Thursday, October 22, 2015

MABALOZI WAIPONGEZA TAASISI YA JKCI KWA KUFANYA UPASUAJI WA MOYO

Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amezungumza na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini kuhusu shughuli za upasuaji wa moyo zinazofanywa na taasisi hiyo. Profesa Janabi amezungunza na mabalozi hao katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo.
 Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Thami Mseleku (kushoto) na Balozi wa Rwanda hapa nchini, Eugene Kayihura (kulia) wanamsikiliza Profesa Mohamed Janabi wakati akieleza mambo ambayo watu wanapaswa kuzingatia ili kuepuka shinikizo la damu kwenye mkutano uliofanyika Hoteli leo Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
 Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Judith Kangoma (kulia) na mwenzake wa Malawi, Hawa Ndilowe wakimsikiliza Profesa Mohamed Janabi leo.
Picha zote kwa Hisani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)

 MABALOZI wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania wameipongeza Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa kuanzisha huduma ya upasuaji wa moyo.

Mabalozi hao wamefurahishwa na huduma hiyo na kueleza kwamba watawashauri raia wao kwenda kupatiwa matibabu kwenye taasisi hiyo.

Balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania, Balozi Edzai Chimonyo amesema kwamba wamefurahishwa na juhudi za taasisi hiyo na kwamba wanapenda kujua jinsi ya kuzuia matatizo ya moyo.

“Napenda kujua ni vipi mtu anaweza kuzuia matatizo ya moyo,” amesema Balozi Chimonyo.
Naye Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Thami Mseleku amesema kwamba ataitumia taasisi hiyo kupima afya yake na kwamba endapo atatozwa fedha kwa ajili kupatiwa matibabu yupo tayari kutoa ili kusaidia wagonjwa wa kawaida wanaopatiwa matibabu hapo.

Akizungumza na mabalozi hao, Kaimu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Mohamed Janabi amesema ili watu wasipate shinikizo la damu wanapaswa kufanya mazoezi, kupima afya mara kwa mara na kuchunguza endapo familia ina tatizo la shinikizo la damu.

Profesa Janabi amesema kwamba endamba mabalozi hao watazingatia hayo wataepuka kupata shinikizo la damu.

Awali Profesa Janabi amewaeleza mabalozi hao huduma zinazotolewa na taasisi hiyo ikiwamo kufanya upasuaji kwa watoto 37 hivi karibuni wakimo watoto wawili kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).

Profesa Janabi amesema upasuaji wa moyo unaofanywa na hospitali hiyo unasaidia kupunguza gharama za matibabu endapo wangekwenda kutibiwa India.
Amesema gharama za mgonjwa kufanyiwa upasuaji wa moyo India ni kuanzia Dola 10,000 hadi 12,000 wakiwamo ndugu wanaomsindikiza mgonjwa nchini humo.

No comments:

Post a Comment