Sunday, December 27, 2015

Mchechu azungumzia tuhuma dhidi yake na malengo ya NHC

Nehemiah Mchechu, moja ya majina maarufu katika nyanja za uongozi wa mashirika nchini, jina lake limeteka mitandao ya kijamii kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Ukiachana na umaarufu wa Rais John Magufuli mtandaoni kwa kazi yake ya ‘kutumbua’ majipu, Mchechu ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), anavuma kwa mema na ‘mabaya’.

Baadhi wanasifu mafanikio yake ya kuliimarisha shirika hilo kwa kipindi cha muda mfupi, lakini wengine wanamtuhumu kulitumia kujinufaisha ikiwamo kujilipa ‘mamilioni’ ya shilingi kama mshahara na posho za vikao.

Tuhuma zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii ni kwamba bosi huyo wa NHC, anajilipa mshahara Sh36 milioni kwa mwezi na kuhudhuria vikao vingi vya bodi vinampatia posho za kutisha.

“Kiwango hicho hakina ukweli,” anasema Mchechu, “mshahara wangu upo chini ya hapo,”anasema.

“Pia, huwezi kujilipa. Unalipwa kwa makubaliano maalumu tangu awali kabla ya kazi kulingana na kazi unayopewa,” anaongeza.

Mchechu anasema yupo NHC kulitumikia taifa kwa kuwa alipotoka sekta binafsi alikuwa akipata mshahara mkubwa, lakini alikubali kiwango kidogo serikalini kwa kuwa alikuwa akijua shirika hilo lilikuwa na hali mbaya kifedha na lilihitaji kuboreshwa.

Kuhusu vikao vya bodi na kamati mbalimbali anazotuhumiwa kushiriki na ‘kuvuna fedha’, Mchechu anasema kamati nyingi zinazorushwa mtandaoni siyo za kweli na hakuna fedha inayolipwa katika vikao hivyo.

“Watu wanapohoji mshahara wangu wanasahau kiwango ninachoingiza kwa Serikali. Jaribu kufikiri tumeirudisha ardhi ya Kawe Tanganyika Parkers yenye thamani ya zaidi ya Sh200 bilioni kutoka mikononi mwa aliyekuwa ameuziwa kipindi hicho, hivi ningekuwa mtu binafsi kwa kufanikisha majadiliano ya kurudisha kiwanja hicho, ningepata kiasi gani?” anasema.

Katika mahojiano maalumu yaliyofanyika hivi karibuni, Mchechu anaeleza kuwa Watanzania ni kigeugeu kwa kuwa wakati anaingia NHC mwaka 2010 akitokea Benki ya CBA, wengi walimuonea huruma wakieleza alikuwa anakwenda kupoteza weledi na mshahara, lakini sasa wanamzushia anapokea fedha nyingi zinazolifilisi shirika.

“Siku waajiri wangu wakigundua nalipwa mshahara mkubwa kuliko ninachofakifanya wataniondoa kwa sababu nawaletea hasara,” anasema.

Bosi huyo wa zamani wa Benki ya Standard Chartered alianza kazi mwaka 2010, wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, kwa kupatiwa mkataba wa miaka minne kuboresha shirika hilo lililokuwa likichechemea.

Mkataba wa awali ulimalizika mwaka jana na kusaini mwingine wa miaka mitano ambao unatarajia kumalizika mwaka 2018/2019.

Kama yalivyokuwa malengo ya Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1962, Mchechu, alikabidhiwa kazi ya kuendeleza sera ya kujenga makazi ya bei nafuu kwa Watanzania.

Kama ilivyokuwa kwa mashirika mengine ya umma, NHC halikuwa likipata faida kubwa ya kuwezesha kuendeleza miradi mikubwa na kwa mujibu ripoti za fedha za shirika hilo, mwaka 2010 lilikuwa limepata faida ya Sh3.1 bilioni.

Ili kulifanyia mabadiliko Shirika hilo, Mchechu anasema, ilihitajika akili na nguvu ya kutosha kwa sababu mambo yalikuwa yakiendeshwa kienyeji na kwamba baadhi ya vigogo walikuwa wakihusika kulifilisi NHC.

Mikataba ya vigogo

Anasema kuwa kuna baadhi ya vigogo serikalini na watumishi wa shirika hilo waliokuwa wakiendesha ukodishaji wa nyumba kwa mikataba ya kilaghai na NHC kwa kulipatia fedha kidogo wakati wanatoza fedha nyingi kwa wapangaji.

Kuna baadhi ya ‘madalali’ walikuwa wakililipa shirika kodi ya Sh700, 000 katika baadhi ya nyumba za biashara kwa mwezi wakati wao wanakusanya zaidi ya Sh5 milioni lakini mikataba hiyo ilivunjwa.

“Tumekirejesha alichokuwa akikitaka Baba wa Taifa kwa sababu kwa sasa karibu kila mkoa una nyumba za bei nafuu zilizojengwa na shirika,” anasema Mchechu akieleza kuwa hadi sasa wamejenga nyumba zaidi ya 3,000 za bei ya chini.

Katika mtandao wa nyumba hizo, zilizokuwa zikiuzwa bei ya chini kuliko zote nchini ni zile zilizopo mkoani Katavi ambazo zilikuwa Sh32 milioni kwa sababu huduma za umeme na barabara zilikuwa zimesogezwa.

Anaeleza kuwa wastani wa bei ya makazi ya bei nafuu ni Sh34 milioni kwa nyumba ya vyumba viwili na Sh43 milioni kwa nyumba ya vyumba vitatu na bei hupanda kutokana na gharama za ujenzi zikiwamo kuandaa miundombinu na kodi ya ongezeko la thamani.

Pia, gharama hizo anasema zinatokana na riba kubwa ya mikopo iliyopo sokoni na kupanda kwa thamani ya Dola ya Marekani mara kwa mara.

Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji wanasema nyumba hizo zinauzwa ghali na kununuliwa na mabepari pekee badala ya walengwa ambao ni watu wa kipato cha chini na sehemu kubwa zinadoda kwa kukosa wateja.

Kwa Mchechu, tuhuma hizo hazimnyimi usingizi. Na kabla ya kujibu hoja hiyo, anatasabasamu kidogo.

“Kila mradi tunaoufanya huwa tunalenga watu wa kundi fulani. Hatukurupuki. Tunaangalia wa kipato cha chini, kati na cha juu. Sina sababu ya kuficha.

“Lakini nyumba zetu ni za bei ya chini kulinganisha na kampuni binafsi hivyo naomba fananisha embe kwa embe na chungwa na chungwa na si vinginevyo,” anasema.

Mchechu anasema kuna baadhi ya miradi mikubwa kama ya Kawe na Morocco ni ya kibiashara zaidi na nyumba zake zinauzwa bei kubwa kwa kuwa zililenga kundi la watu ambao hukimbilia nje ya nchi kununua makazi lakini sasa wanataka wabaki nchini.

“Kama mtu ni wa malengo ya Sh50 milioni halafu anakosoa bei za mradi wa Kawe yupo sahihi kuona bei ile ni kichaa kwa sababu inaenda mara tatu hadi 10 ya kipato chake. Lakini mimi sikulenga kule,” anasema.

Nyumba za bei nafuu

Hata hivyo, anaeleza kwa kuwa NHC malengo yake ni kujenga nyumba za bei nafuu katika halmashauri zote nchini ambako tayari wamenunua ekari 5,600 huku nyingine 22,000 wapo kwenye mazungumzo ya kuuziana na wamiliki.

Kuhusu kudoda kwa nyumba, bosi huyo anapinga kidogo.

Anasema makazi mengi waliyoyajenga kwa bei nafuu yalinunuliwa yote na mengine kabla ya miradi yake kukamilika kupitia mikopo ambayo wananchi wanakopa benki za biashara kununua nyumba za NHC.

“Kibada, Kigamboni (Dar es Salaam) tuliuza ndani ya saa 48, mradi wa Eco Housing na Mchikichini zote zimeuzwa hata hizo za mikoani zina soko…hakuna zilizododa,” anasema Mchechu.

NHC inafahamika kwa muda mrefu kuwa na nyumba za kupangisha za bei nafuu nchini lakini kwa sasa miradi yake ya kupangisha haisikiki kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo, majibu ya kiongozi huyo yanashitua kidogo kwa wanasubiri kiwango kikubwa cha nyumba za kupangisha.

Anasema kuwa katika mikakati yao walipanga kujenga nyumba asilimia 70 kwa ajili ya kuuza na asilimia 30 ya kupangisha kwa watu wa hali ya chini.

Matangazo ya ukodishaji hayawi makubwa sana kama ilivyo katika uuzaji kwa kuwa wananchi wengi wanahitaji nyumba hizo, anaeleza.

“Tanzania ina upungufu mkubwa wa nyumba takriban 3.5 milioni hivyo iwapo nikisema nijenge nyumba moja kwa Sh100 milioni na kuikodisha ile fedha itasaidia familia moja tu lakini nikiuza nyumba mtaji ule nikauzungusha tunaweza kujenga zaidi ya nyumba nane za familia,” anasema Mchechu.

Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani ameanza kubadilisha utendaji kwenye utumishi wa umma na moja ya njia ya kufanikisha hilo ni ziara za kushtukiza katika taasisi na mashirika ya umma.

Mchechu amejiandaje na ujio wa kushtukiza wa Rais?

“Sisi tayari tulikuwa tunaendesha mambo yetu kwa mwendokasi na baadaye tutaongeza zaidi kasi,” anasema.

Katika uongozi wake, anaeleza aliyoyapata NHC yakiwamo kuongeza uwekezaji wa ujenzi nyumba nchini na kukuza mapato ya shirika ambayo mwaka jana yalifikia Sh130 bilioni kutoka Sh36.6 bilioni mwaka 2010 baada ya kubana matumizi na kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi.

“Pesa tumeikuza lakini haitosheelezi miradi hata ukichanganya na mikopo hivyo tunaendelea kutafuta fedha zaidi ili kufanikisha malengo yetu.

“Na pia niwe muwazi kabisa kama nitashindwa kutimiza malengo kwa miaka tisa niliyokaa NHC sidhani kama nitaleta kipya nikipatiwa miaka 20 hivyo baada ya hapa nitarudi sekta binafsi,” anasema.
  • Imeandikwa na Nuzulack Dausen via Mwananchi

No comments:

Post a Comment