Saturday, October 24, 2015

YALIYOJIRI KWENYE MSAFARA WA WAENDESHA BAISKELI KUTOKA MBEYA KWENDA JIJINI DAR ES SALAAM

Rais wa Chama cha Waendesha Baiskeli Tanzania, Godfrey Jacks Muhagama, ambaye pia ni miongoni mwa waendesha baiskeli kwenye msafara huo ulioanzia Mbeya akitoa maelezo ya namna shughuli hiyo ilivyofanikiwa.
 Mwakilishi wa Norwegian Church Aid nchini Tanzania, Tale Hungnes akiwapongeza waendesha baiskeli mara baada ya kufika Dar es Salaam wakitokea kwenye mpaka wa Malawi na Tanzania, Kasumulo Mbeya.
 
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dr. Rashid Rutengwe akisaini madai ya haki ili kuweka imani yake kwa viongozi wa kiserikali ambao watakwenda kwenye mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP21 utakaofanyika desemba mwaka huu huko Paris, Ufaransa.
Wanafunzi wa shule za msingi Wambi na Nyamalala, James Lyimo (kulia) na Vannesa Mgata wakionyesha mti waliokabidhiwa kwaajili ya kupanda katika shule zao
Ofisa Miradi wa Norwegian Church Aid, Tanzania, Gilbert Mworia akikabidhi mti kwa viongozi wa dini Mufindi, Mkoani Iringa, kutoka kulia ni Imamu wa Msikiti Mkuu wa Mafinga na Mch. Annuai Mwinuka wa KKKT, Jimbo la Mufindi Usharika wa Mafinga, zoezi hilo lililofanyika kwenye shule za Msingi Wambi na Nyamalala zote za Mafinga.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dr. Rashid Rutengwe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waendesha baiskeli na viongozi wa msafara huo
Ofisa Miradi wa Norwegian Church Aid, Nizar Suleiman akitoa maelezo juu ya msafara wa kampeni ya uhamasishaji juu ya mabadiliko ya tabianchi, baada ya kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwenye shule ya Sekondari Kola Hill.
Waendesha baiskeli wakiwa katika eneo la Ruaha Mbuyuni
Mwakilishi wa Norwegian Church Aid nchini Tanzania, Tale Hungnes akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waendesha baiskeli, walipofika kwenye mji wa Ilula, Mkoani Iringa.
Baadhi ya akina mama wa mji wa Makambako wakisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa vijana wahamasishaji wa elimu ya mabadiliko ya tabianchi wa YouthCAN Tanzania
Msafara wa waendesha baiskeli ukiingia kwenye mji wa Ilula Mkoani Iringa
Esther Joshua ambaye ni mwanamke pekee kwenye msafara wa kuendesha baiskeli kutoka Mbeya mpaka Arusha, hapa akiwa nje kidogo ya mji wa Mafinga kuelekea Iringa Mjini.
Waendesha baiskeli wakielekea jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Muhongo Rweyemamu akipanda mti kwenye shule ya Sekondari Kola Hill, Mkoani Morogoro ambayo ni sehemu ya kampeni hiyo

Na Dotto Kahindi

Msafara wa Kampeni ya uhamasishaji juu ya mabadiliko ya tabianchi kupitia uendeshaji wa baiskeli ambao ulianza Octoba 17 mwaka huu kwenye mpaka wa Tanzani na Malawi umefika jinini Dar es Salaam ambako utasimama kupisha zoezi zima la uchaguzi mkuu kabla ya kuelekea Namanga Arusha.

Msafara huo ambao umekuwa ukipata mapokezi makubwa kutoka kwa viongozi mbalimbali wa serikali, dini na wananchi kwa ujumla, ukiwa Mkoani Morogoro ulipata mapokezi makubwa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo Dr. Rajab Rutengwe.

Mkuu huyo wa mkoa amewapongeza waendesha baiskeli na kuwaita ni mashujaa na mabalozi wazuri wa kuhamasisha jamii kutunza  mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Msafara huo ambao umeanzia Msumbiji kupitia Afrika Kusini Botswana, Zimbabwe, Zambia, Malawi na sasa Tanzania, utafikia kilele chake mjini Nairobi Kenya mwezi novemba mwaka huu.

Dr. Rutengwe amesema kuwa jambo la kutunza mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi ni muhimu na ni jambo la kila mmoja wetu.
Amewakemea viongozi wa serikali wanaoshirikiana na wananchi kuharibu mazingira kwa kukata miti na kuuza mikaa na kuahidi kuwashughulikia baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.

Akizungumzia umuhimu wa milima ya Uluguru, Nguu na Ukaguru anasema ni muhimu kwa kuwa ni moja ya vyanzo vya maji ambayo huwanufaisha watu wa mikoa ya Morogoro, Dodoma, Pwani na Dar es Salaam. 

“Sisi watu wa Morogoro tukiwa wabinafsi kwa kuharibu vyanzo vya maji kwa kufanya uharibifu kwenye milima ya Uluguru, Nguu na Ukaguru tutakuwa tunawaua wenzetu wanaotegemea milima hiyo” anasema Dr. Rutengwe

Akitoa taarifa ya msafara huo, Ofisa Miradi wa Norwegian Church Aid, Nizar Suleiman anasema kuwa lengo la msafara huo ni kujenga uelewa kwa jamii juu ya mabadiliko ya tabianchi kwa kupitia uendeshaji wa baiskeli na kutumia vijana kutoka kwenye taasisi za kidini nchini kufikisha elimu hiyo.

Anasema msafara huo utahusisha pia uchukuaji wa saini za wananchi ili kuweka imani zao kwa viongozi wa kiserikali ambao watakwenda kwenye mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP21 utakaofanyika desemba mwaka huu huko Paris, Ufaransa.

Msafara huo unatarajiwa kuendelea tena novemba 3 mwaka huu, ukitokea jijini Dar es Salaam kuelekea Namanga Mkoani Arusha ambapo utakabidhiwa kwa waendesha baiskeli wa Kenya.

No comments:

Post a Comment