Tuesday, November 24, 2015

WAZIRI MKUU ATAKA KILA MKURUGENZI ASOME HOTUBA YA RAIS, AIFANYIE KAZI

 Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akisalimiana na katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (TAMISEMI) , Jumanne Sajini baada ya kuwasili kwenye Ofisi ndogo ya TAMISEMI jijini Dar es salaam kuzungumza na watumishi Novemba 24, 2015.
 Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya Wakurugenzi baada ya kuwasili kwenye Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) jijini Dar es salaam kuzungumza na wafanyakazi Novemba 24, 2015.
 Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa  akizungumza na baadhi ya watumishi wa Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) jijini Dar es salaam Novemba 24, 2015. 
 Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) jijini Dar es slaam baada ya kuzungumza nao Novemba 24, 2015. 
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amewataka wakurugenzi wa vitengo na wakuu wa taasisi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) wapate nakala ya hansard ya hotuba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuzindua Bunge la 11, waisome na kufanyia kazi maeneo yote aliyoyaainisha.

“Katibu Mkuu hakikisha umepata hansard ya hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akizindua Bunge na uhakikishe kila mkurugenzi ana nakala na kila mmoja wenu lazima ahakikishe anafanyia maeneo ambayo Mheshimiwa Rais ameyaainisha. Ni lazima tuelewane ni nini tunapaswa tufanye,” alisema.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Novemba 24, 2015) wakati akizungumza na wakuu wa taasisi, wakurugenzi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kwenye mkutano uliofanyika ofisi ndogo ya TAMISEMI, barabara ya Kivukoni, jijini Dar es Salaam.

“Ninatamani kuona mabadiliko ya utendaji kazi Serikalini katika kipindi kifupi. Natamani kila mmoja asiridhike na uzembe unaofanywa huku chini. Ni nyote ni wataalamu, kwa hiyo mnapaswa kudhirisha elimu yenu na ujuzi mlionao,” aliwasisitizia Wakurugenzi hao.

Alisema kila mkurugenzi na mkuu wa taasisi anapaswa kuongeza usimamizi na ufuatiliaji wa kazi kwenye sekta yake kwani hilo litasaidia kukidhi matarajio ya Watanzania ya kuona mabadiliko ya utendaji kazi kwenye Serikali ya Awamu ya Tano. “Ninyi wakurugenzi siyo desk officers bali ni field officers. Nataka muweke utaratibu wa kwenda vijijini mkasimamie watu wenu, pia mhimize uadilifu, uaminifu na weledi wa kazi,” alisisitiza.

“Mambo ninayotaka mhimize watendaji waliopo chini yenu ni pamoja na haya yafuatayo: muda wa kuripoti kazini uzingatiwe, muda wa kukaa kazini uzingatiwe, utokaji kazini kwenda kwenye chai na chakula cha mchana udhibitiwe, na mipango na malengo ya kazi kwa siku ni lazima yafikiwe,” alisema.

“Tunataka kujua mtumishi amefanya nini tangu alipoingia ofisini. Suala siyo kukaa tu ofisini, kwani kuna mtu anakaa ofisini, hajaenda hata kunywa chai lakini ukiuliza amefanya nini hupati jibu la kueleweka. Sisi kama vongozi wao ni lazima tujue wanafanya kazi gani wanapokuwa maofisini,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa ameitisha kikao ofisini kwake kesho saa 4 asubuhi akitaka kupatiwa taarifa ni kwa nini mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) haujaanza kazi hadi sasa. “Kesho saa 4 asubuhi Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu DART na watendaji wako mje ofisini. Nataka kupata maelezo ni kwa nini mabasi hayajaanza kazi hadi leo, je ni lini yataanza kazi, je ni nani anakwamisha. Na hata kama ni sheria, ni kwa nini tusiziharmonise ili kuondoa hivyo vikwazo,?” alihoji Waziri Mkuu.

“Ninataka kupata haya maelezo kwa sababu Watanzania na hasa wana-Dar es salaam, wamesubiri kwa muda kuona mradi ukianza kazi ili uondoe kero ya usafiri. Wao wanajua anayehusika ni TAMISEMI,” aliongeza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi na viongozi wa TAMISEMI, Katibu Mkuu wa OWM-TAMISEMI, Bw. Jumanne Sagini alimweleza baadhi ya mafanikio na changamoto ambazo wizara hiyo imekabiliana nazo katika utendaji wake wa kazi.

Kuhusu ujenzi wa vyumba vya maabara kwa ajili ya kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi, Bw. Sagini alisema vyumba hivyo vimeongezeka kutoka 247 mwaka 2005/2006 na kufikia 6,161 mwaka 2014/2015. Pia alisema vyumba 4,228 viko kwenye hatua za kukamilika ujenzi wake.


Kuhusu utengaji wa madirisha ya kuhudumia makundi yenye msamaha kama wazee na watu wenye ulemavu hospitalini na kwenye vituo vya afya, Katibu Mkuu alisema nayo yameongezeka kutoka madirisha 5,074 mwaka 2010 na kufikia 7,903 mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 55.

No comments:

Post a Comment