Tuesday, September 1, 2015

MWASITI AWATAKA WASANII WABADILIKE NA WAZINGATIE MAADILI WAWAPO JUKWAANI

  Msanii wa Reggae Princes Delyla akiongea na wadau wa Sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii kwenye makao makuu ya Baraza hilo Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Msanii Mwasiti Almas na Afisa Sanaa kutoka BASATA Augustino Makame.
  Msanii wa kizazi kipya Mwasiti Almas(katikati) akisisitiza jambo wakati akiongea na wadau wa Sanaa kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linalofanyika makao makuu ya Baraza hilo Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Msanii wa reggare Princes Dalyla na Afisa Sanaa kutoka BASATA Augustino Makame.
  Mtafiti na Msanii wa Reggae Innoncent Nganyagwa akifafanua jambo kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii. Kulia kwake ni Msanii mwenzake wa Reggae Princes Delyla. 
 Msanii Mwasiti akisakata muziki sambamba na mashabiki wake kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA.
 Msanii Princes Dalyla akitoa burudani kwa wadau wa Jukwaa la Sanaa la BASATA mapema wiki hii
  Sehemu wa wadau wa Sanaa waliohudhuria Jukwaa la Sanaa wiki hii wakifuatilia kwa makini burudani.


NEWS RELEASE
MSANII mahiri wa muziki wa kizazi kipya Mwasiti Almas amewataka wasanii wenzake kuwa wabunifu katika kutanua mianya ya kujiingizia kipato na kuhakikisha wanazingatia maadili wawapo jukwaani ili kulinda hadhi zao.

Mwasiti ameyasema hayo mapema wiki hii wakati akijibu maswali ya wadau wa Jukwaa la Sanaa linalofanyika kwa mwezi mara mbili ziku za Jumatatu makao ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ilala Sharif Shamba.

Wadau hao wa Sanaa walitaka kujua ni kwa nini wasanii wengi hufilisika mara wanaposimama kufanya shughuli za Sanaa na wengine wamekosa ubunifu wawapo kwenye maonesho au wanapozalisha kazi zao hali ambayo inawafanya watumie sehemu za siri za miili yao katika kutafuta mvuto kwa mashabiki.

“Wasanii wengi wanang’ang’ania kwenye sanaa pekee. Hawawekezi kwenye miradi mingine. Kuwa na umaarufu si kuwa na fedha bali umaarufu ni njia tu inayokusaidia kuingia kwenye sekta na miradi mbalimbali kwa ajili ya kujiimarisha kimapato” alisema Mwasiti wakati akifafanua suala la wasanii kufilisika mara wanapochuja kwenye Sanaa.

Alizidi kueleza kwamba wasanii waliopo sasa hawana budi kutambua kwamba hawatakuwepo muda wote bali kuna leo na kesho hivyo lazima kuiandaa kesho sasa.

“Umri wa wasanii unaenda, waliopo sasa hawawezi kuwepo kesho kwani kuna wasanii wengi wanaibuka na lazima wapate nafasi. Ni muhimu sana kwa wasanii kuliona hili. Huko nyuma kaka na dada zetu walipata shida ilikuwa ngumu lakini kwa sasa wasanii tunapata kipato na baadhi wanajitahidi kuwekeza” alisema Mwasiti.

Kuhusu wasanii kufanya maonesho yasiyo na maadili, Mwasiti alisema kwamba inasikitisha sana kwani katika hali ya kawaida msanii anayejitambua na kuthamini utu na hadhi yake hawezi akafanya maonesho ya uchi kwani matendo ya wasanii huathiri sana jamii inayowazunguka.

“Matendo yetu wasanii huathiri sana jamii inayotuzunguka. Sisi ni binadamu na tuna leo na kesho. Sipendi siku zijazo watoto wetu waje kuuliza na kushangaa yale tuyafanyayo sasa maana yataendelea kuonekana” alisema Mwasiti.

Katika Jukwaa hilo BASATA lilimwalika Mwasiti na wa msanii mwenzake wa kike Princes Dalyna anayefanya muziki wa reggae ili kueleza historia, changamoto na mafanikio waliyoyapata katika kazi zao za Sanaa.   

No comments:

Post a Comment