Friday, October 23, 2015

ELIMU YA STADI ZA MAISHA KUOKOA KUNDI KUBWA LA VIJANA WALIO NJE YA SHULE

Afisa vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Godfrey Massawe (aliyesimama) akifuatilia majadiliano ya wawezeshaji kitaifa wakati wa kazi za kikundi kwenye Mafunzo ya Uwezeshaji wa Stadi za Maisha yaliyofanyika Kanda ya Ziwa.

Na: Genofeva Matemu - Maelezo
ILIGUNDULIKA kuwa ulimwenguni kote na hususan nchini Tanzania, Vijana walio nje ya shule ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari ya magonjwa yanayoenea kwa njia ya ngono, VVU na UKIMWI kwa kutokuwa na taarifa na stadi za kuwaongoza hivyo kupoteza kundi kubwa la vijana ambalo ni taifa la kesho.

Ufumbuzi wa tatizo hili umeweza kufanyika kwa kuwapa vijana stadi za maisha zenye upeo mpana wa maarifa na stadi zinazoweza kuwasaidia vijana kuendana na mazingira shindani yanayobadilika.

Stadi za maisha ni moja kati ya mikakati iliyobainika kuleta mabadiliko ya tabia za mtu. Stadi hizi uhusisha stadi na uwezo wa kujenga tabia njema ili kuepukana na matatizo yaliyopo katika maisha ya kila siku.

Mkabala wa stadi za maisha unalenga katika kuendeleza na kukuza stadi zinazoitajika katika mahitaji ya maisha ya kila siku kama vile mawasiliano, kufanya maamuzi, fikra, kuhimili mihemko, uthubutu, ujenzi wa kujiamini, kuzuia shinikizo rika pamoja na mahusiano.

Mkabala huu pia unashughulikia ukuaji wa mtu ili awe na stadi za kumwezesha kutumia aina zote za taarifa kuhusiana na masuala kama vile magonjwa ya ngono, VVU na UKIMWI.
Mahitaji ya stadi za maisha miongoni mwa vijana ni mengi na yanatofautiana baina ya vijana wadogo na wakubwa, vijana walio nje ya shule na walio shuleni, pamoja na walio na wasio katika ndoa hivyo kupelekea kuwa na viwango vya mafunzo ya stadi za maisha vilivyopendekezwa na kubuniwa kuwanufaisha vijana wasio mashuleni.

Wizara inayosimamia masuala ya vijana imekua ikitoa mafunzo ya stadi za maisha kwa vijana walio nje ya shule ili kuwapa vijana stadi za kukabiliana na changamoto za kila siku katika maisha yanayowazunguka.

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) wameweza kufikisha elimu ya stadi za maisha kwa wawezeshaji wa kitaifa kutoka kanda ya Ziwa hivi karibuni ili kuweza kusambaza elimu hiyo kwa vijana walio nje ya shule maeneo yote ya kanda ya ziwa hivyo kuwawezesha vijana kukabiliana na dunia hii ya sasa ya sayansi na teknolojia.

Akifungua mafunzo ya wawezeshaji kitaifa kutoka kanda ya Ziwa yaliyofanyika Mkoa wa Mwanza hivi karibuni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Sihaba Nkinga aliwataka wawezeshaji kitaifa wa stadi za maisha kuwasaidia vijana kujitoa katika mitazamo hasi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwani vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hili.
“Vijana wakijiimarisha katika shughuli za kijamii na kiuchumi wataepuka kuzungukwa na vihatarishi vya maisha kama vile VVU na Ukimwi, mimba zisizotarajiwa pamoja na dawa za kulevya hivyo kujenga nchi kwa kutumia nguvu kazi ya vijana” alisema Bibi. Nkinga.
Mafunzo ya stadi za maisha yamekua yakiongeza hali ya kujiamini kwa vijana na kutoa mbinu za kukabiliana na matatizo ya maisha kwa kuwapa vijana uwezo wa kutumia muda wao kikamilifu kuzungumza na watu wasiowajua kuliko ilivyokua hapo awali.
Aidha Bibi. Nkinga alisema kuwa matarajio ya serikali ni kuona vijana wa kitanzania  wanajitambua kua wao ni nani, wanaenda wapi, na watafikaje kwa kujua uwezo na udhaifu binafsi walionao ili  waweze kupanga malengo waliyonayo na kuyatekeleza kulingana na fursa zilizopo.

Vijana wanaopata fursa ya kuwezeshwa katika stadi za maisha wameongeza viwango vyao vya stadi za kujitambua na uwezo wa kuwasiliana na watu wa rika zote hivyo kubadili tabia za vijana wa rika mbalimbali.

Mkurugenzi Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. James Kajugusi amesema kuwa kila kijana ana sifa za kujiunga na mafunzo ya stadi za maisha zitakazowawezesha kukataa visingizio kama vile umasikini, maradhi na masuala yanayoshauriwa na marafiki ambayo yanaweza kuwaingiza katika vishawishi.

Bw. Kajugusi amesema  kuwa Mafunzo ya stadi za maisha yamelenga kupata waelimishaji wa kitaifa wa stadi za maisha watatu kutoka kila mkoa katika mikoa yote ya Tanzania bara ambao watawafikia waelimishaji rika wa kila mkoa ili kuweza kufikisha elimu waliyoipata kwa vijana wa rika mbalimbali katika Mikoa, Wilaya, kata, vijiji, vitongoji, mitaa, vijiwe na sehemu rasmi za shughuli za vijana.

Stadi za maisha zinaweza kuwekwa katika makundi matatu ambayo ni stadi za maisha kwa ajili ya kujitambua, kwa ajili ya fikra na kwa ajili ya mahusiano baina ya watu hivyo kwa pamoja aina hizi huweza kutoa majibu kwa vijana kuwa wao ni nani, wanataka kwenda wapi na watafikaje hapo wanapotaka kwenda.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bibi. Susan Ndunguru amesema kuwa vijana waliopata mafunzo ya uwezeshaji wa stadi za maisha ni mabalozi ambao kama watatumia vizuri uwezo walioupata katika mafunzo hayo watabadili fikra za vijana wengi nchini hivyo kuweza kujenga taifa lenye afya nzuri, weledi pamoja na ujuzi.
Stadi za maisha humjenga kijana kufanya maamuzi sahihi hivyo kuondokana na majuto na kumfanya kuwa huru katika kutoa maamuzi binafsi.

Kwa kawaida stadi za maisha humpa kijana mwitikio wa uthubutu unaompa fursa ya kusimamia anachotaka au anachoamini bila kumdharau au kuumiza kihisia mtu mwingine.
Mtaalamu wa masuala ya Stadi za Maisha Bw. Benny Lugoe amesema kuwa  wawezeshaji wa kitaifa waliopata Mafunzo ya Stadi za Maisha wana ari na motisha ya kujifunza na kama wataendelea kuwa na ari hiyo watakua wabunifu na wawezeshaji wazuri kwa vijana ndani ya jamii wanazoishi.

Aidha Mwezeshaji wa Kitaifa wa Stadi za Maisha kutoka Mkoa wa Shinyanga Bw. Ezra Manjerenga amesema kuwa vijana wa Mkoa wa Shinyanga wamekua wakikabiliwa na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi hivyo ugeni wa mafunzo ya stadi za maisha katika Mkoa huo utawavutia vijana wengi jambo ambalo litapelekea kutimiza lengo la serikali kufikisha mafunzo hayo kwa vijana wa rika mbalimbali.

Stadi za maisha zinatoa fursa kwa vijana kupata taarifa za afya ya uzazi na upatikanaji wa huduma ya afya ya uzazi, pia humpa kijana haki ya kutambuliwa, kusikilizwa na kuheshimiwa utu wake bila kujali kiwango cha elimu, hadhi yake au sifa nyingine itakayombagua na kumuweka katika mazingira hatarishi.

Vijana waliopata mafunzo ya stadi za maisha wamepewa dhamana na serikali kwenda kuwatumikia vijana na kuhakikisha kuwa uhamasishaji wa mabadiliko chanya miongoni mwao ili kuweza kuachana na tabia zote hatarishi na kushiriki vyema kwenye shughuli za uzalishaji mali.

Serikali inatambua kuwa vijana ni rasilimali muhimu kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na kwa ajili ya maendeleo ya nchi kwa ujumla hivyo kusimamia kwa ukaribu zaidi elimu ya stadi za maisha kwa vijana wote nchini. 


No comments:

Post a Comment