Tuesday, October 20, 2015

WANAFUNZI WA ST. JOSEPH WACHANGIA CHUPA 125 ZA DAMU MUHIMBILI

  Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya akitoa damu leo jijini Dar es Salaam katika shule ya St. Joseph Cathedral High School zamani ikijulikana Shule ya Sekondari Forodhani. Balozi Msuya ambaye alisoma kwenye shule hiyo mwaka 1975 ni mmoja wa wanafunzi wa zamani waliojitokeza kutoa damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaotibiwa Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
 Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya akiwa na wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo hivi sasa. Kutoka kulia ni Benjamin Fred, Maria Joseph na Vanessa Elieza Mwakila. 
 Mmoja wa wanafunzi akichangia damu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

WANAFUNZI waliosoma St. Joseph Cathedral High School zamani ikijulikana Shule ya Sekondari Forodhani leo wamejitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya Watanzania ambao wanahitaji damu.

Wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo hivi sasa kwa kushirikiana na wenzao wa zamani wamefanikiwa kutoa chupa 125 za damu.

Akizungumzia katika uchangiaji wa damu shuleni hapo , Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha amesema suala la damu ni changamoto kwani hospitali hiyo inahitaji wastani damu wa chupa 100 kila siku na kwamba kwa siku hivi sasa zinapatikana chupa 24 hadi 40.

Alifafanua kwamba hivi sasa hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa wastani wa chupa 60 za damu kwa siku.

Kutokana na hali hiyo amewaomba Watanzania kuendelea kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya Watanzania kwani suala hilo linagusa maisha ya watu wote.

Ametaja makundi ambayo huitaji damu kwa haraka kuwa ni wagonjwa wa dharura, mama wajawazito, watoto na wagonjwa wa saratani.

Aligaesha amewashukuru wanafunzi hao na wale wanaosoma hivi sasa kwenye shule hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kuchangia damu na kusisitiza kuwa kitendo walichokifanya ni cha kuigwa.

Kwa upande wa wanajumuia waliosoma shuleni hapo wamesema wameamua kujitokeza kuchangia damu ili kuwahamasisha wanafunzi kuwa na utamaduni wa kujitolea katika jamii jambao ambalo hivi sasa limefifia.
Aidha kwa upande wa MNH imekuwa ikitoa matangazo mbalimbali ili Watanzania wajitokeze kuchangia damu kwa wagonjwa wanaopatiwa matibabu kwenye hospitali hiyo.

Katika shughuli ya leo, Balozi Msuya alifika katika shule hiyo na kuchangia damu kama walivyofanya wanafunzi wengine waliosoma hapo miaka 1950.

Balozi huyo alisoma katika shule hiyo mwaka 1975, baadhi ya wanafunzi wengine ni Mariam Zialora ambaye amesoma hapo 1964, Glen Dias mwaka 1954, Saada Jaha mwaka 1970, Albertina Doarado mwaka 1968, Solomon Mihayo mwaka 1990, Tahir Othman 1990, Edith Mabena mwaka 1992, Edward Makwani mwaka 1970 na Ephrahim Tumwidike mwaka 2012.
Leo wanafunzi hao wa zamani wameonyesha upendo wa hali ya juu kuungana na wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo hivi sasa katika kuchangia damu. Uamuzi huo wa wanafunzi hao wa zamani unapaswa kuigwa na shule nyingine kwa lengo la kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu.

Shughuli ya kuchangia damu leo imefanywa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS).

No comments:

Post a Comment