Monday, October 5, 2015

TANZANIA YASHUKURIWA KWA KUSAIDIA KUREJESHA AMANI KWA BAADHI YA MAENEO YA MASHARIKI MWA DRC

 Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa MONUSCO, Bw. Martin Kobler akisisitiza jambo wakati wa mazugumzo yake na  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania,  Balozi Tuvako Manongi. Bw. Kobler alifika katika Ofisi za Uwakilishi wa Kudumu, kuishukuru Tanzania kwa mchango wake wa ulinzi wa amani katika Mashariki ya DRC. Mchango ambao amesema umeleta tofauti kubwa.
"Tafadhali nifikishie salamu  na shukrani zangu  kwa Mhe. Rais, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri wa Ulinzi" maneno ya  Bw. Martin Kobler kwa Balozi Manongi walipokuwa wakiagana  baada ya mazungumzo yao mwishoni mwa wiki. 

Na Mwandishi Maalum, New   York 
Ushiriki  wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Misheni ya  kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa  katika  Jamhuri ya Kidemokrasi  ya Kongo ( MONUSCO), kumeelezwa kutoa mchango mkubwa katika kurejesha hali ya Amani na utulivu katika baadhi ya maeneo ya   Mashariki ya nchi hiyo.

Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki,  na  Mwakilishi  Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  katika  DRC na Mkuu wa MONUSCO  Bw. Martin Kobler, wakati alipofanya  mazungumzo na Balozi Tuvako Manongi,  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Bw. Kobler  na ambaye alitumia fursa hiyo kuaga na kuishukuru  Tanzania kwa  ushiriki  na  mchango wake,  amesema,  katika maeneo mengi  ambayo walinzi wa Amani  wa Tanzania  wanayalinda hali ya Amani imerejea kiasi  ambacho wananchi waliokimbia  vita wamerudi na kuendelea na shughuli zako za kila siku.

“ Katika  maeneo  kwa mfano la Kamango ambako wapo wanajeshi wa Tanzania,  nilipowauliza wananchi wa eneo  lile ni nini wanachotaka, jibu lao lilikuwa moja tu,  waliniambia wanataka amani na usalama,  wanaomba walinzi wa Amani wa  Tanzania     wasiondoke kwa sababu wakiondoka   hawana  uhakika wa usalama wa maisha yao” anasimulia  Kobler.

Akasema  mji huo wa Kamango wenye wakazi wapatao 80,000  ambao ulikuwa magofu na usiokuwa na  watu, hivi sasa hali imebadilika, watu wamerejea,  mji  umestawi biashara zimeshamiri na wananchi wanaendelea na shughuli zao pasipo kuwa na mashaka ya  usalama wao.

“ Ninazo simulizi nyingi kuhusu utendaji mzuri wa wanajeshi wenu, ni wazi pia katika utekelezaji wa majukumu yao, wapo waliopoteza maisha, lakini mchango wao na maisha yao hayakupotea bure wamefanya kazi nzuri. 

Mimi binafsi  naomba unifikishie salamu zangu na   shukrani zangu za dhani kabisa kwa viongozi wako  wakuu,   Mhe. Rais Kikwete,  Waziri wa Mambo ya  Nje  na  Waziri wa Ulinzi  ambao sikupata  nafasi ya kuwashukuru mimi mwenyewe”. anasema Kobler.

Jeshi  la Wanachi wa Tanzania  linahudumu katika Misheni ya MONUSCO  kupitia Force Intervention  Brigade ( FIB) ambayo inaundwa na wanajeshi kutoka Tanzania,  Afrika ya Kusini na Malawi.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu,   amesisitiza  umuhimu  na  nafasi ya Afrika  na hususani Nchi za Maziwa   Makuu wa kuhakikisha kwamba wanaendelea kuisaidia DRC  ili iweze kuwa na Amani ya kudumu.
Kwa upande wake,  Balozi Tuvako  Manongi  amemshukuru Bw.  Martin Kobler kwa  kuwajibika katika pindi cha miaka miwili ya  uwakilishi wake, na mchango wake  katika kujaribu kuwakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha   Amani na utulivu unakuwapo katika DRC.

Akasisitiza kuwa Tanzania kama ilivyo kwa  nchi nyingine inataendelea kusaidia kwa kadri inavyowezekana na kwa kushirikiana na  wadau wengine ili wananchi wa DRC hususani mashariki mwa nchi hiyo na ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi  katika mazingira magumu na hatari wanakuwa na fursa ya kuendesha maisha yao kwa Amani na utulivu.

Akaongeza kwamba ili hatimaye Amani ya kudumu iweze  kupatikana,  utashi  na ukomavu wa kisiasa kutoka makundi yanayopigana ndani ya DRC yenyewe  unahitajika kwa kuweka silaha zao  chini na kuzugumza na kuweka maslahi ya wananchi wao mbele ya kitu kingine.


No comments:

Post a Comment