Thursday, January 7, 2016

Tunawajibika kuhakikisha Watanzania wananufaika – Prof Ntalikwa

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa akiwa katika kikao kazi na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo na Kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (Kulia) akimkabidhi mwongozo wa majukumu ya kazi Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe. Wanaoshuhudia ni Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (Kushoto) akimkabidhi mwongozo wa majukumu ya kazi Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo. Wanaoshuhudia ni Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara.

Na Veronica Simba
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa amesema ni jukumu la watendaji wote wa Wizara kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na rasilimali zinazotokana na sekta husika.

Aliyasema hayo hivi karibuni katika kikao chake cha kwanza cha kazi na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara.Profesa Ntalikwa alisema pamoja na jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na Wizara kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na rasilimali hizo, bado kuna manung'uniko kutoka kwa jamii hali ambayo inaashiria kuwa jitihada zaidi zinahitajika.

Akizungumzia sekta ya nishati, Profesa Ntalikwa alisema wananchi wanalalamika kuhusu kukatika-katika kwa umeme, gharama kubwa za umeme na ukosefu wa umeme wa uhakika na wa kutosha. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, alisema kunahitajika kuwepo miradi mipya ya kuzalisha umeme.

Aidha, alisema kuwa moja ya malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa wananchi ni kufufua na kujenga viwanda ili kukuza na kuimarisha uchumi. “Viwanda ni umeme, hivyo hatuna budi kuzalisha umeme wa kutosha.”

Kwa upande wa sekta ya madini, Katibu Mkuu Ntalikwa alisema jitihada zinatakiwa ili kufikia malengo ya kuongeza mchango wake katika pato la taifa kutoka asilimia 3.5 ya sasa hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025. 

“Tunapaswa kuweka mikakati thabiti itakayotuwezesha kufikia malengo hayo na kuyavuka ikiwezekana,” alisema.Profesa Justin Ntalikwa ni miongoni mwa Makatibu Wakuu wapya wa Wizara mbalimbali walioteuliwa na kuapishwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli. 

Manaibu Katibu Wakuu wapya wa Wizara ya Nishati na Madini walioteuliwa na kuapishwa na Rais Magufuli ni Profesa James Mdoe anayeshughulikia sekta ya Madini na Dk. Juliana Pallangyo anayeshughulikia sekta ya Nishati. 

No comments:

Post a Comment