Friday, October 23, 2015

TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA DODOMA MHE. CHIKU GALLAWA KUHUSU UCHAGUZI MKUU WA OKTOBA 25, 2015 MKOANI DODOMA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
 TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA


Mkoa wa Dodoma
Anwani ya Simu REGCOM
Simu Nambari: 2324343/2324384
E-Mail No. ras@dodoma.go.tz
Fax No. +255 026 2320046





    Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,
                            S.L.P.  914,
                              DODOMA.

Ndugu wananchi wa Mkoa wa Dodoma, tarehe 25 Oktoba, 2015 ni siku ya Uchaguzi Mkuu hapa nchini; ambapo, Watanzania wale wenye sifa za kupiga kura na waliojiandikisha, watapata fursa na kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi mbalimbali wa nchi yetu, kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani.

Maandalizi ya kufanikisha zoezi la Uchaguzi Mkuu kwa Mkoa wa Dodoma yamekamilika. Hadi kufikia siku ya leo tayari wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma wameshapokea vifaa vyote vitakavyo tumika kwenye zoezi la uchaguzi. Hadi tunavyozungumza sasa, vifaa hivyo vinapelekwa kwenye vituo vya kupigia kura.

Vilevile, wasimamizi wa uchaguzi kwenye wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma wameshapokea fedha za kuendeshea uchaguzi Mkuu.  Aidha, Mafunzo kwa watendaji wote watakaoshiriki katika zoezi la uchaguzi yanahitimishwa kwenye wilaya za Dodoma.

Mkoa wa Dodoma tumefanikiwa kuandikisha jumla ya wananchi 1,053,136 kuwa wapiga kura sawa na asilimia 102.74 ya lengo, ambapo lengo ilikuwa kuandikisha watu/wapiga kura 1,025,084, Hivyo, natumia fursa hii kuwataka wale wote waliojiandikisha kupiga kura katika Mkoa wa Dodoma, kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Jumapili Oktoba 25.

Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa 1:00 asubuhi na zoezi la kuhesabu kura litaanza saa 10:00 jioni. Natumia fursa hii kusisitiza mambo machache ya muhimu kwenye zoezi la uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na wadau mbalimbali wanaoshiriki Uchaguzi Mkuu kama ifuatavyo:
·        Wananchi wale wenye sifa za kupiga kura, wanahimizwa kwenda kupiga kura kwa amani na utulivu kwa kuzingatia muda na kisha kurejea makwao/majumbani baada ya kumaliza kupiga kura.

·        Viongozi wa vyama vya siasa na wagombea wa nafasi mbalimbali wawaandae wanachama na wafuasi wao kwenda kupiga kura, bila kuvunja sheria za uchaguzi, taratibu na kanuni zilizowekwa; wakidumisha hali ya Amani na utulivu.

·        Hairuhusiwi kwa mtu yeyote siku ya uchaguzi kufanya kampeni ya aina yoyote wala kuvaa mavazi ya chama chochote cha siasa.
·        Hairuhusiwi kwa mtu yoyote kutoa Rushwa kwa lengo la kumshawishi mtu kupiga kura au kumshawishi asipige kura.

·        Kila mtu aliyejiandikisha kupiga kura atunze shahada yake ya kupigia kura na asiitoe kwa mtu mwingine wala yeye kutumia shahada ya mtu mwingine kwani ni kosa la jinai kutumia shahada ya mtu mwingine kupigia kura. vilevile ni kosa kutumia shahada bandia.

·        Ni vizuri kila mmoja akahakikishe jina lake kwenye kituo alichojiandikishia ili kupata uhakika wa kuwepo kwenye orodha na kupiga kura kabla ya siku ya kupiga kura Oktoba 25.

·        Wananchi wote wakae katika hali ya utulivu wasiwe na hofu wala woga, Jeshi la polisi litafanya doria mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha kunakuwa na hali ya Utulivu na hali ya Amani ili kila mtu apate fursa ya kushiriki zoezi la Uchaguzi.

Kabla sijahitimisha salamu zangu, narudia kuwasisitiza Wananchi wote wa Dodoma wale wenye sifa za kupiga kura wajitokeze kwa wingi kupiga kura siku ya Jumapili, Serikali imejiandaa vya kutosha na kuwahakikishia wananchi uchaguzi Mkuu kufanyika kwa amani, utulivu na kuwa uchaguzi wa Huru na Haki.

Nawaomba wananchi wote wajiepushe na vitendo vyovyote vinavyosababisha vurugu na Uvunjifu wa Amani; tuendeleze sifa yetu ya Mkoa wa Dodoma kufanya Uchaguzi tukiwa katika hali ya usalama.

Mwisho kabisa, nawatahadharisha wale wote wenye nia mbaya au wanaojipanga kutaka kujaribu kuvuruga zoezi la uchaguzi au kuleta vurugu ya aina yoyote hapa Mkoani Dodoma kuwa,  vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga imara na vitamshughulikia mara moja mtu huyo. Wananchi mnaombwa kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama au kwa kiongozi yoyote wa eneo husika.
  
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

Imetolewa na:
OFISI YA MKUU WA MKOA WA DODOMA

Oktoba 23, 2015.

No comments:

Post a Comment