Mfululizo mpya wa makala zilizochapishwa na The Lancet unatoa ushahidi kuwa kuboresha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kunaweza kuokoa maisha ya zaidi ya watoto 820,000 kila mwaka duniani na Dola za Kimarekani bilioni 300 kila mwaka.
“Katika kipindi cha miaka iliyopita kumekuwa na maendeleo katika kupunguza vifo vya watoto na utapiamlo nchini Tanzania. Hata hivyo, watoto 270 chini ya miaka mitano wanakufa kila siku na karibu asilimia 40 ya watoto hao wanakufa ndani ya mwezi mmoja wa kuishi. Kati ya watoto wanaonusurika, mtoto mmoja kati ya watatu wanadumaa kwa sababu ya utapiamlo sugu.
Watoto hawa wanakosa fursa zao katika maisha. Hali duni ya lishe inaathiri uwezo wa mtoto kujifunza na pia uwezekano wa mtoto huyo kutengeneza kipato akiwa mtu mzima. Lakini kuna afua zinazojulikana zinazoweza kusababisha mabadiliko makubwa na kuhamasisha kunyonyesha maziwa ya mama. ” amesema Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Bibi Maniza Zaman, wakati akiongea na vyombo vya habari Dar es Salaam. “Mfululizo wa makala ya “The Lancet” unatoa ushahidi wenye ushawishi kuhusu faida mbalimbali za kunyonyesha. Uwekezaji kwenye kulinda, kukuza, na kusaidia unyonyeshaji maziwa ya mama kunaweza kuokoa maisha ya watoto wa Tanzania, na hatimaye, kusaidia kukuza uchumi.”
Makala za “The Lancet” zinaonyesha kuwa kuna faida nyingi za kiafya za kunyonyesha maziwa ya mama. Unyonyeshaji maziwa ya mama kwa kiasi kikubwa sana kunaweza kuzuia karibu nusu ya matukio ya kuhara na theluthi moja ya maambukizo ya njia ya hewa– zikiwa ni sababu mbili zinazoongoza kupelekea vifo kwa watoto walio chini ya miaka mitano. Watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama kwa kawaida wanahitaji kupelekwa hospitali mara chache zaidi na kuwa na uwezekano mdogo wa kupata maambukizo na magonjwa, pia wana uwezekano mdogo zaidi wa kuwa na uzito mkubwa na kupata kisukari baadaye maishani mwao.
Kuna faida za kiafya kwa mama pia. Kwa kila mwaka ambao mama ananyonyesha, uwezekano wa kupata saratani ya matiti ya hatua ya pili unapungua kwa asilimia 6. Viwango vya sasa vya kunyonyesha maziwa ya mama tayari vinazuia vifo karibu 20,000 vinavyotokana na saratani ya matiti kila mwaka duniani – idadi hii inaweza kuwa kubwa zaidi kwa kuboresha mbinu za unyonyeshaji wa maziwa ya mama. Pia kunyonyesha kwa muda mrefu zaidi kumehusishwa na kupungua kwa saratani ya mfuko wa mayai.
Kuongeza viwango vya unyonyeshaji maziwa ya mama katika jamii kuna faida za kiuchumi. Watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama wanapata matokeo mazuri zaidi kwenye vipimo vya upeo wa kiakili. Kimataifa, imekadiriwa kuwa gharama zinazotokana na kuwepo na watoto wenye upeo mdogo zaidi wa kikakili unaohusishwa na kutonyonyeshwa maziwa ya mama ni jumla ya takriban dola za kimarekani bilioni 300 kwa mwaka. Nchi zenye kipato cha chini na kipato cha wastani zinapoteza zaidi ya dola za kimarekani bilioni 70 kila mwaka. Nchi zenye kipato cha juu zinapoteza zaidi ya dola za kimarekani bilioni 230 kila mwaka.
Hata hivyo, hapa Tanzania kuna mikoa inayooyesha mwelekeo unaotia moyo. Kwa mfano, mkoa wa Kilimanjaro, Tanga na Iringa ina asilimia 75 ya watoto wananyonyeshwa maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa. Zaidi ya nusu ya watoto wenye umri wa miezi 0-5 wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika miezi 6 ya mwanzo wako katika mikoa ya Iringa, Kigoma, Morogoro, Singida, Katavi na Geita, huku Kagera ikiwa na kiwango kikubwa zaidi cha asilimia 70.
Ili kuimarisha jitihada za kitaifa za kuboresha unyonyeshaji maziwa ya mama, vikwazo vinavyowakabili wanawake wengi duniani kote pia vinapaswa kushughulikiwa nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na:
• Mapungufu kwenye uelewa wa watoa huduma ya afya ambayo yanawaacha wanawake bila taarifa au msaada sahihi;
• Kukosekana kwa mifumo imara ya msaada kwenye familia na jamii, pamoja na mila na tamaduni zisizounga mkono kunyonyesha maziwa ya mama; na
• Likizo ya uzazi ya muda mfupi au kutokuwepo kabisa kwa likizo hiyo. Likizo ya uzazi ya muda mfupi inaweza kuongeza uwezekano wa kutonyonyesha maziwa ya mama au kuacha kunyonyesha maziwa ya mama mapema kwa asilimia 400;
Jambo lingine ni uuzaji usiofaa wa vyakula mbadala vya maziwa ya mama (ikiwa na pamoja na maziwa ya kopo kwa ajili ya watoto wachanga) na watengenezaji na wasambazaji ambao hutoa matangazo yanayohusiana na ulishaji wa watoto wachanga hali inayodhoofisha unyonyeshaji maziwa ya mama kama njia yenye ufanisi ya kuboresha afya katika siku za kwanza za maisha ya mtoto. Hapa Tanzania, Kanuni ya Uuzaji wa Chakula (Udhibiti wa Ubora) cha Mbadala wa maziwa ya Mama na Bidhaa Teule ya mwaka 2013, inalinda unyonyeshaji. – ufuatiliaji na utekelezaji imara zaidi wa Kanuni hiyo unahitajika.
Wanawake wanaofanya kazi wanahitaji kusaidiwa kupitia sheria zinazolinda uzazi zinazotosheleza. Kwa wanawake waliopo kwenye sekta isiyo rasmi, kuna haja ya kuboresha mifumo ya misaada ya kifamilia na kijamii, na kuandaa mazingira bora zaidi ya kufanyia kazi, ili kuokoa muda na nguvu za wanawake waweze kufanikisha unyonyeshaji maziwa ya mama.
“Kunyonyesha maziwa ya mama ni njia ya asili zaidi, yenye ufanisi zaidi wa gharama, iliyo rafiki zaidi kwa mazingira na rahisi zaidi tunayoijua ya kuwapa watoto wote, tajiri au maskini, mwanzo mzuri zaidi kiafya wa maisha,” alimalizia kusema Bibi Zaman. “Kuweka vipaumbele kwenye kuwekeza katika kukuza unyonyeshaji maziwa ya mama ni pendekezo bora.”