na Viongozi wa Serikali za Mitaa wa wilaya hiyo kwenye mkutano uliofanyika Dar es Salaam leo kuhusu jinsi ya kutatua na kukomesha kero za ardhi
Watendaji na Viongozi wa Serikali za Mitaa wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo, Paul Makonda (hayupo pichani)


Na Dotto Mwaibale
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ametoa siku 20 kwa Wenyeviti wote wa Serikali za Mitaa  Manispaa hiyo kuwa na ramani ya mitaa ili kuyatambua maeneo ya wazi.
Makonda amewataka watendaji wa Manispaa hiyo kwenda na kasi ya serikali ya kuwatendea haki wananchi katika kumaliza migogoro ya ardhi.
Akizungumza Dar es Salaam leo mchana na Wenyeviti zaidi ya 100 wa Serikali za Mitaa ya9 Manispaa ya Kinondoni ,Makonda alisema baadhi ya watendaji wanatanguliza maslahi mbele kuliko mahitaji ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.
Alisema migogoro ya ardhi ni kero kila sehemu  misibani, harusini na kwenye mazishi suala kubwa ni la ardhi na kuongeza kuwa mabaraza ya ardhi ya Kata hayana uhalali wa kuamua kesi hizo kwa kuwa baadhi yao hata uelewa wa masuala hayo hawana na yamekuwa  yakiongeza matatizo.
"Leo tumekutana hapa kwa sababu ya migogoro ya ardhi na kuanzia sasa ndani ya Wilaya ya Kinondoni nataka kurudisha heshima ya Wenyeviti wa Serikali za  Mitaa nawaagiza kuanzia sasa mtu yeyote kutoka Wizarani,Manispaa au hata mwekezaji lazima apitie kwanza kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mitaa,"alisema.
Alisema watendaji wengi Manispaa ndio chanzo cha migogoro ya ardhi kwa kutotimiza wajibu wao na wameshindwa kuonyesha dira ya kuwasaidia wananchi.
"Kibaya zaidi ili kujitengenezea mazingira ya ulaji wenyeviti hawashirikishwi katika hatua za awali wanahusika zaidi pale kunapotokea mgogoro,"alisema.
Aliongeza kuwa "Sina hofu wala uoga wala sina sifa ya kupendwa wala kutafuta kupendwa hivyo nitahakikisha ninatumia Mamlaka niliyopewa kufanya migogoro hii ya ardhi Kinondoni na kuwa historia na nikitaka jambo huwa sishindwi"alisema.
Alisema baada ya wenyeviti hao kupewa ramani atahakikisha anakutana na Wazi ri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wilium  Lukuvi na maofisa wa ardhi.
"Hapo sasa watakaobainika kuhusika katika michezo michafu na kuchochea migogoro basi Waziri Lukuvi aondoke nao maana wameshindwa kazi"alisema
Makonda aliwataka wenyeviti hao kuonesha maeneo ya wazi na yale yaliyovamiwa ili kuchukua hatua kwani wenye dhamana wapo ofisini huku wananchi wakiwa wanateseka na migogoro hiyo.
Mkuu wa Idara ya Mipango Miji  Manispaa ya Kinondoni  Juliana Letara alisema Wenyeviti wote watapewa ramani za mitaa yao ndani ya wiki mbili kwa kuwa zipo kwenye kompyuta ofisini hivyo atawapatia ramani hizo.
Alisema kutokana na migogoro mingi ya ardhi anapendekeza kufanyike mapendekezo ya mabadiliko ya sheria kwa kuwa kesi zote za mabaraza ya kata zinaigharimu serikali zaidi ya  milioni tatu kwa siku.
Alizitaja kesi hizo kuwa ni za ardhi ya hifadhi,ardhi ya kawaida na ile ya kimila 
"Tulikopa benki ya TIB mkopo kwa  ajili ya kupima Viwanja likiwemo eneo la Mabwepande lakini kila siku tunatozwa riba ya sh.milioni tatu jambo ambalo ni gumu na ipo siku litashindikana na ndio maana tunauza Kiwanja hadi milioni 20 na 30,"alisema. 

Baadhi ya wenyeviti wa Serikali za Mitaa ambao walipata nafasi ya kuzungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo walimtaka Makonda kuondoa majipu sugu katika Manispaa hiyo likiwemo la maofisa mipango miji.
Alisema  wako tayari kufanyazi na Makonda lakini sio wafanyakazi hao kitengo cha ardhi kwa kuwa wamekuwa chanzo cha migogoro mikubwa ya ardhi.

No comments:

Post a Comment