Friday, November 27, 2015

SIKU KUU YA SHUKRANI NCHINI MAREKANI Photo by CARLOS BARRIA/REUTERS

Na Swahilivilla Blog Washington 
Mamilioni ya Wamarekani jana waliadhimisha Siku Ya Shukrani (Thanksgiving). Hii ni moja kati ya Siku Kuu rasmi nchini humu inayoadhimishwa kila Akhamis ya nne ya mwezi wa Novemba.
Asili yake:
Image: U.S. President Obama performs 68th annual pardoning of Thanksgiving turkey Abe at White House in Washington
Rais wa Marekani Barack Obama akimuachia huru Bata. Photo na CARLOS BARRIA/REUTERS
Vyanzo vya kihistoria vinatofautiana kuhusu asili ya Siku Kuu hii. Lakini maelezo yanayosadikiwa na wengi ni kuwa chimbuko lake linarejea mwaka 1621.
Walowezi kutoka Ulaya walipokuwa wakiwasili katika Mabara ya Amerika walipata matatizo ya kuanzisha maisha mapya. Mnamo mwaka 1620 meli iliyopewa jina la Mayflower ilitia nanga nchini Marekani ikiwa na abiria 102 kutoka Uingereza. Miongoni mwao walikuwemo Wakristo waliokuwa wakitafuta sehemu watakayokuwa huru kufanya ibada zao, na pia walikuwemo waliohajiri kwa ajili ya tamaa ya kumiliki ardhi.
Walipowasili Marekani walikumbana na matatizo mbalimbali yakiwemo ukosefu wa uzoefu wa mazingira mapya, na nusu yao walifariki dunia kutokana maradhi na mengineyo.
Baada ya kutimiza mwaka mmoja, mnao mwezi November 1621, Walowezi waliobakia hai kwa msaada wa wenyeji ambao waliwapa jina la "Wahindi Wekundu", walifanikiwa kupata vuno la mwanzo la mahindi. 
Kwa hivyo waliwaalika wenyeji wao na kufanya karamu maalum kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kuwapa neema zake, na kuwashukuru wenyeji wao kwa kuwasaidia mbinu za maisha katika ulimwengu uliokuwa mpya kwao. Inaarifiwa kuwa yakula vingi katika karamu hiyo iliyodumu kwa muda wa siku tatu vilitokana na mapisi ya wenyeji wa asili hapa Marekani.
Kutoka hapo siku hiyo ikawa inaadhimishwa katika makoloni mengine katika Bara la Amerika, kila koloni likiiadhimisha kwa aina yake tofauti. Mnamo mwaka 1863, Rais Abraham Lincolin akaitangaza kuwa Siku Kuu rasmi kitaifa.
Katika enzi za leo:
Siku Kuu Ya Shukrani au Siku Ya Kutoa Shukrani, imekuwa ni miongoni mwa Siku Kuu kubwa kabisa za kitaifa nchini Marekani ambayo huwakutanisha pamoja watu wa aila. Kwa vile inakuja siku ya Alkhamis, sehemu nyingi za kazi hutoa mapumziko siku ya Ijumaa pia, na hivyo kuwawezesha watu kusafiri kutoka sehemu mbalimbali kwenda kujumuika na aila zao, wakiongezea pia Jumamosi na Jumapili ambazo kwa kawaida huwa ni siku za mapumziko katika wiki.
Kwa hali hiyo, biashara katika sekta za usafiri na nishati nazo pia huchangamka kutokana na wingi wa watu wanaosafiri kutoka sehemu moja au nyengine. Sekta ya biashara inayokumbwa na mkosi siku hii ni mikahawa, kwa vile watu hula majumbani.
Kwa jina la utani siku hii huitwa "Turkey Day", kwa vile mlo mkuu katika karamu huwa ni bata mzinga, yakiwepo pia machopochopo mengine. Ikiwa siku hii ni faraja kwa wafanyakazi wanaopata mapumziko ya siku nne mfululizo na neema kwa wafugaji wa bata mzinga kwa vile biashara yao hungezeka, kwa viumbe bata hao hii inakuwa ni siku ya nakama kutokana na kuchinjwa kwa wingi.
Sehemu nyingi za kazi hutoa mabata wa bure kwa wafanyakazi wao au kadi za malipo ili kwenda kunua sehemu wanazotaka. Kwa kawaida karamu hii hufanyika wakati wa jioni, ingawaje baadhi ya watu huifanya majira ya mchana.
Wakati mabata wengi huonja uchungu wa visu kwa ajili ya Siku Ya Shukrani, angalau bata mmoja husalimika. Hii ni kutokana na ada ya kila mwaka ya Ikulu ya Marekani kumwachia huru bata kama sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo. Siku ya Jumatano, Rais Barack Obama aliwaachia huru mabata wawili. Sherehe hizi hufanyika rasmi wakiwepo pia waandishi wa habari.
Miongoni mwa ada za Siku Kuu Ya Shukrani, ni mchezo wa kabumbu la Kimarekani (American Football). Jioni, wakati watu wakiwa wanawararua mabata majumbani, halkadhalika hupata nafsi ya kuburudika kwa kuangalia pambano la mchezo huo unaopendwa zaidi nchini humu, ambalo aghalabu huwa la kukata na shoka. Timu zinazopata nafasi ya kucheza siku hiyo hujisikia heshima kubwa.
Changamoto zake:
Ingawaje Siku Ya Shukrani ni katika Siku Kuu kubwa nchini Marekani, hata hivyo pia inakabiliwa na changamoto zake. Kuna zile za watu wanaopigania haki za wanyama na kuwahurumia mabata wanaochinjwa kwa wingi katika siku hii. Aidha kuna changamoto za kihistoria.
Baadhi ya watu wanaipinga Siku Kuu hii kwa vile kusherehekea kwake ni sawa na kuhalalisha Ulowezi na Ukoloni na Ubeberu wa Wazungu katika Mabara ya Amerika. Itakumbukwa kwamba, leo hii tunapoitaja Marekani akilini mwetu zinatujia sura za Wazungu, na wenyeji wa asili takriban hawajulikani kabisa.

No comments:

Post a Comment