Wednesday, October 21, 2015

HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, MATHIAS CHIKAWE (Mb) ALIYOTOA KATIKA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 21 OKTOBA, 2015 KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA WIZARA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) wakati wa mkutano uliofanyika leo katika ukumbi wa Wizara hiyo, jijini Dar es salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana,
Kama mnavyojua tarehe 25 ya mwezi huu wa Oktoba mwaka 2015 siku ya Jumapili katika nchi yetu kutafanyika Uchaguzi Mkuu kwa ajili ya kuchagua rais, wabunge na madiwani zoezi ambalo litawashirikisha watanzania wote waliojiandikisha kupiga kura kwa mujibu wa sheria.

Zoezi hili kwa mujibu wa sheria za uchaguzi litasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi yaani NEC kama ambavyo imekuwa ikifanyika katika chaguzi mbalimbali zilizopita ama kuwahi kufanyika katika nchi yetu.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inalo jukumu kubwa la kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao unaimarishwa kabla, wakati na baada ya zoezi hilo la Uchaguzi Mkuu katika maeneo yote ya nchi yetu, ili wananchi waweze kuwa salama na kuendelea na maisha yao ya kila siku.
Ndugu Waandishi wa habari,
Kumekuwepo na taarifa mbalimbali za vitisho zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na hata mitaani na watu wasio na nia njema kwa taifa letu,  zikiwataka wananchi wanunue mahitaji yao mbalimbali ikiwemo vyakula na kuvihifadhi kwa ajili ya kuja kuvitumia wakati na baada ya uchaguzi kwa ubashiri wa kuwepo kwa vurugu wakati ama baada ya uchaguzi.

Taarifa hizi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na mitaani kwa ujumla ni taarifa potofu ambazo zinalenga kuwajengea wananchi hofu na mashaka, wasiwasi na vitisho pasipo sababu zozote zenye tija kwa taifa letu.
Ndugu zangu Waandishi wa habari,
Nitoe rai kwa Raia wote waishio hapa nchini yaani Watanzania na Wageni kupuuza taarifa zote zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na mitaani kwa kuwa taarifa hizo si za kweli, na wala hazilengi kulinda amani iliyopo nchini kwetu.  

Pamoja na hayo kumekuwa na matamko kwa baadhi ya wanasiasa katika kampeni zao kudai kuwa Serikali itasitisha posho za askari mara baada ya Uchaguzi Mkuu,  Taarifa hizi si za kweli kwani Posho za Vyombo vyote vya dola   vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi  ni za kudumu kama ilivyoelekezwa katika waraka wetu, hazitafutwa wala kubadilika na iwapo zitabadilika ni kwa kupandishwa na wala si kufutwa.

 Nawaomba wananchi wote watii sheria  za nchi na zile  za Tume ya Uchaguzi zinazoongoza Uchaguzi Mkuu sambamba na kufuata Maelekezo yatakayotolewa na Tume hiyo kabla, wakati na baada ya kupiga kura jambo litakalosaidia kuilinda amani ya nchi yetu, kwani kila Mtanzania anao wajibu wa kuilinda amani kwa kufuata sheria za nchi bila kushurutishwa.

Wananchi wanapaswa kutambua kuwa baada ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu maisha ya watanzania yanapaswa kuendelea kama kawaida hivyo itikadi zao za vyama vya siasa zisiwatofautishe na kuwajengea chuki, uhasama ama uadui kwani watanzania ni wamoja na wamekuwa wakiishi kwa amani, umoja na ushirikiano katika kuendeleza taifa hili.

Ndugu waandishi wa Habari,  
Wananchi hawapaswi kuwa na hofu yoyote kwa kuwa Serikali ya awamu ya nne ambayo imeongoza na kuwatumikia wananchi kwa kipindi cha miaka kumi  inakusudia kwa dhati kukabidhi madaraka kwa serikali iyajo ya awamu ya tano katika hali ya amani na utulivu.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama inawahakikishia wananchi kuwa itahakikisha hali ya amani na utulivu inakuwepo na kuimarishwa kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu mpaka pale ambapo Uongozi wa  serikali ya awamu ya  tano utakapoingia madarakani.

Wananchi watoe taarifa Polisi pale watakapoona  kuna dalili za uvunjifu wa amani  kwa kupiga simu ya bure namba 112.

Nawashukuru kwa kunisikiliza, Asanteni .
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.


No comments:

Post a Comment