Monday, October 19, 2015

UJUMBE WA TPDC WATEMBELEA UBALOZI WA TANZANI LONDON

 Mheshimiwa Naibu Balozi wa Tanzania, London, Mhe. Msafiri Marwa, akizungumza machache kumkaribisha Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Bwana Michael P. Mwanda, kuzungumza na baadhi ya Maafisa wa Ubalozi huo. Mwenyekiti huyo wa TPDC, alipata fursa ya kutembelea Ofisi za Ubalozi mara baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Baraza la utetezi, ukuzaji na uendelezaji wa shughuli za kiuchumi (Global Local Content Council), kutokana na ugunduzi wa rasilimali za mafuta na gesi katika nchi husika, uliofanyika hapa London (13-15 October 2015), Mwenyekiti Michael Mwanda aliambatana na Mtaalam wa Mafuta na Gesi kutoka TPDC, Engineer Antelimi D nchini Uingereza.
 Naibu Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Msafiri Marwa (kushoto), kwenye picha ya Pamoja na  Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Bwana Michael P. Mwanda (kati) na Engineer Engineer Antelimi. Ujumbe huo wa TPDC ulitembelea Ofisi hizo za Ubalozi na kupata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya Maafisa wa Ubalozi.
Naibu Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Msafiri Marwa ( wa nne, kushoto), kwenye pichani, pamoja na  Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Bwana Michael P. Mwanda ( wa nne, kulia) na Engineer Engineer Antelimi (pili kulia). Pichani kutoka kulia ni Bwana Magnus Ulungi (kwanza kulia), dada Isabella Kafumba, Bwana Michael Mwanda, Balozi Msafiri Marwa, Bwana Yusuf Kashangwa, Bwana Allen Kuzilwa pamoja na Kanali Jackson Mwaseba.


UJUMBE WA TPDC WATEMBELEA UBALOZI
TANZANIA ilikuwa ni miongoni mwa nchi zilizowakilishwa kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa Baraza la utetezi, ukuzaji na uendelezaji wa shughuli za kiuchumi (Global Local Content Council), kutokana na ugunduzi wa rasilimali za mafuta na gesi katika nchi husika, uliofanyika hapa London (13-15 October 2015)

Lengo kuu la Baraza hili ni kuzifanya nchi husika zinufaike na rasilimali inayopatikana katika nchi hizo na isiwe ni kwa wawekezaji wa kigeni tu (ambao ndio wenye mitaji na teknolojia ya kutosha inayowawezesha kutafiti na hatimaye kufikia kuivuna rasilimali hiyo).

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo uliongozwa na Ndugu Michael P. Mwanda, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC). Wajembe wengine waliokuwa naye mkutanoni ni Engineer Antelimi D. Raphael kutoka TPDC na Yusuf Kashangwa kutoka Ubalozi wa Tanzania hapa London.

Baada ya Mkutano huo, ujumbe wa TPDC pia uliutembelea Ubalozi na kupata fursa ya kuongea na watumishi juu ya masuala ya msingi yanayoihusu sekta ya mafuta na gesi nchini Tanzania. Ndugu Mwanda alianza kwa kuieleza historia fupi ya utafiti wa mafuta nchini, kwamba ulianza (1954) kabla hata hatujapa uhuru. Hata baada ya Uhuru, utafutaji wa mafuta mafuta uliendelezwa tena kwa bidii zaidi hasa baada ya kuundwa kwa TPDC. Alisema pamoja na lengo kuwa la utafutaji wa mafuta, Tanzania haikuweza na haijaweza kuyapata, na badala yake imefanikiwa kugundua tu gesi.

Kampuni ya Agip ndiyo iliyokuwa ya mwanzo kugundua gesi hapo Songo Songo baada ya kufanya utafiti kwa kipindi kirefu (1969-79). Lakini mwanzo walisema kiasi kilichopatikana ni kidogo hakitoshelezi mahitaji ya kibiashara. Agip walendelea kufanya utafiti na hatimaye waliweza kugundua tena gesi mara hii hapo Mnazi Bay mwaka 1982. Gesi hii haikupata kutumika kutokana na wagunduzi kudai haitoshelezi. 

Kutokana na matatizo ya umeme unaotokana na nguvu ya maji kwa sababu ya ukame, ndipo wataalamu wa Shirika la Taifa la Petroli (TPDC) walipochukua hatua mnamo mwaka 1992 ya kufanya tena tathmini ya kiasi cha gesi iliyokwishagunduliwa na hatimaye waliweza kugundua kuwa kulikuwa na kiasi kikubwa cha gesi hapo Songo Songo mwaka 1999, hatua iliyopelekea Serikali kufanya uamuzi wa kuitumia gesi hiyo kuzalisha umeme hapo Songo Songo (2004) na Mnazi Bay (2006).

Baada ya hapo shughuli za utafiti wa mafuta na gesi ukaelekezwa zaidi baharini na hatimaye kiliweza kugundulika kiasi kikubwa cha gesi baharini mwaka 2010. Kuanzia hapo macho na masikio ya walimwengu yakaelekezwa Tanzania na Makampuni mwengi ya kigeni yakaonyesha nia zaidi ya kuja kuwekeza katika sekta hii.

Kwa hiyo mpaka sasa kiasi cha rasilimali hii ya gesi ni 47 TCF kilichopatikana baharini na 8TCF zilizopatikana pwani. Jumla ya kiasi cha gesi kilichikwisha thibitishwa kupatikana na 55 TCF.
Baada ya historia hiyo fupi, ndugu Mwanda alieleza baadhi ya hatua zilizokwishachukuliwa na Serikali katika kufanya maandalizi ya kuhakikisha kuwa nchi au Watanzania wananufaika na ugunduzi wa rasilimali. Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuzipitia na kutunga Sera mpya za Utafiti wa Petroli na Gesi, Nishati, na kutungwa kwa Sheria za ushirikishaji wa wazalendo na ya Matumizi ya mapato yatokanayo na rasilimali hizi.

Hatua nyingine ni kuanza kutumia gesi katika kuzalisha umeme palepale inapopatikana na kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara na kiasi kingine kusafirishwa kwa njia ya bomba hadi Dar es Salaam, kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme ili kupunguza makali ya mgao wa umeme uliokuwa ukiikabili nchi kutokana na kutegemea nguvu ya maji ambayo yameendelea kupungua mwaka hadi mwaka kutokana na ukame.

Hatua nyingine ambayo imechukuliwa na Serikali ni kuwaelimisha wananchi wananchi juu ya masuala yanayoihusu Sekta hii ili wasiwe na matarajio yasiyoweza kutekelezeka kutokana ushawishi wa taarifa zisizokuwa sahihi zinatolewa na watu tu mitaani kutokana na ugunduzi wa rasilimali hii, ikawa ndiyo sababu ya kubweteka kiuchumi au ya uvunjifu wa amani iliyopo.


Kwa mfano, uvunaji wa gesi iliyopo baharini, unahitaji maandalizi makubwa ya ujenzi wa miundo mbinu na viwanda huku Pwani vitakavyotumia gesi hiyo. Sghuli hizo bila shaka haziwezi kukamilishwa hivi karibuni. Wataalam wanasema kuwa zinaweza kukamilishwa labda katika kipindi cha miaka kumi ijayo. 

Hivyo ni vizuri pia wananchi wakaendeleza shuguli zao za kiuchumi katika sekta nyingine, kwani utegemezi katika sekta moja hauwezi kuwa ni ufumbuzi wa matatizo yote ya kiuchumi. Muda huu wakati hatua za maandalizi zinaendelea, ni vyema vijana wakaendelezwa kitaaluma ili baadae waweze kupata fursa za ajira katika sekta hii.

No comments:

Post a Comment